Wednesday, 9 September 2015

Tagged Under:

Gwajima aibua mazito ya Slaa

By: Unknown On: 12:14
  • Share The Gag
  • MCHUNGAJI Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana amejibu mashambulizi dhidi ya tuhuma zilizotolewa
    dhidi yake na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Wilbrod Slaa.

    Septemba mosi mwaka huu, Dkt. Slaa alizungumza na waandishi wa habari na kusema ameamua kuachana na siasa baada ya kushindwa kukubaliana na viongozi wenzake wa CHADEMA juu ya utaratibu
    uliotumika kumkaribisha Bw. Lowassa.

    Bw. Lowassa ndiye mgombea urais wa CHADEMA akiwakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambapo katika mkutano huo alimuita Mchungaji Gwajima 'mshenga' akidai ndiye aliyefanikisha Bw. Lowassa kujiunga CHADEMA.

    Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mchungaji Gwajima alisema, Josephine Mushumbusi ambaye ni mchumba wa Dkt. Slaa, ndiye aliyemshawishi aachane na siasa baada ya chama hicho kukubali kumpokea Bw. Lowassa.

    Alisema Mushumbusi aliamini CHADEMA kingemteua Dkt. Slaa kugombea urais na kushinda katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu hivyo alijiandaa kuwa mke wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.

    Mchungaji Gwajima alisisitiza kuwa, Dkt. Slaa alilazimishwa ajiondoe CHADEMA na Mushumbusi siku ambayo Bw. Lowassa alikuwa akikabidhiwa kadi ya uanachama wa chama hicho.

    "CHADEMA walifanya mkutano wa Kamati Kuu ambao ulihudhuriwa na Lowassa...mimi niliingia katika mkutano huo kama mjumbe mwalikwa au mshenga kama anavyosemwa, wote tulipokewa getini na Profesa Beregu pamoja na Slaa, baadaye tulikaa kikao na kufanya mazungumzo yaliyomalizika   usiku.

    Dkt. Slaa kufukuzwa

    'Ilipofika saa 7.19 nikiwa nyumbani, nilipokea ujumbe mfupi wa maneno katika simu yangu (sms), kutoka kwa mlinzi anayekuwa analinda nyumba ya Dkt. Slaa aitwaye Cornel ambaye hupo hapa.

    "Cornel alisema ilipofika saa 6.20 usiku, alipokea simu kutoka kwa mlinzi wa Dkt. Slaa akimweleza bosi wao wameachana naye maeneo ya Chama akirudi nyumbani na gari anaendesha mwenyewe," alisema.

    Aliongeza kuwa, baada ya kufika nyumbani mlinzi huyo alimpokea mkoba wake anaotumia kuweka kompyuta mpakato, kwenda kumuamsha mkewe ili aweze kumfungulia na alipotoka nje, alimwambia Dkt. Slaa arudi alikotoka na hataki kumuona nyumbani kwake.

    "Cornel aliyasikia maneno hayo yakitoka mdomoni kwa Mushumbusi ambayo yalikuwa yakimdhalilisha Dkt. Slaa na ghafla alitoka na sanduku la nguo na kumtupia nje...Slaa alikwenda kulala kwenye gari hadi asubuhi alipofunguliwa mlango...usiku huo huo nilimtumia ujumbe Gwajima kumwarifu kilichotokea lakini hakunijibu," alisema Cornel.

    Alisema baada ya kupata ujumbe huo, alimpigia simu Dkt. Slaa na kumwambia amepata taarifa kuwa amelala kwenye gari na alimjibu kuwa, kuna mwanaye amejisahau na kumfungia katika gari.

    Mchungaji Gwajima alisema, urafiki wake na Dkt. Slaa ulianza siku nyingi wakati wa harakati za kuiunda CHADEMA iweze kusimama na katika kipindi hicho, Slaa alimwomba ampatie walinzi wanne wa kiroho kutoka kanisani kwake na mpishi Bi. Marcelina Mushi (50) hivyo namfahamu
    Slaa kuanzia jikoni hadi chumbani.

    Alisema walinzi hao walifanya kazi ya ulinzi nyumbani kwa Dkt. Slaa kwa zaidi ya miaka minne, usiku na mchana na aliomba ulinzi baada ya kupata vitisho vingi vya kutaka kuuawa.

    Anamjua vizuri Dkt. Slaa

    Katika hatua nyingine, Mchungaji Gwajima alisema anayajua mambo mengi ya Dkt. Slaa na alivyokuwa akimfahamu zamani si alivyo sasa kwani amebadilika, kuwa muongo akiendeshwa na mchumba wake.

    "Nilimuuliza Dkt. Slaa juu ya mkewe kutaka astaafu siasa naye alikubali kushawishiwa na kuniomba niingilie kati...nilimpigia simu Mushumbusi ambaye alikiri kumpa Slaa masharti mawili likiwemo la Lowassa kama anaingia CHADEMA, Dkt. Slaa aachane na siasa.

    "Nilifanya jitihada za kumuomba Mushumbusi alegeze msimamo wake,
    kuna siku tulikaa Kibo Complex kuanzia asubuhi hadi saa nane mchana lakini alikataa; akiendelea kusema alijipanga kuwa mke wa Rais na tayari alianza maandalizi na wafanyabiashara wa nje," alisema.

    Ndesamburo agonga mwamba

    Mchungaji Gwajima alisema, mjumbe mwingine aliyekwenda kumuomba Mushumbusi abadili msimamo wake ni Mzee Philemon Ndesamburo naye alishindwa na kumtafuta Mchungaji Maxmillian na wenzake ambao nao walimbembeleza abadili msimamo wake lakini alikataa.

    Matatizo ya Mushumbusi

    Alisema Mushumbusi alikuwa na matatizo ya kuanguka na kuzimia kutokana na imani za kishetani hivyo hata kama Dkt. Slaa angechaguliwa kuwa rais, asingeweza kufanya kazi ipasavyo kutokana na matatizo
    ya mchumba wake lakini Mungu ameepusha.

    "Kilichotokea kwa Dkt. Slaa si yeye bali ni mashetani kwani mchumba wake amewahi kudondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataita wa Julius Nyerere mara moja, nyumbani kwake mara mbili na mara zote nilimwombea na mapepo yakatoka," alisema.

    Alikana kuzungumza na Dkt. Slaa juu ya Maaskofu 30 wa Kanisa Katoliki aliodai walihongwa fedha na Bw. Lowassa ili waweze kumchagua hivyo dhamira yake ililenga kuwachafua viongozi wa dini.

    "Slaa anasingizia kuwa Maaskofu 30 walihongwa, lengo lake ni kutaka wasiaminike na kuonekana hawafai, Maaskofu wa Katoliki hawakupewa rushwa wala wa KKKT na mimi pia sikupewa rushwa," alisema.

    Awagusa Usalama wa Taifa

    Mchungaji Gwajima alisema Dkt. Slaa alisema analindwa na watu wa Usalama wa Taifa na kudai hicho ni kitendo cha ajabu na kumuonya pamoja na mkewe akidai wanatumika na Usalama.

    "Nawaomba Usalama wa Taifa walinde nchi ikae kwa amani, wasijiingize kwenye siasa au kulinda kikundi fulani," alisema.

    Alisema kama Dkt. Slaa ataendelea kuwatukana Maaskofu, Mashekhe na viongozi wengine wa dini, atatoa siri nzito ikiwemo watu wanne aliodai alikutana nao nchini Afrika Kusini wakiwa na mizigo yao.

    "Nawaomba viongozi wote wa dini msimjibu Dkt. Slaa kama atatoka kujibu, nitapambana naye na ushenga wangu utatimia siku hiyo na aliyemtuma Dkt. Slaa akome," alisema Mchungaji Gwajima.

    Aliongeza kuwa, Dkt. Slaa si mwadilifu alipokuwa Padre wa Kanisa Katoliki kwani alizaa watoto ambapo urafiki wake na Lowassa ulianza tangu akiwa CCM.

    Created by Gazeti la Majira

    0 comments:

    Post a Comment