* Tume ya Uchaguzi yakana tuhuma za Freeman Mbowe
* Dk. Magufuli asema CCM haiwezi kung’oka kama jino
* Lowassa aonya asema kuyakataa mabadiliko ni kujiandalia tabu
Na Waandishi Wetu
WAKATI zikiwa zimebaki siku 26 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu,
kampeni za wagombea urais zinaonekana kushika kasi katika mikoa
mbalimbali nchini.
Wakati vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
vikisema mwisho wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umewadia, mgombea wa chama
hicho Dk. John Magufuli amesema CCM haiwezi kung’oka madarakani kama
jino.
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliibua tuhuma dhidi ya
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akisema kitendo cha wakurugenzi wa tume
hiyo kuhamishwa ni mkakati wa kutaka kuibeba CCM.
Hata hivyo tume hiyo ya uchaguzi imekanusha madai hayo na kusema
hakuna mtumishi wake aliyehamishwa kwa ajili ya kutaka kuhujumu uchaguzi
wa mwaka huu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Luvuba
alisema hadi sasa hakuna mkurugenzi yeyote aliyehamishwa tofauti na
mabadiliko yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika nafasi ya
Mkurugenzi wa Uchaguzi kwa kumteua Julius Malaba kuwa jaji.
“Nakwambia ndugu yangu, Mbowe na Chadema waache
kutapatapa…wanaingilia utendaji kazi wa tume na Serikali, nawaomba
wasiendelee kupotosha umma.
“Hii si mara ya kwanza kuibuka na madai haya, wanazungumzia wizi wa
kura kila siku, waiachie tume ifanye kazi zake, hakuna wizi wa kura
wowote ule tunaongozwa na sheria za nchini,”alisema Jaji Lubuva.
“Nipo njiani natoka Arusha, nimekutana na wanasheria wa nchi jana
(juzi) na pale alikuwapo kiongozi mmoja wa Chadema akawa anazungumzia
malalamiko haya haya…nikamwambia ndugu yangu mbona hakuna kitu kama
hicho.
“Pamoja na kulalamika hivyo, wenzake wa vyama NCCR-Mageuzi,CUF
walikuwapo, jamani hatuna haya mambo, nawaomba tena wasiendelee
kupotosha umma… si si mata ya kwanza kutoa madai haya,”alisema Jaji
Lubuva.
Kuhusu madai ya Mbowe kwamba kuna kura feki ambazo zimeanza kusambazwa mikoani, Jaji Lubuva alisema hakuna kitu kama hicho.
“Kila siku nawasikia wanasema wanataka kulinda kura, huku ni
kutapatapa tu…sasa sikia wanasema kuira zimepelekwa mikoani hakuna kitu
hiki…nasema kwa kujiamini hakipo,”alisema.
Kauli ya Jaji Lubuva, imekuja muda mfupi baada ya Mbowe ambaye pia ni
mgombea ubunge Jimbo la Hai, kuibua tuhuma hizo katika mkutano wa
hadhara mkoani Kilimanjaro.
Katika madai yake, Mbowe alisema wakurugenzi wote katika tume ya
uchaguzi wameondolewa na kuwekwa maofisa wengine kutoka taasisi za
kijeshi kwa lengo la kutaka kuhujumu uchaguzi.
Mbowe
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Himo
Polisi mkoani Kilimanjaro katika Jimbo la Vunjo, Mbowe alisema mbali na
kubadilisha viongozi hao, lengo ni kuiba kura na tayari Serikali imeanza
kutawanya kura kwenye mikoa mbalimbali nchini.
“Mtu mwenye wajibu wa kisheria wa kusimama uchaguzi ni NEC baada ya
CCM kuona Lowassa (mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa), anashinda
wameamua kuandaa mazingira ya kuchakachua tume yenyewe.
“Mkurugenzi wa Uchaguzi, Malaba (Julius) walianza kumwondoa yeye
mwezi mmoja uliopita wakaleta mwingine, wiki mbili zilizopita
wakurugenzi wote wamewang’oa na kuwaingiza wengine wa mwisho kuondolewa
alikuwa mkurugenzi wa idara ya Tehama, inayoshughulika na daftari la
kudumu la wapiga kura.
“Wameanza mkakati mwingine wa kutengeneza kura bandia na tayari zimepelekwa mkoani Kilimanjaro,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe alisema hakuna mkakati wowote ovu utakaopangwa na
CCM bila wao kuujua kwa sababu kila wanachokipanga asubuhi, wao
wanakipata mchana.
Alisema mabadiliko ambayo Ukawa unayapigania, yanamgusa kila
Mtanzania bila kujali dini yake wala kabila lake hivyo ni vigumu mtu
kujaribu kuyahujumu.
Alisema vingozi kama mgombea ubunge Jimbo la Vunjo, James Mbatia
(NCC-Mageuzi), wana mchango mkubwa na kazi ya kuendelea kufanya kwa
ngazi ya taifa ili kuhakikisha mabadiliko hayo yanatokea.
“Tumekuja hapa viongozi wote kwa sababu ya kazi kubwa anayofanya
Mbatia kitaifa, mabadiliko tunayozungumza si kwa faida ya yake wala
Lowassa ( Edward) ni kwa faida ya Watanzania wote,” alisema Mbowe.
“Nyie ni kati ya watu wachache mliyepata mgombea ambaye hata taifa
linamhitaji, huu ni mwaka wa mabadiliko, mimi nilikuwa CCM, Lowassa na
viongozi wengine wametoka ili kuleta mabadiliko, katika mfumo wa vyama
vingi kama chama hakijatekeleza walichoahidi lazima kitoke madarakani,”
alisema.
Msemaji wa JWTZ
Naye Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kanali Ngamela
Lubinga alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema hayana ukweli wowote.
“Siwezi kukupa majibu siko sehemu nzuri, lakini madai haya
yalishatolewa ufafanuzi na tume yenyewe kupitia Elius Malima,”alisema
Kanali Lubinga.
Lowassa naye anena
Kwa upande wake, mgombea urais wa Ukawa kupitia Chadema, Edward
Lowassa alisema ameamua kuwania nafasi hiyo kwa sababu anauchukia
umasikini na CCM imeshindwa kulitatua kwa miaka 50.
“Miaka 50 ya CCM ni shida, nagombea urais kwa sababu nachukia
umasikini, umasikini ni ujinga, siutaki, nitaanza na eneo la elimu,”
alisema.
Akiwa Kahe, Lowassa alisema endapo wananchi watashindwa kufanya mabadiliko na kurudi kwenye maisha ya zamani itakuwa tabu kubwa.
Mbatia
Kwa upande wake,mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia
(NCCR-Mageuzi) pamoja na mambo mengine alizungumzia mdahalo wa wagombea
urais.
“Mdahalo wanaoutaka CCM na lowassa si saizi yake, Dk. Magufuli aje
kwangu nimtoe jasho, namwambia hata kama ni leo jioni aje kwangu nimtoe
jasho. Yeye ni saizi yangu si saizi ya Lowassa,” alisema.
Akiwa Kahe, Mbatia aliwataka wananchi kutumia haki yao ya kupiga kura, kwani hiyo ni haki ya kila mwenye sifa za kufanya hivyo.
“Kama una haki ya kupiga kura, uwezo wa kupiga kura, usipopiga kura, huna haki ya kulalamika,” alisema Mbatia.
Katika hatua nyingine, Mbatia aliawaambia wananchi wa Kahe kuwa
wakimchagua kuwa mbunge, ndani ya siku 14 atahakikisha hospitali ya kata
hiyo inapata umeme.
Alisema suala hilo halihitaji kulisemea bungeni ama kuisubiri serikali ifanye hivyo bali ni jambo la kufanywa na mbunge pekee.
Dk. Magufuli
Naye Dk. Magufuli alibeza kauli za wapinzani akisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakiwezi kung’oka madarakani kama jino.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wake wa kampeni wilayani Mbarali mkoani Mbeya jana.
Alisema anashangazwa na watu wanaotaka CCM ing’oke madarakani na
kueleza kuwa chama hicho hakiwezi kung’oka kirahisi, kwani kina mizizi
kuanzia ngazi ya kijiji.
“Eti kuna watu wanapitapita mitaani wanasema CCM imechoka, lazima ing’oke madarakani.
“Ehee wakae wakijua CCM haiwezi kung’oka kama jino…ndivyo walivyoamua Watanzania wakae wakijua,” alisema.
Kuhusu mgogoro wa shamba la Kapunga kati ya mwekezaji na wananchi,
Dk. Magufuli ameahidi kulirudisha shamba hilo kwa wananchi iwapo
atachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano.
Alisema suala hilo ni kipaumbele chake cha kwanza kama akishinda urais na kuingia madarakani.
Alisema anatambua namna wananchi wanavyohangaika kwa kukosa mahali pa
kuendeshea shughuli za kilimo, wakati mwekezaji kwa kushirikiana na
baadhi ya viongozi wamemega ardhi ya wananchi.
Alisema katika ubinafsishaji wa shamba hilo, mwekezaji alitakiwa
kupewa ekari 5,000 na badala yake amepewa ekari 7,000 kinyume cha
utaratibu.
Alisema mgogoro huo umechukua muda mrefu, kwani aliyekuwa mbunge wa
jimbo hilo, Modestus Kilufi alishindwa kuwasilisha hati za mashamba hayo
serikalini ili hatua stahiki zichukuliwe.
Baada ya kushindwa kura za maoni, Kilufi alijunga na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambako alikaa kwa siku tano, kisha
kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo na kuteuliwa kugombea ubunge wa
Mbarali.
Alisema hayuko tayari kuongoza nchi na kuona wananchi wake wakikosa
eneo la kuendeshea kilimo kwa ajili ya masilahi ya mwekezaji.
“Natambua Igurusi na Mbarali, mmekuwa na kilio kikubwa kuhusu shamba
la mpunga la Kapunga, mwekezaji badala ya kupewa ekari 5,000 amepewa
zaidi ya ekari 7,000.
“Tena katika ekari hizi, zipo 1,800 ambazo ni mali ya wananchi,
ninasema kama mtanichagua nitatumia sheria namba 4 ya ardhi na sheria
namba 5 ya vijiji zote za mwaka 1999, nitafuta hati za shamba hili na
kurudisha kwenu wananchi.
“…unapokuwa rais wa nchi kwa mujibu wa sheria, ardhi yote inakuwa
chini yako, nami nasema hapa nitaifuta hati hii mchana kweupe kikubwa
ninawaomba mnichague,” alisema Dk. Magufuli.
Kuhusu askari wa Hifadhi ya Taifa (TANAPA) katika Bonde la Ihefu
kuwapiga wananchi na kuwafukuza, Dk. Magufuli alisema suala hilo
halitatokea katika uongozi wake.
Created by Gazeti la Mwananchi.
Tuesday, 29 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment