Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zuberi Ally.
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imethibitisha
kutokea kwa vifo vya mahujaji Watanzania wanne, waliokufa wakati
wakishiriki ibada ya Hijja, iliyofanyika Makka, Saudi Arabia juzi.
Taarifa ya wizara hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana,
ilieleza kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, umeeleza kuwa
mahujaji hao walikufa kutokana na msongamano mkubwa wa watu uliotokea
kwenye eneo la Mina.
Miongoni mwa waliokufa na kutambuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo ni
Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla,
huku taratibu zikiendelea kuchukuliwa kutambua mwili wa Mtanzania wa
nne.
“Ubalozi unaendelea na jitihada za kupata jina la Mtanzania mwingine
aliyekufa kwenye tukio hilo. Aidha, Serikali ya Saudia imeahidi kutoa
taarifa kamili, ikiwemo idadi ya watu waliokufa na majeruhi na nchi
wanazotoka mara itakapokamilika,” ilieleza taarifa hiyo.
Mbali na Watanzania hao wanne, taarifa hizo zimeeleza kuwa kuna
mwingine aliyetokea nchini Tanzania na kufa katika tukio hilo, Fatuma
Mohammed Jama, ambaye imebainika ni raia nchi jirani ya Kenya. “Mtu
mwingine aliyekufa ni raia wa Kenya anayeishi nchini, ambaye
ametambulika kwa jina la Fatuma Mohammed Jama,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini humo, kwa
kushirikiana na taasisi zinazoshughulikia masuala ya Hijja za Tanzania,
ikiwemo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na mamlaka za Serikali
ya Saudi Arabia, wanaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua endapo
kuna vifo na majeruhi wengine kutoka Tanzania.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imewaomba wananchi kuwa watulivu
katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali ikiendelea kufuatilia.
Rambirambi za Rais Kikwete Kwa upande wake, Rais Jakaya Kikwete
ametuma salamu za rambirambi kwa Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin
Abdulaziz Al Saud kutokana na vifo vya zaidi ya mahujaji 700
vilivyotokea juzi.
“Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud, nimesikitishwa na taarifa ya
vifo vya zaidi ya mahujaji 700 na wengine 800 kujeruhiwa Alhamisi
Septemba 24 mwaka huu katika msongamano wa watu uliotokea nje ya mji
mtakatifu wa Makka, wakati mahujaji hao wakikamilisha Hija yao.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na
Watanzania, natoa salamu zangu za rambirambi kwako, kwa Wasaudia na
familia za mahujaji wote. “Familia yangu na Watanzania wanawaombea kwa
Mungu marehemu wote ili roho zao zipumzike mahali pema peponi na
kuwaombea subira kwa familia za mahujaji dunia nzima,” alieleza Rais
Kikwete katika salamu zake kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa.
Mufti Akizungumzia hali hiyo katika taarifa yake iliyotumwa kwa
vyombo vya habari jana, Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakari Zuberi, aliye
katika eneo la tukio Saudi Arabia, alisema majina ya Watanzania
waliokufa katika tukio hilo, yamepatikana baada ya miili yao kukutwa na
vitambulisho vyao.
Kwa mujibu wa Mufti Zuberi, mbali na taarifa za vifo vya Watanzania
hao wanne na Mkenya mmoja, pia kulikuwa na taarifa za majeruhi ambao
baadhi alionana nao baada ya kutoka hospitalini.
Pia alisema ameagiza maofisa wa Bakwata alioambatana nao huko,
kufuatilia habari za mahujaji wa Kitanzania katika hospitali mbalimbali
na sehemu za kuhifadhia maiti, ili apate uhakika wa usalama wa mahujaji
kutoka Tanzania.
Mufti Zuberi amewaomba ndugu na jamaa wa mahujaji kuwa watulivu na
kuwa na subira katika wakati huu mgumu, kwa kuwa Serikali ya Saudi
Arabia inaendelea na kazi ya kutambua uraia wa kila mwili ili watoe
taarifa na hivyo wakati wowote taarifa zaidi zitatolewa.
Wakati huo huo, Mroki Mroki anaripoti kuwa mashirika ya kimataifa
yamemnukuu Waziri wa Afya wa Saudi Arabia, Khalid al- Falih, akisema
kuwa vifo vya mahujaji zaidi ya 710 vilivyotokea huko Makka, vimetokana
na mahujaji hao kutozingatia maelekezo ya mamlaka husika.
Taarifa iliyotolewa na kuchapishwa katika tovuti ya Waziri huyo,
ilielezea kuwa uchunguzi utafanyika kubaini chanzo cha vifo vya mahujaji
hao ambao havijawahi kwa zaidi ya miaka 25.
Mahujaji wapatao 717 wamepoteza maisha na mamia wengine wamejeruhiwa
baada ya kukanyagana katika mji wa Mina, nje kidogo ya Makka, ambapo
watu zaidi ya 2,000,000 wanaswali ibada ya hija.
Watu takriban 863 walijeruhiwa huku wengine wakikwama, wakati wa
mkusanyiko huo mkubwa wa kila mwaka wa mahujaji kutoka sehemu mbalimbali
duniani. “Uchunguzi utafanyika juu ya tukio la kufa mahujaji katika mji
wa Mina.
Tunadhani baadhi ya mahujaji walianza kutembea bila kupata maelekezo
kutoka kwa wahusika maalumu wa kuwaongoza. Uchunguzi utakuwa wa haraka
na tutatoa matokeo yake mapema,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Falih alisema majeruhi watatibiwa katika hospitali zilizopo Makka na
ikitokea ipo haja ya kuwapa rufaa majeruhi hao, basi watatibiwa katika
hospitali mbalimbali nchini humo. Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa
Saud Arabia ameagiza kuangaliwa upya kwa utaratibu wa Hija baada ya
tukio hilo.
Katika tukio hilo, makundi makubwa mawili ya mahujaji yaligongana
wakati yalipokutana Mina, yakielekea “kumrushia mawe shetani” kwenye
nguzo saba zijulikanazo kama Jamarat, kilometa chache Mashariki mwa
Makka. Ilielezwa kuwa matokeo ya uchunguzi huo, yatakabidhiwa kwa Mfalme
Salman, ambaye atayatolea maamuzi stakihiki.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudia kupitia kwa msemaji wake, Meja
Jenerali Mansour al-Turki alisema mvutano baina ya makundi hayo mawili
makubwa na hali ya joto kali, vinaweza kuwa chanzo cha vifo hivyo.
Hujaji kutoka Kenya, Isaac Saleh alisema anaitupia lawama serikali ya
Saudi Arabia kwa kushindwa kusimamia vyema mkusanyiko huo wa Hija hadi
kusababisha vifo. “Naweza kuilaumu Serikali ya Saudia kwa tukio hili, na
tayari watu watatu katika kundi langu wamepoteza maisha huku wengine
hatujui walipo,”alidai Saleh.
Rahman Shareef, pia kutoka Kenya alisema, “Jamarat leo pako shwari.
Nilikuwa na hofu hapo jana (juzi) lakini nashukuru nipo salama na
naamini hata familia yangu inaniona niko salama.” Nchi za India,
Indonesia, Pakistan na Netherland, zilithibitisha kuwa baadhi ya
mahujaji wake wamekufa.
Uturuki iliarifu kuwa mahujaji wake 18 hawajulikani walipo. Navyo
vyombo vya habari vya Morocco, vimeripoti kuwa mahujaji wake 87 ni
miongoni mwa waliopoteza maisha.
Created by Gazeti la HabariLeo
Saturday, 26 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment