SIKU moja baada ya Serikali kutangaza kuwa mahujaji 50 wa Tanzania
waliokuwa katika Mji Mtakatifu wa Makka, Saudi Arabia, hawajulikani
walipo tangu kutokea kwa tukio la kukanyagana na kusababisha vifo vya
watu 769, imesema imepokea majina 18 ya watu ambao hawajulikani walipo.
Katika tukio lililotokea eneo la Mina, nje kidogo ya Makka, Alhamisi
iliyopita ambayo ilikuwa ya maadhimisho ya Sikukuu ya Idd el Haji,
mahujaji watano wa Tanzania waliripotiwa kufa, na wengine kujeruhiwa.
Taarifa ya Serikali kwa vyombo vya habari jana, iliwataja mahujaji wa
Tanzania ambao hawajaonekana kuwa ni Abdul Iddi Hussein, Awadh Saleh
Magram, Burhani Nzori Matata, Yussuf Ismail Yusuf, Saleh Mussa Said,
Adam Abdul Adam na Archelaus Antory Rutayulungwa.
Wengine ni Farida Khatun Abdulghani, Rashida Adam Abdul, Hamida Ilyas
Ibrahim, Rehema Ausi Rubaga, Faiza Ahmed Omar, Khadija Abdulkhalik
Said, Shabinabanu Ismail Dinmohamed, Salama Rajabu Mwamba, Johari
Mkesafiri Mwijage, Alwiya Sharrif Salehe Abdallah na Hafsa Sharrif Saleh
Abdallah Aidha, ilisema mbali ya taarifa za kupatikana kwa majina hayo,
Wizara imepokea taarifa ya kutambuliwa kwa mwili wa mmoja wa Tanzania
anayeitwa Hadija Shekali Mohammed wa kikundi cha Ahlu Daawa.
“Serikali ya Saudi Arabia imetoa picha za maiti za mahujaji waliokufa
Makkah ambao wamehifadhiwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti kwa ajili
ya utambuzi. Hivyo, Ubalozi wa Tanzania nchini humo kwa kushirikiana na
Tanzania Hajj Mission pamoja na vikundi vya mahujaji unaendelea na
zoezi la kuzihakiki picha hizo ili kubaini kama zinalingana na sura za
mahujaji wetu waliopotea.
“Pia Mamlaka ya Serikali ya Saudi Arabia imesema kuwa imechukua alama
za vidole za mahujaji waliokufa ili wazilinganishe na zile
walizozichukua Uwanja wa Ndege wakati mahujaji hao wakiingia nchini
humo.
Wizara inaamini kuwa taarifa za alama za vidole zitakapotolewa
zitasaidia sana kuwatambua mahujaji wetu,” ilieleza sehemu ya taarifa
hiyo. Waanza kurejea Wakati huohuo, kundi la mahujaji 90 kati ya zaidi
ya 3,000 waliokwenda Makka kuhiji kwa lengo la kutimiza moja ya nguzo
kuu za Uislamu, wanatarajiwa kuwasili nchini leo alfajiri.
Idadi hiyo ya mahujaji ni wale ambao walipelekwa huko kupitia Taasisi
ya Haji Caravan, wakati wengine wanatarajiwa kurejea nchini kesho na
keshokutwa. Juzi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
kupitia Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma, ilieleza kuwa
mahujaji wa Tanzania ambao wapo salama, walimaliza ibada yao ya Hija
Jumamosi iliyopita na juzi walitarajiwa kuanza safari ya kurejea
nyumbani.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya mtandao akiwa Saudia,
aliyekuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage ambaye alishiriki
ibada hiyo, alisema msafara huo wa watu 90 wa Taasisi ya Haji Caravan
utafika leo alfajiri. “Sisi ambao tuko salama tutarejea nchini kesho
(leo) alfariji. Tuko 90, ni wa taasisi moja, Haji Caravan. Lakini
wengine watarudi Alhamisi na Ijumaa,” alieleza Rage.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 29 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment