Dar es Salaam. Mchakato wa
kupata wagombea urais kutoka vyama vikuu vya siasa kwa ajili ya Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba 25 umeandika historia ya aina yake baada ya vigogo wanne
kujitoa na wengine kuachia nafasi katika vyama vyao ghafla na kuzua
mtikisiko.
Vigogo hao ambao ni gumzo kubwa katika
majukwaa ya kampeni ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa
(2006—2008) na Frederick Sumaye (1995—2005) waliojitoa siku chache baada
ya kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania kuteuliwa na CCM
kuwania urais na kujiunga na Chadema, ambako Lowassa alipitishwa kuwa
mgombea urais akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Kupokewa kwa Lowassa na viongozi wa
Ukawa (Chadema, CUF, NCCR – Mageuzi na NLD), kulitarajiwa kuwapa faraja
wanachama wao lakini kumesababisha mtikisiko mkubwa baada Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu wadhifa wake akidai nafsi
imemsuta na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuachia wadhifa
huo na kutangaza kujitoa katika siasa za vyama huku akianzisha mapambano
makali dhidi ya chama hicho.
Wachambuzi wa masuala ya
siasa nchini wanasema wanasiasa hao waliofanya uamuzi mgumu wamegundua
chama si maisha yao yote, hivyo, wanaweza kuhamia kingine au kustaafu na
bado shughuli za siasa zikaendelea.
Meneja Utafiti na
Uchambuzi wa Sera wa Taasisi ya Hakielimu, Godfrey Bonaventure anasema
uamuzi mgumu uliofanywa na Lowassa na Sumaye unaashiria kukua kwa
demokrasia.
“Mtu anapoamua kuhama, amegundua kuwa chama
si maisha yake yote, anaweza kutafuta sehemu nyingine na kuendeleza
safari yake,” alisema.
Alisema uamuzi waliouchukua
Lowassa na Sumaye ni mzuri kwani umeongeza nguvu upande wa pili jambo
ambalo litakuza demokrasia na kuwasaidia wapinzani kuongeza nguvu na
kuufanya uchaguzi wa mwaka huu uwe wa mchuano mkali.
“Kitendo
cha Lowassa kuhamia Ukawa ni manufaa kwa upinzani kwani wale wanaohama
wanakwenda na wafuasi wao, mbinu za uongozi, wahisani, rasilimali na
nguvu mpya. Hata kama hawatashinda, tayari watakuwa wametengeza sura
fulani ya ushindani,” alisema.
Alisema uchaguzi wa
mwaka huu umekuwa na mchuano mkali kwa sababu ya Lowassa na Sumaye
kinyume na hapo biashara ingekuwa ni ileile.
Kuhusu
kujiuzulu nyadhifa kwa Dk Slaa na Profesa Lipumba, Bonaventure anasema
kwamba kumepunguza kitu ndani ya vyama vyao na upinzani kwa ujumla
ingawa hadhani kama kutaathiri kampeni wala Ukawa.
Created by Gazeti la Mwananchi
Created by Gazeti la Mwananchi
0 comments:
Post a Comment