MGOMBEA wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Edward Lowassa amesema atalitafutia soko zao la korosho na kuimarisha
mfumo wa stakabadhi ghalani kama atachaguliwa kuwa Rais.
Aliyasema hayo juzi wakati anahutubia wananchi wa wilaya ya Masasi
waliojitokeza kumsikiliza kwenye viwanja vya Boma mjini humo. Alisema
atahakikisha zao la korosho linalotegemewa na wananchi wa mikoa ya
Kusini ya Lindi na Mtwara linatafutiwa soko la ndani na ikibidi atatoa
ruhusa kwa wakulima hao kuuza zao hilo nje ya nchi.
Pamoja na ahadi hiyo mgombea huyo alisema kipaumbele chake kikubwa ni
elimu huku akiendelea kukumbusha ahadi yake kuwa akiingia madarakani
serikali yake itatoa elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Alisema serikali yake itapitia upya mikataba ya madini ili Watanzania
wanufaike na rasilimali zao.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani Lowassa alisema
akipewa ridhaa na Watanzania na kufanikiwa kuingia Ikulu wiki moja ya
mwanzo ya urais wake atarekebisha mfumo huo ili uwe mzuri zaidi kuliko
ulivyo sasa huku akijinasibu kuwa ataondoa kodi zote zinazombana
mkulima.
Katika hatua nyingine mkutano huo wa kampeni wa Lowassa uliingia
dosari baada ya meneja kampeni wa Lowassa John Mrema kumuomba mwenyekiti
mwenza wa Ukawa na ambaye anagombea nafasi ya ubunge jimbo la Masasi,
Emanuel Makaidi kusalimia wananchi wa mji wa Masasi na uwanja mzima
kulipuka kwamba hawamtaki Makaidi.
Created by Gazeti la Habari Leo
Thursday, 24 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment