NA FESTO POLEA
TAMASHA la 34 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo
lililoanzishwa mwaka 1981 na Chuo cha Sanaa Bagamoyo (kwa sasa Taasisi
ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo), linatarajiwa kufanyika kwa siku sita
katika viwanja vya chuo hicho bila ya kuwa na ushiriki wa wasanii wa
Bongo Fleva.
Mwenyekiti wa Tamasha hilo, John Mponda, alilieleza MTANZANIA
kwamba hakuna msanii wa Bongo Fleva yeyote aliyejitokeza kuomba
kushiriki katika tamasha hilo, jambo ambalo linaonyesha kutokuwa na
wasanii hao katika tamasha hilo.
“Tamasha hilo litaanza Septemba 21 hadi 27, likiwa na kauli
mbiu kwamba ‘Sanaa na Utamaduni katika Uchaguzi huru na wa Amani’ na pia
tunawakaribisha wasanii wa bongo fleva wajitokeze kwa kuwa muda bado
upo,’’ alieleza Mponda.
Mwenyekiti huyo alisema licha ya wasanii hao kutojitokeza,
lakini idadi kubwa ya vikundi vya ngoma za asili, maigizo, sarakasi,
mazingaombwe, muziki wa kisasa na asili, sanaa za ufundi na bidhaa
mbalimbali vitatoa burudani kupitia kazi zao.
Aliongeza kwamba vikundi 48 vimethibitisha kushiriki, ambapo
ni vikundi 43 vya Tanzania na vikundi vitano kutoka nchi ya Kenya,
Namibia, Afrika Kusini, Korea na Congo.
Licha ya tamasha hilo kuwa la burudani, pia kutakuwa na mada
ndogondogo zitakazotolewa kupitia kongamano na warsha zitakazohusu haki
za binadamu, rushwa na kupinga mauaji ya albino.
Tamasha hilo lilianzishwa ili kuwapa nafasi wanafunzi wa chuo
hicho kuonyesha kwa vitendo waliyojifunza kwa mwaka mzima kwa
kushirikisha wakazi wa maeneo hayo, lakini baadaye likabadilishwa na
kuwa tamasha la kila mwaka.
Created by Gazeti la Mtanzania
Friday, 18 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment