Wednesday, 9 September 2015

Tagged Under:

Kila la heri wanafunzi darasa la saba

By: Unknown On: 05:49
  • Share The Gag

  • Wanafunzi wa darasa la saba nchini, leo wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, huku wakiwa na shauku kubwa kufanya mtihani huo kwa kutumia mfumo mpya wa ufanyaji na usahihishaji wa mitihani ambao ulianza kutumika nchini miaka mitatu iliyopita. Mtihani huo ambao utafanyika kwa siku mbili, utahusisha wanafunzi 775,729 ambao walijiandikisha kufanya mtihani huo, kati ya hao wavulana ni 361,502 sawa na asilimia 46.6, huku wasichana wakiwa 414,227 sawa na asilimia 53.4.
    Baraza la Mitihani Tanzania (Nacte), limesema maandalizi ya mtihani huo yamekamilika na kubainisha kwamba utafanyika katika shule 16,096 nchini. Mtihani huo utahusu masomo ya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii, ambapo watahiniwa 748, 514 watajibu maswali kwa Kiswahili na wengine 27,215 watajibu kwa Kiingereza. Mfumo unaotumika katika usahihishaji unajulikana kama ‘Optical Mark Reader’ (OMR), ambao watahiniwa watatumia fomu maalumu za teknolojia hiyo kujibu maswali katika fomu ambazo pia zitasahihishwa kwa mashine maalumu.
    Hata hivyo, Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimekuwa kikilalamika kwamba mfumo huo haufai katika mazingira yetu na kwamba lazima mwanafunzi aonyeshe uwezo wake katika kupambanua maswali na kujieleza. Hoja ya msingi hapa inayojengwa na CWT ni kwamba kutathmini kunakwenda sambamba na kubaini uwezo wa mwanafunzi kujieleza na kuhangaisha akili yake katika kutafuta na kukokotoa majibu na kwamba mfumo huo uliowekwa na Serikali hauna tija kabisa na utasababisha madhara makubwa. Lakini Nacte inasema majaribio ya kutumia fomu hizo yalishafanyika na kwamba mrejesho ulishatolewa kwa wahusika juu ya makosa yaliyojitokeza katika majaribio hayo na namna ya kuyasahihisha. Baraza hilo limeweka msisitizo juu ya umuhimu wa kuwapo umakini zaidi wakati wa mitihani na pia, limesema mpaka sasa mfumo huo umepata mafanikio makubwa na ya kujivunia.
    Sisi tunawatakia watahiniwa wote kila la kheri, hasa tukitilia maanani kwamba miaka saba ya elimu ya msingi ni safari ndefu ambayo inapaswa kuwapa ufahamu na uelewa wa masuala ya ‘elimu dunia’. Ni ngazi muhimu ambayo kila mwananchi anapaswa kuipitia na ndiyo maana Serikali imetoa sera ya elimu ya msingi kutolewa bure.
    Ni katika muktadha huo, tunadhani watahiniwa wengi watafanya vyema katika mtihani huo na kupanda daraja kwa kujiunga na elimu ya sekondari. Ni jambo jema kwamba mwaka huu idadi ya wasichana watakaofanya mtihani leo ni kubwa kuliko ya wavulana. Hayo ni maendeleo makubwa yanayoleta matumaini kwamba wasichana hawataachwa nyuma tena katika masuala ya elimu hapa nchini.
    Wasiwasi wetu ni kwamba mtihani huo unaweza usifanyike katika mazingira ya utulivu, kutokana na kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea kila kona ya nchi. Tungetarajia mamlaka husika kuchukua hatua mapema, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mtihani huo unafanyika katika nyakati tofauti na kampeni hizo zinazoanza asubuhi kila siku au kuahirisha kampeni hizo kwa siku mbili ambazo mtihani huo utakuwa ukifanyika.
    Vinginevyo hatua stahiki na za makusudi zinapaswa kuchukuliwa na Serikali kuhakikisha kampeni hizo haziathiri mitihani hiyo kwa namna yoyote ile. Matumaini yetu ni kwamba mamlaka husika zitadhibiti vitendo vya udanganyifu katika mtihani huo na kuepuka kurudia makosa na kasoro zilizojitokeza huko nyuma.
    Craeted by Gazeti la Mwananchi

    0 comments:

    Post a Comment