NA BENJAMIN MASESE, MWANZA
BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limefanya uchunguzi na
kugundua kuwa Waislamu watamchagua rais asiye na uchungu na nchi yake
kwa sababu hawahudhurii mikutano ya kampeni.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kaimu Mufti wa
Tanzania, Sheikh Haamid Jongo, alisema kutokana na uchunguzi huo,
amewataka Waislamu wote nchini kuhudhuria mikutano ya wagombea wote wa
nafasi ya urais bila kujali ukubwa wake ili kusikiliza sera badala ya
kusubiria kusoma mitandaoni na kusikiliza kupitia vyombo vya habari.
Jongo ambaye hakubainisha jinsi walivyofanya uchunguzi wao, alisema
wamebaini baadhi ya wagombea nafasi ya urais wanataka nafasi hiyo kwa
ajili ya heshima na si kuwatumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo.
Alisema lengo la kuwataka kwenda kusikiliza sera za wagombea urais wa
vyama vyote ni kumpata kiongozi mpenda maendeleo na mwenye moyo
unaofanana na aliyewahi kuwa Rais wa Afrika Kusini, marehemu Nelson
Mandela na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Tanzania ni nchi ya amani na utulivu, hivyo tunataka kiongozi
anayeweza kufanya uamuzi mgumu, sasa tutampata kiongozi huyo kwa kwenda
kusikiliza sera za wagombea majukwaani na si vijiweni, tunahitaji
mabadiliko ya maendeleo na siyo kwenda Ikulu kutafuta heshima ya
kupigiwa mizinga.
“Leo nawalenga Waislamu tu kwa kuwapa wito kwamba wasishangilie
nyimbo za wasanii wanaotembea na wagombea, wasikilize wagombea wenyewe,
kama Bakwata hatuungi kauli za kudai kwamba hakuna kilichofanyika kwa
miaka 54 ya uhuru, yapo yamefanyika kwa kiwango fulani.
“Hizi changamoto zinazotukabili Watanzania ni za kawaida, maana
maendeleo huzaa changamoto, zipo nchi zimeendelea kiuchumi lakini watu
wake wanajinyonga kutokana na kubaliwa na changamoto, Tanzania haipo
peponi kiasi cha kuwaambia Watanzania kwamba akiingia madarakani hakuna
tena umasikini, hakuna mtu anayeweza kumaliza umasikini wa mtu bali ni
kupunguza tu,” alisema Jongo.
Alisema wapo baadhi ya wagombea wa nafasi ya urais wanaonyesha
wanataka nafasi hiyo ili kutafuta heshima, kitendo kinachowapa wasiwasi
Watanzania kutopata kiongozi atakayepunguza changamoto zinazowakabili.
Creted by Gazeti la Mtanzania
Saturday, 26 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment