Anna Mghwira ni Mwenyekiti wa kitaifa wa chama
kipya cha siasa, ACT – Wazalendo.Alizaliwa Januari 23, 1959 katika
hospitali ya Mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao
Manispaa ya Singida Mjini.
Baba mzazi wa Anna alikuwa
diwani na kiongozi wa Tanu kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake
alijishughulisha na kilimo na ufugaji na wazazi hawa kwa ujumla walipata
watoto tisa, akiwamo Anna.
Mghwira alianza safari ya
kielimu katika Shule ya Msingi Nyerere Road mwaka 1968 – 1974 akaendelea
na sekondari kwenye Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka 1975 – 1978,
kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya sekondari katika Seminari ya
Lutheran kati ya mwaka 1979 – 1981.
Aliendelea na
masomo ya chuo kikuu mwaka 1982 baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha
Theolojia (Chuo Kikuu cha Tumaini) na kuhitimu Shahada ya Theolojia
mwaka 1986. Mwaka huohuo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) kusomea Shahada ya Sheria.
Kati ya mwaka 1987 na
1998, Anna aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, akifanya kazi
ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu mkubwa. Safari ya elimu ya Mghwira
ilikamilikia Chuo Kikuu cha Essex, Uingereza ambako alianza Shahada ya
Uzamili ya Sheria (LLM) mwaka 1999 na kutunukiwa shahada hiyo mwaka
2000.
Licha ya kuwa mwanasheria na mwanatheolojia
aliyebobea, Anna amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu
katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa, utumishi katika mashirika ya
kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo amejihusisha na masuala
ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za binadamu.
Anna
ana historia ya kupenda siasa, masuala ya jamii na michakato ya
maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko yake mbalimbali katika
majarida na magazeti ya hapa ndani ya nchi.
Safari yake kisiasa
Alianza
siasa tangu wakati wa Tanu akiwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu
(Tanu Youth League) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na
ushiriki wa juu katika Tanu lakini baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza
ushiriki wake ili ajipe muda katika masomo na baadaye ndoa na malezi ya
watoto.
Kwa kipindi kirefu, hakuwa anajihusisha na
siasa hadi alivyoamua kujiunga na Chadema mwaka 2009 ambako alishika
nafasi mbili tu za uenyekiti wa baraza la wanawake ngazi ya wilaya na
katibu wa baraza la wanawake mkoa. Machi mwaka huu alijiunga rasmi na
ACT – Wazalendo na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho,
alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa ACT.
Aliolewa
na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na walibahatika kupata watoto
watatu wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha. Hata hivyo, kwa bahati mbaya,
mumewe hivi sasa ni marehemu.
Mbio za ubunge
Mghwira
alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza Januari 2012 baada
ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo
la Arumeru Mashariki baada ya kifo cha Solomon Sumari.
Alishiriki
kura ya maoni ndani ya Chadema akihitaji kupewa ridhaa. Hata hivyo,
chama hicho kilimpitisha Joshua Nassari (Joshua) na Mghwira alikuwa na
kazi ya kuendelea kumuunga mkono hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama
hicho. Pia, amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki,
kupitia Chadema japokuwa hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.
Urais AC T-Wazalendo
Jambo
la kwanza linalompa nguvu mwanamama huyu ni umahiri wake katika elimu.
Yeye ni msomi nguli wa masuala ya sheria lakini ana shahada tatu za vyuo
vikuu. Nchi yoyote ingependa pamoja na sifa nyingine, iongozwe na Rais
ambaye elimu si kikwazo kwake.
Kwa nchi kama Tanzania
ambayo mfumo dume umewakandamiza wanawake kwa kipindi kirefu, Anna
anakuwa mmoja wa wanawake wachache wenye uwezo mkubwa.
Kwa
sababu Anna ni mwanamke imara na anayepambana kwa muda mrefu sasa.
Kitendo tu cha yeye kuwa mwanamke ni baraka tosha kwa siasa za kisasa
ambazo zinaanza kuchangamkia, kukubali na kutafuta mchango wa wanawake
katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Jinsia yake inampa fursa
ya kuendelea kuaminiwa zaidi katika jamii ambayo inazidi kupoteza imani
na uaminifu wa wanaume.
Anna pia ana uthubutu.
Alipambana na changamoto za ndoa na shule. Wanawake wengi huchagua
kufanya jambo moja na kuacha mengine, yeye alikwenda nayo yote na
kuyakamilisha salama. Uwezo na uthubutu huu vinamfanya kuwa mwanamama
imara anayeweza kukabidhiwa uongozi wa taasisi kubwa.
Pamoja
na kuwa na elimu kubwa, uzoefu wa kutosha wa kukaa nje ya nchi na
kufanya kazi na taasisi za kitaifa na kimataifa, Anna ni mwanamama wa
kawaida sana.
Watu wa karibu naye wanamtaja hivyo. Si
mtu wa kupoteza muda na mambo yasiyo na tija, anapenda kuandika makala
za kuelimisha jamii, kufanya kazi na jamii na kujitolea na kujichanganya
na wananchi wasio na uwezo na wenye kuhitaji msaada. Sifa zote hizi ni
nguvu muhimu kwa binadamu yeyote ambaye anahitaji uongozi mkubwa wa
nchi.
Created by By Kelvin Matandiko in Gazeti leo
Created by By Kelvin Matandiko in Gazeti leo
0 comments:
Post a Comment