*Yaiua Kagera, Kiiza akipiga ‘hat trick’, waionyeshea Yanga alama ya saa
*Azam, Mtibwa Sugar nazo zaendeleza dozi, Coastal Union mambo magumu
NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM
TIMU ya Simba imeonekana kuwa moto wa kuotea mbali kwenye Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL), baada ya kupata ushindi wa tatu mfululizo
kwa kuichapa Kagera Sugar mabao 3-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Simba kabla ya kuingia kwenye mchezo huo iliweza kuzichapa ugenini
timu za Tanga, African Sports bao 1-0 na Mgambo JKT 2-0 mechi zote
zikifanyika Uwanja wa Mkwakwani.
Wakati Simba ikifanya hayo, matajiri Azam FC na Mtibwa Sugar nazo
ziliendeleza ushindi wao kwa asilimia 100, Azam ikiichapa Mwadui bao 1-0
ugenini kwenye Uwanja wa Mwadui na Mtibwa Sugar ikiichabanga Ndanda 2-1
ndani ya Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Shujaa wa Simba kwenye mchezo wa jana alikuwa ni mshambuliaji wake
mpya kutoka Uganda, Hamis Kiiza ‘Diego’, aliyefunga mabao hayo yote na
kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Ligi Kuu msimu huu kufunga hat
trick.
Simba ilianza kwa kasi mchezo huo, mshambuliaji wake, Ibrahim Ajibu,
alikosa bao akiwa kwenye nafasi nzuri akizidiwa ujanja na mkongwe wa
Kagera Sugar, George Kavila aliyeokoa vizuri.
Kiiza alisawazisha makosa kwa kuipa uongozi Simba dakika ya 30 baada
ya kufunga bao la kwanza kwa kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na
kiungo Awadh Juma, hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Simba ilienda
ikiwa mbele kwa bao hilo.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Simba, ambapo alikuwa ni Kiiza
tena aliyetikisa nyavu za Kagera Sugar kwa mara ya pili kwa kichwa
dakika ya 46 akiunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na beki,
Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, faulo hiyo ilitokana na kiungo wake, Peter
Mwalyanzi, kufanyiwa madhambi na mabeki wa Kagera.
Kagera Sugar ilicharuka dakika ya 50 baada ya kuandika bao pekee
walilopata kwenye mchezo huo lililofungwa na Mbaraka Yussuf, aliyetumia
vema uzembe wa beki wa Simba, Hassan Isihaka aliyeshindwa kumkaba vema
na kupiga shuti lililopita katikati ya miguu ya kipa wa Simba, Manyika
Peter na kutinga wavuni.
Kiiza aliihakikishia ushindi Simba kwa kufunga bao la tatu dakika ya
90 kwa shuti zuri nje ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa Kagera Sugar,
Agatony Anthony na mpira kuisha kwa matokeo hayo.
Kituko kilichotokea kwenye mchezo huo ni wachezaji wa Simba pamoja na
Mkuu wa Idara ya Habari ya Mawasiliano ya timu hiyo, Haji Manara,
kuonyesha ishara ya saa kwa kidole kugusishwa kwenye sehemu inapovaliwa
saa mkononi tukio ambalo lilidaiwa kuwa wanawaonyeshea mahasimu zao
Yanga ambao wanacheza nao Jumamosi hii.
Kwenye Uwanja wa Mwadui, bao pekee la Azam lilifungwa na nahodha
wake, John Bocco kwa shuti akiwa ndani ya eneo la 18 na kumwacha kipa wa
Mwadui, Shaban Kado akiuangalia mpira ukitinga wavuni bila kufanya
lolote.
Lakini Azam ilicheza pungufu kwa takribani dakika 37 baada ya kupata
pigo dakika ya 53 kufuatia beki wake, Aggrey Morris, kuonyeshwa kadi
nyekundu na mwamuzi kwa kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Mwadui, Paul
Nonga, ndani ya eneo la hatari na kuwa penalti.
Hata hivyo, Mwadui ilishindwa kutumia vema penalti hiyo kusawazisha
bao hilo baada ya mshambuliaji, Rashid Mandawa kuikosa kufuatia kipa wa
Azam, Aishi Manula kuicheza vema kwa kuipangua.
Mwadui iliyoonekana kucheza vizuri baada ya Azam kupata kadi hiyo
ilikosa mabao mengi ya wazi kupitia washambuliaji wake Mandawa na Nonga.
Mtibwa Sugar iliyoibuka na ushindi wa mabao 2-1, yenyewe ilijipatia
mabao yake kupitia kwa beki Salim Mbonde na Said Bahanuzi huku la Ndanda
likifungwa na Kigi Makasi.
Mechi nyingine iliyofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, wenyeji
Coastal Union waliendeleza mwenendo mbaya kwenye ligi kwa kulazimishwa
suluhu na Toto Africans ya Mwanza.
Coastal Union mpaka sasa haijaonja ladha ya ushindi ikifungwa mabao
2-0 na Yanga, ikafungwa tena na Ndanda bao 1-0 kabla ya jana kuambulia
suluhu hiyo.
Baada ya matokeo hayo, Yanga imeendelea kukaa kileleni ikiwa na
pointi tisa sawa na Simba iliyo nafasi ya pili, Azam inafuatia nafasi ya
tatu na Mtibwa nafasi ya nne.
Mkiani zipo JKT Ruvu na African Sports ambazo hazijaambulia pointi yoyote mpaka sasa.
Created by Gazeti la Mtanzania
Monday, 21 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment