Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Fransis Mutungi.
WATANZANIA wametakiwa kujiandaa kisaikolojia kushiriki kikamilifu
kwenye uchaguzi mkuu ujao bila hofu kwa kuwa kura zao zitakuwa salama.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Mwanza hivi
karibuni, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi anasema
wapiga kura hawapaswi kuwa na hofu kwa kuwa uchaguzi utafanyika kwa
usalama.
“Yamezuka maneno kutoka kwa watu wasioitakia mema nchi wakiwatisha
wananchi kuwa kura zao zitaibiwa, nitumie fursa hii kuwaeleza Watanzania
kuwa kamwe kura zao hazitaporwa, zitakuwa salama”, anasema Jaji
Mutungi.
Anafafanua kuwa Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa kuzingatia sheria ambapo
Tume ya Uchaguzi (NEC) imepewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa
sheria za uchaguzi na kuhakikisha unafanyika kwa kuzingatia haki ili
kutimiza demokrasia. “Pia Jeshi la Polisi limepewa dhamana ya
kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na lina jukumu la kulinda
kura,” anasema. Anawataka kuondoa hofu na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi
na NEC wana jukumu zito na la kisheria la kulinda kura hadi matokeo ya
uchaguzi yatakapotangazwa. “
Tusitake kuwaaminisha Watanzania kuwa vyama visivyoweka vikosi vyao
vya ulinzi vitaibiwa kura”, anasema Mutungi. Anasema kwa siku za hivi
karibuni baadhi ya vyama vya siasa viliamua kujiundia vikundi vyao vya
ulinzi kwa lengo la kujilinda, ambapo anakiri baadhi ya vikundi hivyo
hivyo vipo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za vyama vyao, lakini
vimeonesha mwelekeo wa ukiukwaji wa Katiba ya nchi.
Anasema hii ni baada ya vyama hivyo, kuamua kutoa mafunzo makubwa
mazito kwenye vikundi vyao hivyo vya ulinzi mithili ya yale yanayotolewa
kwenye majeshi ya ulinzi katika nchi yetu. Mutungi anasema ingawa
baadhi ya vikundi vya vyama hivyo vipo kwa mujibu wa Katiba za vyama
vyao vinapofundishwa mafunzo ya kijeshi vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 147 inayoeleza kuwa mamlaka
pekee yenye uwezo wa kuanzisha vikosi vya ulinzi ni Serikali.
“Hakuna Chama cha siasa, wala mtu yeyote wala kikundi chochote chenye
mamlaka hayo, isipokuwa Serikali peke yake”, Jaji Mutungi anasisitiza.
Anasema ukweli bado unabaki kwamba hata kama kuna taasisi au kikundi cha
watu au chama kitakachoanzisha kikosi chenye mwelekeo wa kijeshi,
kikundi hicho bado kitakuwa ni batili hata kama ilani na sera za baadhi
ya vyama vya siasa zinaelekeza kufanyika kwa mafunzo hayo.
Anasema ofisi yake ilishaanza kulishughulikia suala hilo, ambapo
anasema ilishatolea ufafanuzi wa hoja hiyo kwa vyama vyote vya siasa
nchini. Amewataka Watanzania na viongozi wa vyama vya siasa nchini
kutolifanyia mzaha jambo hilo la uundaji wa vikundi hivyo vya ulinzi wa
kuwa vinaweza kutumika vibaya na kuvuruga amani ya nchi. Amevitaka vyama
vya siasa kujifunza kutoka nchi jirani za Kongo DRC na Burundi kutokana
na machafuko waliyoyapata baada ya kuunda vikundi vya aina hiyo.
“Nchi jirani kama Congo zilipata machafuko kwa sababu ya vikundi vya
kijeshi ambavyo awali vilipuuziwa katika nchi hizo na baadaye
zilisababisha matatizo makubwa”, anasema Jaji Mutungi. Anavitaka baadhi
ya vyama vya siasa kuacha kuhubiri sera zao huku vikitishia kuwepo kwa
umwagaji damu kwa vitisho hivyo itasababisha wananchi wengi wasijitokeze
kupiga kura Oktoba 25 mwaka huu.
“Vyama vinavyojikita kwenye lugha za vitisho wakati huu wa kampeni,
ikiwemo hoja ya umwagaji wa damu, kama njia ya kupeleka vitisho kwa
wananchi itasababisha wasijitokeze kupiga kura”, Mutungi anaeleza.
Anasema Tanzania imekuwa na tatizo la wananchi wake kutoelewa kwa mapana
mambo mengi ya demokrasia na siasa kutokana na elimu ya uraia nchini
kutowekewa mkazo.
“Hii tumeiona katika kipindi hiki, baadhi ya viongozi wa vyama vya
siasa wanaendesha kampeni siziso za kistaarabu, huku baadhi yao kwa
sababu ya kutokuwa na elimu ya uraia, wanaamini ndizo zinazohitajika”,
anaeleza. Ili kuondokana na tatizo hilo Jaji Mutungi anapendekeza elimu
ya uraia kutolewa mashuleni kuanzia madarasa ya chini ya shule za msingi
na sekondari ili kuanza kuwajengea watoto uzalendo wa kuipenda na
kuifahamu vizuri nchi yao.
Anasema elimu hiyo ikiboreshwa na ikafundishwa kwa vijana wa
Kitanzania itasaidia kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania kuifahamu
vyema nchi yao na wakati mwingine kuwa tayari kuitetea kwenye mambo
ambayo yanaweza kuhatarisha amani. Anaiomba Serikali ihakikishe kuwa
inaboresha mitaala hiyo ili kujenga uelewa kwa wananchi kwa kuimarisha
demokrasia na kufanya siasa za kistaraabu kwa kuzingatia utamaduni wa
Mtanzania, uelewa mpana wa demokrasia na ujenzi wa uzalendo wa nchi.
“Watoto wetu leo hii wanaishia kuangalia picha za nchi za Magharibi
runingani, ni rahisi mtoto kukuambia Rais wa Marekani anaitwa nani
kuliko kumuelezea Rais wa nchi yake, hii ni kwa sababu elimu yetu ya
uraia bado haijawekewa mkazo wa kutosha”, anaeleza. Anasema elimu ya
uraia itakayotolewa izingatie mazingira na utamaduni halisi wa Mtanzania
ikiwa ni pamoja na kuwajenga vijana wa kitanzania kwenye maadili ya
kuthamini utu na tabia njema.
Mutungi amewataka wananchi, vyama vya siasa, viongozi wa dini,
waandishi wa habari na wanasiasa kutambua kuwa wana jukumu kubwa la
kuidumisha na kuienzi amani iliyopo nchini ili uchaguzi wa mwaka huu uwe
wa huru na haki. “Tusikubali kuingia kwenye mitego ambayo inasababisha
machafuko ya kisiasa kama ambavyo tumeona kwenye nchi nyingine ambazo
sasa zinatumia gharama kubwa kurudisha amani…. sisi kazi yetu ni
kuimarisha na kuboresha amani tuliyo nayo maana ndiyo msingi wa mambo
yote, ikitoweka hata uchaguzi wa mwaka huu hautafanyika,” anasema
Mutungi.
Anasema makundi hayo yakiicha amani itoweke yatambue kuwa haiwezi
kununuliwa sehemu yoyote ile duniani bali baadaye hutafutwa kwa gharama
kubwa kwa kutumia fedha za walipa kodi kujenga miundombinu itakayokuwa
imeharibiwa kwa sababu ya kutoweka kwa amani. “Mtu anaweza kununua
chakula lakini hawezi kununua hamu ya kula chakula, hivyo ndivyo ilivyo
kwenye suala la amani pia”, anasema.
Anawataka Watanzania kutokubali kulishwa sumu za jazba ili wavuruge
amani nchini, bali wahakikishe kuwa amani iliyopo hapa nchini inalindwa
na kuenziwa. Anasema baadhi ya watu hapa nchini wamekuwa wakitumia
kuwepo kwa migogoro wakiifananisha na kuvunjika kwa amani, ambapo
anasema migogoro ni sehemu ya kawaida ya binadamu.
“Kuwepo kwa migogoro ndani ya ndoa haimaanishi sasa ndoa haipo,
migogoro imekuwepo na ndoa zimeendelea kudumu”, anasema na kuongeza kuwa
jukumu la kutafuta amani sio la Msajili wa vyama vya siasa peke yake
bali ni la kila mtu katika jamii, Polisi, NEC na wananchi. Anasema
wananchi nao wana nafasi kubwa ya kulinda amani wakati wa uchaguzi
kutokana na wao kuwa na kura ya maamuzi ya kuwachagua viongozi
wanaowataka wao.
“Leo hii Watanzania wakisema chama kinachofanya fujo hatukipi kura,
hakuna chama au mwanasiasa atakayefanya fujo”, anasema. Anawataka
wandishi wa habari na vyombo vyao wafanye kwa kuzingatia weledi na
maadili ya utendaji kazi wao, lakini visijihusishe kwa namna yoyote
katika kukuza migogoro nchini hasa wakati huu wa uchaguzi mkuu.
“Migogoro ikitokea vyombo vya habari visichochee bali viandike
taarifa za kuhamasisha amani ili wananchi wapate fursa ya kushiriki
kwenye shughuli za uzalishaji”, Mutungi anasisitiza. Anasema ofisi yake
itaendelea kufanya kazi kwa usawa ikitoa elimu kwa vyama vyote vya siasa
ili kila chama kiweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 29 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment