Mama Janet Magufuli |
HAIKUWA kazi rahisi kwa Mama Janet Magufuli kuaga walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbuyuni jijini Dar es Salaam aliyoitumikia kwa miaka 18 ya ualimu na miaka mingine saba ya kusoma shule hiyo aliyosisitiza ina historia ya maisha yake, pale alipoaga na kudondosha machozi.
Hafla ya kuagwa kwa Mama Magufuli ilifanywa jana katika shule hiyo iliyopo Oysterbay katika Manispaa ya Kinondoni.
“Nimeona niwaage rasmi, nimekuwa nanyi kwa miaka 18 ya ualimu lakini pia nina historia na shule hii, nimesoma hapa shule ya msingi na watoto wangu wote wamesoma hapa pia,” alisema mke huyo wa Rais John Magufuli, maarufu akiwa shuleni kama Mwalimu Pombe.
Alisema anawaaga jumuiya ya shule hiyo kutokana na nafasi yake hivi sasa katika kumsaidia Rais Magufuli katika kuwatumikia Watanzania, lakini bado ataendelea kuwa mwanajumuiya wa Shule ya Mbuyuni.
Akizungumzia historia ya maisha yake na shule hiyo, Mama Magufuli alisema baba yake mzazi (sasa marehemu) askari Mbizo wa Kituo cha Oysterbay (sio mbali kutoka shuleni) kwa wakati huo, alimuandikisha kuanza elimu ya msingi hapo.
Na wakati huo, mwalimu aliyempokea na kumuandikisha, hivi sasa marehemu, Mwalimu Hatibu, alimwandikisha darasa la kwanza na kuanza kusoma, na kwamba muda wa masomo ulipoisha, baba yake alimfuata na kumrudisha nyumbani.
“Hii shule siwezi kuaga, niliandikishwa darasa la kwanza hapa na baba yangu aliyekuwa askari wa Kituo cha Oysterbay, baada ya kumaliza masomo nilirudi tena kufundisha mwaka 1997, na watoto wangu wote wamesoma hapa, ni vigumu kuaga,” alisema Mama Magufuli kwa majonzi huku akitoa machozi.
Alisema akiwa hapo, alikuwa mwalimu wa somo la Uraia na Historia kwa darasa la tatu na la tano, kazi aliyoifanya kwa miaka 18 hadi mwaka jana katikati alipoomba ruhusa ya kwenda kumsaidia kampeni mumewe, Dk Magufuli.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili shule hiyo ambayo imeingia katika historia kwa kutoa wake wa marais wawili akitangulia Mama Salma Kikwete, Mama Magufuli alisema atazifikisha kwa Rais ili aangalie jinsi ya kusaidia kuzitatua zikiwemo pia changamoto za walimu wa nchi nzima.
Awali, akisoma risala ya walimu, Mwalimu Mkuu Doroth Malecela alisema pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi walioandikishwa kuanza elimu ya msingi na upatikanaji wa ruzuku kwa wakati, changamoto kubwa ni uhaba wa madarasa, matundu ya vyoo na madawati.
Pia fedha za likizo za walimu kutopatikana kwa wakati na tatizo la kutopanda madaraja kwa walimu kwa wakati mara wajiendelezapo kielimu na pia walimu wastaafu kucheleweshewa stahiki zao kwa wakati.
Awali, wakati Mama Magufuli alipoingia shuleni hapo, alipokewa na alikwenda moja kwa moja kwenye Ofisi ya Mwalimu Mkuu kusaini kitabu cha wageni na kisha kwenda ofisi za walimu na kuketi kwenye kiti alichokuwa akitumia wakati akifundisha, kisha akaelekea kwenye jukwaa lililoandaliwa kwa ajili ya hafla ya kuagwa.
Wakimzungumzia Mwalimu Pombe, wanafunzi wa shule hiyo katika risala yao iliyosomwa na Jane Andrew ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba, walisema tangu aondoke hawajala tena makande wala chakula kingine; wakimaanisha kuwa sasa hakuna utaratibu wa chakula bure chini ya elimu bure.
Aidha, walimu waliomzungumzia Mwalimu Pombe, walisema wamesikitika kuondoka kwake kwa sababu ni mwalimu mzuri na mwenye huruma, ukarimu na asiyejikweza.
“Yaani tunasikitika kweli, tutammisi mwalimu mwenzetu, alikuwa hana makundi ni rafiki wa walimu wote, hakuchagua rafiki, wote aliwaona ni marafiki, huwezi sema nani ni rafiki yake zaidi ya mwingine, sote alituona tu wamoja”, alisema Mwalimu Amina Kisenge.
Naye wajina wake, Mwalimu Janet Salakana alisema Mwalimu Pombe alikuwa mmoja wa walimu wenye huruma na alijitoa kusaidia wanafunzi wasiojiweza na mfano mzuri ni kununua baiskeli ya mwanafunzi asiyeweza kutembea mwenyewe kutokana na miguu kukosa nguvu.
Katika wosia kwao, Mama Magufuli aliwasisitiza wanafunzi shuleni hapo kusoma kwa bidii na kuacha tabia ya kuangalia video za usiku zinazooneshwa kwenye vibanda ambazo haziwajengi kimaadili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda aliyemkaribisha Mama Magufuli shuleni hapo, alisema ili kusaidia sekta ya elimu kuendelea zaidi na kuwapunguzia mzigo walimu, amezungumza na baadhi ya wamiliki ya mabasi ya abiria ya jijini ili kutowatoza nauli walimu na kuwapa kipaumbele kuwahi kazini.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment