MGOMBEA Urais wa Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Edward Lowassa, amesema kila Mtanzania anatakiwa kujipima
aone kama anastahili kukipigia kura Chama cha Mapinduzi (CCM).
Amesema maisha ya Watanzania ni magumu na kila mmoja anatakiwa
kumpigia kura yeye pamoja na wagombea wengine wanaounda Ukawa kwa kuwa
wamedhamiria kuboresha maisha ya Watanzania.
Lowassa ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu, aliyasema hayo jana
mjini hapa alipohutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Laini Polisi
mjini Nzega, Mkoa wa Tabora.
“Bado siku 49 muamue kama mnataka kuendelea kuishi bila elimu bora;
bado siku 49 muamue kama mnataka kuishi bila maji; bado siku 49 muamue
kama mnataka kulala kitanda gani hospitalini na vile vile bado siku 49
muamue kama mnataka kula mlo mmoja, miwili au milo mitatu kwa siku.
“Siku hizo zinakuja, tafakarini vizuri, angalieni nyuma tangu TANU
itawale nchi hii hadi CCM ilipoanza kutawala umepata kitu gani?
“Jipimeni, angalieni nyuma kwa nini muendelee kuwa waoga, kwa nini
mfanye uamuzi wa kupiga kura. Nipeni kura zenu nikafanye mabadiliko
katika nchi hii kwa sababu tuko nyuma sana katika maendeleo.
“Mwambieni huyo aliyekopa tumbaku hapa Tabora kwamba nikiingia
madarakani tu ile wiki ya pili atawalipa mara mbili kwa sababu nitaunda
Serikali ya kisasa, sitaki Serikali nyoronyoro, nataka Serikali
inayokimbia.
“Lazima tusonge mbele, hatuna sababu ya kuzidiwa na Wakenya, hatuna
sababu ya kuzidiwa na Wanyarwanda na pia nchi yetu haina sababu ya
kuzidiwa na Waganda,” alisema Lowassa.
SUMAYE: Walioficha fedha nje watazirudisha
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, alisema kama Lowassa
atafanikiwa kuingia madarakani Watanzania walioficha fedha nje ya nchi
watazirudisha.
Kwa mujibu wa Sumaye, fedha hizo ambazo Serikali ya CCM imeshindwa
kuzirudisha zitatakiwa kurudi kwa sababu ni mali ya Watanzania.
“Jana (juzi) mmemsikia Magufuli (Mgombea urais wa CCM, Dk. John
Magufuli), akisema atakapoingia madarakani atarudisha mashamba ya
wananchi yaliyoporwa.
“Kwanza kabisa namwambia Magufuli kwamba Ikulu haingii, lakini sisi
tutakapoingia madarakani tutahakikisha walioiba fedha za Watanzania na
kuzificha huko Ulaya au Uswisi wanazirudisha,” alisema Sumaye.
Sumaye pia alizungumzia suala la rushwa nchini na kusema kama CCM
wangekuwa waungwana wasingemsimamisha mtu yeyote kugombea urais kwa
sababu wameshindwa kuwaletea maisha bora Watanzania.
“Magufuli anasema akiingia madarakani atakomesha rushwa sasa kama ana
uwezo huo kwa nini ameshindwa kuikomesha wakati na yeye ni waziri
katika Serikali iliyokithiri kwa rushwa?
“Magufuli anasema akiingia madarakani atakuza uchumi, kama kweli ana
uwezo wa kukuza uchumi kwa nini ameshindwa kuukuza kupitia Serikali ya
CCM ambayo yeye ni waziri?
“Magufuli hana lolote, msimchague kwa sababu ameshiriki kununua feri
mbovu inayotoka Bagamoyo kwenda Dar es Salaam,” alisema Sumaye.
Katika maelezo yake, Sumaye alizungumzia pia taarifa za viongozi wa
CCM wanaodaiwa kuwatisha wananchi wasimchague Lowassa kwa kisingizio
kwamba nchi itaingia katika vita kama ilivyotokea Libya na katika nchi
nyingine za Afrika Kaskazini.
Sumaye alisema hakuna vita itakayotokea wapinzani watakapoingia
madarakani na kwamba vita hiyo itatokea kama Serikali ya CCM haitataka
kuondoka madarakani.
MBOWE: Ulofa, upumbavu ni kwa sababu ya CCM
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema ili umasikini
unaowakabili Watanzania uweze kuondoka lazima washirikiane kuiondoa
madarakani CCM.
Alisema ulofa na upumbavu wanaodaiwa kuwa nao Watanzania umesababishwa na Serikali ya CCM kwa kuwa haiwajali Watanzania.
Mbowe alisema tofauti zao siasa walizokuwa nazo walilazimika
kuziacha na kuungana wakati wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu lengo
lao ni kuing’oa CCM madarakani.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alilazimika kuwapigisha kura za mikono
wananchi wa Nzega waliohudhuria mkutano huo ili kutatua mvutano wa
wagombea wa ubunge katika Jimbo la Nzega Mjini lililokuwa na wagombea
wawili wa Ukawa.
Wakati wa kura hizo, mgombea wa Chadema, Charles Mabura, aliibuka
mshindi dhidi ya mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Meza John.
Pamoja na mkutano huo, Lowassa alihutubia mikutano mingine ya kampeni katika Majimbo ya Bukene, Sikonge na Igunga mkoani Tabora.
Wakati huo huo, leo Lowassa anatarajia kulisimamisha tena jiji la Dar
es Salaam atakapohutubia mikutano ya kampeni katika Majimbo ya Kawe na
Kibamba.
Lowassa atafanya mikutano hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu Ukawa
walipozindua kampeni zao Agosti 29 mwaka huu katika Viwanja vya
Jangwani.
Created by MAREGESI PAUL, NZEGA in Gazeti la Mwananchi
Monday, 7 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment