Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
anayeungwa mkono na Ukawa, Juma Haji Duni akihutubia mkutano wa kampeni
katika jimbo la Busanda mkoani Geita.
VURUGU zinazoendelea ndani ya umoja wa vyama vinne vya upinzani
(Ukawa), kuhusu kuachiana majimbo na kata baada ya kusambaa katika mikoa
ya Mtwara, Tabora na Kilimanjaro, sasa zimegonga hodi mkoani Morogoro.
Hali hiyo ambayo imevuruga hadi majimbo ya wenyeviti wenza wa Ukawa,
ni tofauti na mtafaruku mwingine unaoendelea ndani ya chama kimoja
katika safu za uongozi wa juu, ambazo zimepewa jina la ‘kushuka njiani
wakati safari ikiendelea’.
Mkoa wa Morogoro una majimbo 11 ya uchaguzi, ambapo CUF katika mgawo
huo ilipewa majimbo mawili ambayo ni Kilosa na Morogoro Kusini Mashariki
na Chadema ikanyakua majimbo tisa.
Morogoro
Akizungumza na gazeti hili mjini Morogoro jana, mgombea wa Ubunge wa
Jimbo la Kilosa, Abeid Mlapakolo (CUF), alisema pamoja na kuwa na
makubaliano hayo, ameshangazwa kuona Chadema imemsimamisha mgombea
ambaye anaendelea kufanya kampeni katika kata mbalimbali zilizomo kwenye
jimbo hilo.
Kwa mujibu wa Mlapakolo, mgombea huyo wa ubunge wa Chadema, Rajab
Msabaha, tayari ameshasambaza mabango na vipeperushi maeneo mbalimbali
ndani ya jimbo hilo na amekuwa akifanya kampeni kinyume na makubaliano
yaliyofikiwa na viongozi wa Ukawa.
Mlapakolo alidai mbali na kupiga kampeni, Msabaha pia alishiriki
katika mapokezi ya mgombea wa urais wa Chadema anayeungwa mkono na
Ukawa, Edward Lowassa alipowasili Kata ya Dumila iliyopo katika Jimbo la
Kilosa Septemba 15, mwaka huu na wafuasi wake kadhaa.
“Jimboni ni vurugu tupu, wafuasi wa Chadema wananivurugia shughuli za
kampeni...mimi ndiye mgombea halali wa Ukawa Jimbo la Kilosa, lakini
ndugu zangu hawa wamemweka mgombea wao wa ubunge,” alisema na kuongeza.
Vurugu hizo zimemkuta pia mgombea wa ubunge wa Jimbo la Morogoro
Kusini Mashariki, Salama Omary (CUF) ambaye amesema licha ya jimbo hilo
kupewa CUF, Chadema nao wamemsimamisha mgombea wa ubunge kinyume na
makubaliano.
Salama alisema bado mgombea wa ubunge wa Chadema, David Lugakingira,
anaendelea kufanya kampeni za uchaguzi licha ya viongozi wake kumtaka
asifanye hiyo.
Hatua
Kutokana na hali hiyo, Mlapakolo na Salama wameamua kuwasilisha
malalamiko kuhusu Chadema kukiuka makubaliano hayo kwa mgombea wa urais
wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia Chadema, Edward Lowassa,
anayeungwa mkono na Ukawa.
Mlapakolo amesema tayari amefikisha suala hilo mbali na
litashughulikiwa na viongozi wa Taifa wa Ukawa, ambao wanatarajiwa kwa
kupeleka timu ya viongozi kwenda kutatua sakata hilo.
Naye Salama amefikisha sakata hilo kwa Lowassa ambaye alidai kuwa
mgombea urais huyo aliahidi kufanyia kazi malalamiko hayo na kufikia
uamuzi wa pamoja wa viongozi wa Ukawa.
Mtwara, Makaidi Mkoani Mtwara tangu mwanzoni mwa mwezi huu, mgombea
ubunge wa Jimbo la Masasi ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk
Emmanuel Makaidi (NLD), alijikuta akikataliwa na wananchi katika vijiji
mbalimbali vya jimbo hilo kila anapopanda jukwaani, huku wengine
wakimzomea wakidai kuwa yeye sio chagua lao.
Dk Makaidi mwenyewe alipoulizwa alikaririwa akisema hawezi kukatishwa
tamaa na kikundi cha watu wachache, kinachopiga propaganda zisizo na
msingi, huku akiwataka wakazi wa Masasi, kuamini kuwa uteuzi wa majimbo
uliofanywa na Ukawa, umezingatia misingi ya makubaliano ya umoja huo.
Akijaribu kuweka mambo sawa, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mtwara,
Kassimu Bingwe, alikaririwa akisema mgawanyo wa majimbo uliofanywa na
uongozi wa Ukawa Taifa, ulitoa ridhaa kwa NLD kuweka wagombea Masasi,
Ndanda na Lulindi na kudai kuwa kinachotokea ni njama za wapinzani.
Hali hiyo ya Masasi, ilisababisha Mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma Duni
Haji, alipotembelea jimbo hilo kushindwa kuhutubia baada ya wafuasi wa
CUF, kupiga kelele za kumkataa Makaidi, huku wakisisitiza kumtaka Ismail
Issa Makombe maarufu Kundambanda, ambaye alikuwa mgombea wa CUF kabla
ya kuondolewa na Ukawa.
*Kilimanjaro, Mbatia
Katika Mkoa wa Kilimanjaro kwenye Jimbo la Vunjo, wagombea udiwani 16
kutoka Chadema, juzi walitangaza kutomuunga mkono mgombea ubunge wa
Vunjo kupitia NCCR-Mageuzi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa,
James Mbatia.
Mmoja wa madiwani hao, ambaye ni mgombea wa kata ya Mamba Kusini,
Fredy Shayo, alisema hali hiyo imetokea baada ya vyama hivyo kushindwa
kuelewana katika makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja, ambapo
Chadema na NCCR-Mageuzi vimesimamisha wagombea wao wa udiwani kwenye
kata zote 16 za jimbo la Vunjo.
Katibu wa Chadema Jimbo la Vunjo, Emmanuel Mlacky alikiri kuwa
mwenendo wa Ukawa katika jimbo hilo haupo vizuri, kwa sababu
unahatarisha uhai wa Chadema pamoja na uhai wa Ukawa.
Mlacky alisema maridhiano ya Ukawa yalilenga kumsimamisha mgombea
mmoja kuanzia ngazi ya urais, wabunge na madiwani ambapo baada ya
makubaliano hayo jina Mbatia liliridhiwa na viongozi wakuu wa umoja wao,
huku ngazi ya madiwani ikiachiwa mamlaka ya jimbo kuona namna ya
kusimamisha wagombea wa udiwani.
Alisema licha ya kukaa kwenye vikao vya maridhiano zaidi ya mara nane
bila mafanikio, lakini viongozi wa NCCR wameona baada ya Mbatia
kupitishwa na Makao Makuu kwa makubaliano, wamefikiri ndio inawapa
nafasi ya kusimamisha madiwani karibia kata zote, jambo ambalo ni
kinyume.
Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, alisema haungi
mkono madiwani wa chama chake kumsusia Mbatia, pia chama chake hakiungi
mkono kubaguliwa kwa wagombea udiwani wa Chadema na mgombea huyo wa
ubunge.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR-Mageuzi, Heme Msabaha
alisema, mambo yanayoendelea yanawapa ishara kuwa huenda Chadema wakawa
wanatumika kwa lengo baya.
Simiyu, Regina
Katika Mkoa wa Simiyu, uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa Jimbo
la Itilima kupitia Chadema, Martine Magire, uliingia doa baada ya
wafuasi wa CUF wakiongozwa na mgombea ubunge wa chama hicho katika jimbo
hilo, Martine Makondo, kuvamia na kufanya vurugu katika uzinduzi huo.
Kutokana na vurugu hizo, mke wa mgombea urais wa Chadema, Lowassa
ambaye alikuwa mgeni rasmi, Regina Lowassa, aliondolewa jukwaani dakika
15 baada ya kuwasili katika uzinduzi huo.
Chanzo cha vurugu hiyo, ni mgombea huyo wa CUF aliyeingia katika
uzinduzi huo akiwa amebebwa na wafuasi wake, kudai kuwa amehujumiwa na
mgombea wa Chadema na kusababisha jina lake likatwe na Kamati Kuu ya
chama chake.
Kamanda wa Polisi wa Simiyu, Gemin Mushy, alikaririwa akisema askari
walitumia busara na kuepuka kumtoa mgombea huyo wa CUF jukwaani, kwa
kuwa mazingira hayakuruhusu kumkamata.
Bundi NCCR
Wakati hali ikiwa hivyo majimboni na katika kata, migogoro katika
safu za uongozi za vyama hivyo vinavyounda Ukawa, baada ya kutoka
Chadema na CUF, sasa imehamia NCCR-Mageuzi.
Tayari aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa,
ameshaachana na chama hicho katika migogoro hiyo, huku aliyekuwa
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, akijiuzulu nafasi
zote ndani ya chama chake na kubakia mwanachama wa kawaida.
Lakini juzi, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Leticia Mossore akiwa
na Katibu Mkuu wa NCCR, Mosena Nyambabe na wajumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa na Kamati Kuu, walimua kupingana na Mwenyekiti wao wa Taifa,
Mbatia, mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano wao na waandishi wa habari, Mossore alilalamika kuwa
Ukawa imekuwa ikimshirikisha Mbatia peke yake kutoka NCCR-Mageuzi na
kuacha wengine, huku wanachama waliohama CCM, wakipewa umuhimu mkubwa
kuliko walioasisi umoja huo.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema kinachoonekana ni CUF kuwa
Ukawa-Zanzibar, kwa kuwa haijali yanayoendelea Tanzania Bara na Chadema
imekuwa ndiyo Ukawa-Tanzania Bara, kwa kuwa haijali yanayoendelea
Tanzania Bara, huku NCCR-Mageuzi ikijikuta haipo popote, badala yake
ikidhoofika siku hadi siku.
Mossore alifafanua katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, jinsi Ukawa ilivyoshindwa kupata muafaka wa kuachiana majimbo.
“Kwa mfano, NCCR-Mageuzi tuliachiwa majimbo 12 tu ya Kasulu Vijijini,
Kigoma Kusini, Muhambwe, Kasulu Mjini, Vunjo, Ileje, Mbinga Mjini,
Manyovu, Buyungu, Ngara, Nkenge na Korogwe Mjini. Ikumbukwe kwamba mwaka
2010, NCCR-Mageuzi ilisimamisha wagombea katika majimbo 67. Kwa maana
hiyo UKAWA umeturudisha nyuma katika kupata wabunge na kuimarisha chama
zaidi ya miaka 20 baada ya kuundwa kwake,” ilifafanua taarifa yake hiyo
kwa waandishi, aliyoitoa pamoja na Nyambabe.
Taarifa ilisema, “Licha ya kukubaliana kwamba NCCR-Mageuzi iachiwe
majimbo 12, wenzetu wa vyama vingine katika UKAWA wamesimamisha wagombea
katika majimbo 6 kati ya hayo. Wametuvunja moyo na kutuonesha kwamba
hawatujali. Tuna mifano mingi ya kuonesha jinsi wagombea wetu
wanavyofanyiwa vurugu. Pia tumeshindwa kupata muafaka wa namna ya
kuachiana wagombea udiwani katika kata nyingi”.
Mossore na Nyambabe walimshauri mwenyekiti wao, Mbatia, aitishe vikao
vya kikatiba ili waweze kujadiliana kuhusu hatima ya NCCR. Pia,
walimshauri Mbatia asiwe msemaji wa Chadema wakati anakiacha chama chake
cha NCCR kinadhoofika.
“Kwa mfano, Dk Slaa alipoishambulia Chadema hakuna kiongozi wa
Chadema aliyemjibu, isipokuwa Mbatia ndiye aliyeamua kujiingiza kwenye
ugomvi ndani ya Chadema.” Ilisema taarifa hiyo. Taarifa ilisema,
“Tutachangishana ili tusafiri kwenye majimbo na kata za wagombea wetu na
kuwasaidia kwenye kampeni ili wasibaki wapweke kama yatima”.
Taarifa hiyo ya NCCR ilisema, “Tunasisitiza kwamba upinzani wa kweli
nchini hauwezi kujengwa kwa njia za hila, kwa kukiuka taratibu za
kidemokrasia tulizojiwekea wenyewe, kwa kukiuka misingi muhimu kama
uadilifu, kwa kuweka mbele tamaa na maslahi binafsi kuliko taifa, kwa
kutegemea propaganda”.
Imeandikwa na John Nditi, Morogoro na Arnold Swai, Vunjo in Gazeti la Habari Leo
Sunday, 20 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment