NA EVANS MAGEGE
MKE wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo(Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, ambaye
amekuwa akitupiwa tuhuma nyingi za kumponza na kumsababishia aibu mume
wake amesema kuwa hajaona jambo lolote lenye maudhui ya kujibu tuhuma
zinazoelekezwa dhidi yake.
Kauli hiyo ya Mushumbusi imekuja siku chache baada ya Askofu wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye Dk. Slaa alimtaja
kama mshenga wa tukio la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kujiunga
na Chadema, kudai ana ushahidi unaoonyesha kuwa mama huyo ndiye chanzo
cha mume wake kuacha siasa.
Mushumbusi ambaye yuko nje ya nchi, alitoa msimamo huo katikati ya
wiki hii wakati akiwasiliana na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya barua
pepe.
Amejipambanua kwa kusema kwamba mafanikio yake yataonekana muda si mrefu hivyo kwa sasa amefunga mikono.
“You will see my fruits bro (utayaona mafanikio yangu kaka). For now my
hands closed (kwa sasa nimefunga mikono yangu,” alisema Mushumbusi.
Awali gazeti hili lilimuomba kufanya naye mahojiano kwa njia ya barua
pepe juu ya mambo yote ambayo yameendelea kuibuliwa dhidi yake hata
hivyo alikataa na kumueleza mwandishi wa habari hizi kwamba amruhusu
aendelee na maisha yake nje ya siasa.
Katika majibu hayo, Mushumbusi alisema majungu na
propaganda anawaachia wahusika na kwamba pamoja na shutuma
zote zinazotolewa dhidi yake bado hajaona jambo lolote lenye maudhui ya
kujibu.
“Baba niruhusu niendelee na maisha ya siasa nje ya siasa.
Majungu, propaganda nawaachia wahusika…sijaona issue (jambo) yoyote
yenye content (maudhui) ya kujibu,” alijibu Mushumbusi.
Mushumbusi alimweleza mwandishi wa habari hii kwamba kwa sasa hana
nafasi lakini zaidi maisha yanamuhitaji hivyo hawezi kupoteza muda wake
kwa vitu visivyomuongezea thamani.
“Am very busy now (sina nafasi sasa). And life is demanding too (na
maisha yananihitaji pia), why should I waste time with things which are
not adding any value in me? Thank you. (Kwanini nipoteze muda kwa vitu
ambavyo haviniongezei thamani yoyote? Asante),”
alisema Mushumbusi. Msimamo huo wa Mushumbusi umekuja zikiwa zimepita
siku chache baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Jesephat Gwajima, kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kujibu
mapigo kwa kusema Dk. Slaa ametekwa na mke wake hivyo
haiwezekani kumtoa.
Katika mkutano huo, Askofu Gwajima alisema tatizo si Dk. Slaa au
Lowassa bali mtu anayechochea matatizo ni Jasephine Mushumbusi ambaye
amemponza mume wake kwa kumshawishi kuachana na Chadema kisa ‘u-first
lady’.
Alisema kwamba, akiwa kama rafiki wa familia hiyo, alijitahidi kutafuta
usuluhishi wa mgogoro uliokuwapo kati ya Dk. Slaa na mkewe lakini jambo
hilo halikufanikiwa kwa sababu Mushumbusi hakutaka kubadili msimamo.
Askofu Gwajima alisema kwamba, Mushumbusi ndiye aliyemuamuru Dk. Slaa
kuacha kazi yake ya ukatibu mkuu wa Chadema. Alitolea mfano sehemu ya
majibu aliyoambiwa na mke wa Dk. Slaa wakati akitatua mgogoro
uliokuwapo:
“Mimi nilishajiandaa kuwa first lady na nilishaandaa biashara zangu huko
nje za nchi hivyo siwezi kubadili msimamo wangu,” alimnukuu.
“Mke wake Slaa ana viashiria vyote vya matendo ya kishetani. Ni dhahiri
kuwa yawezekana Slaa anayofanya yote sio akili zake,banamuendesha
vibaya. Sasa kwa mfano angeteuliwa kuingia Ikulu ingekuwaje nchi hii?”
alihoji Gwajima.
Kabla ya hayo kujiri, wiki iliyopita gazeti hili lilizungumza
na Mushumbusi kwa njia ya simu ambapo alielezea kubeza tuhuma
zote zinazoelekezwa kwake na mumewe. Katika maelezo yake alisema mambo
yote yasemwayo dhidi yao hayako katika fikra zao kwa sababu wanajipanga
kuelekea upande mwingine wa kuwa wawekezaji.
Mushumbusi alifafanua aina ya uwekezaji aliopanga na mumewe kuufanya
baada ya kupewa fedha na marafiki zao ni kujenga shule, hospitali pamoja
na kuwawezesha wanawake wajasiriamali.
Created by Gazeti la Mwananchi
Sunday, 13 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment