Na Waandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimezindua kampeni za Urais Zanzibar kwa
kishindo huku mgombea wake, Maalimu Seif Sharif Hamad, akiahidi ajira
kwa Wanzibari wote ndani ya miaka mitano na kubadilisha uchumi wa nchi
hiyo kuwa imara kama ule wa Singapore.
Akizungumza na maelfu ya wananchi wa visiwa hivyo waliojitokeza jana
kwenye uwanja wa Kibanda Maiti Unguja, Maalim Seif alisema endapo
atapatiwa ridhaa ya kuongeza nchi, atapigania pia mamlaka kamili ya
Zanzibar ikiwa ni pamoja na kupata katiba inayotambua Muungano wenye
usawa.
Ndoto yangu ya kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki
ipo palepale, nitahakikisha tunakuwa na uchumi imara ambao utakuwa
unakua kwa haraka,”alisema Maalim Seif.
Alisema katika uongozi wake atahakikisha nchi hiyo inajenga
bandari ya kisasa kwa vitendo na si maneno kama wanavyofanya wengine.
Alisema pia kuwa serikali inayomaliza muda wake ilikuwa na mipango ya
kujenga Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na kuahidi kuuzindua Oktoba mwaka
huu lakini dalili zinaonyesha suala hilo halitawezekana.
“Airport (uwanja wa ndege) ilisemwa itazinduliwa Oktoba lakini juzi
nilitembelea ujenzi wa uwanja huo inaonekana haiwezekani,”alisema Maalim
Seif.
Alisema uboreshaji wa miundombinu ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na
bandari, kutafanya watu wawe wanafika visiwani hivyo kununua bidhaa kama
ambavyo sasa wanapoenda Dubai.
Alisema serikali yake pia itafungua Benki ya Uwekezaji ya
Zanzibar(ZIB) ambayo itakuwa inatoa mikopo kwa watu mbalimbali wakiwamo
vijana lengo likiwa ni kuwapa mitaji watu wote.
“Benki itakuwa inatoa mikopo ya masharti nafuu, lengo ni kuwasaidia
vijana wasiokuwa na mitaji kujiendesha katika maisha,”alisema Maalim
Seif na kuongeza:
“Hakuna jambo linaloniuma kama kuona vijana wakiwa wanarandaranda
(kutembea)barabarani, matumaini yangu nikimaliza miaka mitano kutakuwa
hakuna mtu asiyekuwa na ajira,”alisema Maalim Seif.
Akizungumzia mafuta na gesi, alisema ataanzisha wizara maalumu ya
kushughulika na nishati hiyo na kwamba ndani ya siku 100 atakuwa
ametengeza sheria na sera yake wananchi waweze kuonja matunda yake.
Muungano
kuhusu muungano alisema ahatakikisha visiwa hivyo vinapata mamlaka kamili viweze kufanya uamuzi kwa masuala yanayowahusu.
“Wazanzibari wanataka kuona nchi yao imepata mamlaka kamili, walio
madarakani hivi sasa wameshindwa, zimefanyika juhudi za kuleta Tume ya
Jaji Joseph Warioba kwa kukusanya maoni.
“Mlio wengi mlitaka muungano wa mkataba lakini tume wakasema tupate
serikali tatu kwa bahati mbaya CCM waliikataa na kuweka vitu vyao.
“Hata waliokuwa mbele katika mambo hayo walishindwa kuitetea Zanzibar
na badala yake walipofika huko waliufyata wakaandaa rasimu yao
wakakubali Zanzibar iendelee kudhalilishwa”.
Alisema endapo atachaguliwa yeye pamoja na mgombea urais wa Muungano,
Edward Lowassa, watashirikiana na kuhakikisha wanaitisha upya bunge la
katiba na kurudisha maoni ya wananchi ambayo yataelekeza kuwapo
serikali tatu ambazo zina mamlaka.
Misingi ya utawala bora
Maalim Seif alisema atahakikisha anaimarisha misingi ya utawala
bora ambayo itazuia Wazanzibari kunyanyaswa na kuteswa ndani ya nchi
yao.
“Mambo ya watu kuvaa soksi usoni wanapiga watu mwisho Oktoba 25,
siwezi kukubali Wazanzibari wanadhalilishwa ndani ya nchi yao,”alisema
Maalim Seif.
Alisema pia hataruhusu Mzanzibari aliyefanya kosa visiwani humo kwenda kusomewa mashtaka Tanzania Bara.
“Mahakama ya Dar es Salaam na Zanzibar ni sawa ila leo wameamua
kuwatoa watu huku kuwapeleka huko, nasema watarudi kama wana makosa
watahukumiwa huku kwa mahakama ya Zanzibar,”alisema Maalim Seif.
Lowassa alaani uchanaji mabango yake
Naye Mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema)
anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa,
amekemea vikali tabia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuchana
mabango yake akisema ni kinyume na sheria.
Alisema katika kipindi hiki cha kampeni, mambo mengi yanaweza
kujitokeza hivyo wanachama hao wanapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu
kuepusha matatizo.
Alisisitiza kauli yake kuwa Ukawa wataendelea kufanya kampeni za
ustaarabu kuhakikisha wanapata ushindi kwa sababu uwezo huo wanao huku
akiwataka CCM kuacha tabia ya kufikiria kuiba kura.
“Siku hizi wameanza tabia ya kuchukua mabango yetu na kuyaangusha,
wakimaliza wanayatupa porini, nawaambia waache kabisa mchezo huo, sisi
tutandelea kufanya kampeni za ustaarabu kuhakikisha tunapata ushindi
kwa sababu uwezo tunao.
“Mtanipa kura…? Wangapi watamchagua Lowassa…wanyooshe mikono juu,
uwezo wa kushinda tunao, ninawaambia CCM waache kuiba kura,”alisema
Lowassa.
Lowassa pia alimzungumzia mgombea urais wa Zanzibar wa Chama cha
CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ni kiongozi aliyepigania ukombozi wa
taifa hilo hivyo anapaswa kuungwa mkono aweze kupata ushindi.
Naye Mwasisi wa CCM, Mzee Nassoro Moyo alisema Wazanzibari wanaopenda
amani na utulivu hawana budi kuwachagua wagombea wa CUF waweze kupata
ushindi na kuwaletea wananchi maendeleo.
“Kama kuna Mzanzibari anapenda amani na utulivu, anapaswa kuwapigia
kura ya ndiyo viongozi wa CUF waweze kuendeleza amani,”alisema Mzee
Moyo.
NCCR-MAGEUZI
Katibu Mkuu wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema CCM
kimekuwa kikikataa kutoa ushindi kwa CUF lakini mwaka huu kitautoa
kulingana na wanavyotaka wenyewe.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu aliwataka
Wazanzibari wasijisahau kwa madhira na kero zilizofanywa na CCM, hivyo
wafanye uamuzi mgumu kuhakikisha wanapata ushindi.
“Wazanzibari tusijisahau kwa matatizo yetu yaliyotukuta, tunapaswa
kuwa bega kwa bega kuhakikisha tunapata ushindi,”alisema Mwalimu.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu alisema leo ni
siku ya kumbukumbu kwa wananchi waliofariki dunia kwenye meli ya MV
Spice Islanders ambayo imetimiza miaka minne tangu ilipozama katika
Bahari ya Hindi.
Ilivyokuwa
VIWANJA vya Kibanda Maiti jana vilifurika umati wa watu waliokuja
kushuhudia uzinduzi wa kampeni za mgombea urais wa Chama cha Wananchi
(CUF) Zanzibar, Maalif Seif Sharif Hamad.
Mkutano huo uliopangwa kuanza saa 9:00 alasiri, lakini kuanzia saa
4:00 asabuhi tayari baadhi ya wanachama wa chama hicho walianza kuwasili
uwanjani hapo.
Ilipotimu saa 7 mchana uwanja huo ulikuwa umefurika umati wa watu huku wengine wakigombea mahali pa kukaa.
Makundi mbalimbali ya vijana walikusanyika uwanjani hapo huku
wakiimba nyimbo mbalimbali, huku baadhi yao walikuwa wakipeperusha
bendera za CUF na zile za chama cha zamani cha Afro Shirazi (ASP).
Hata hivyo vikundi mbalimbali vya ngoma navyo havikuwa nyuma, ambapo
wasanii walijipanga wakituimbuiza nyimbo mbalimbali za kuisifia CUF na
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Vikundi hivyo vya ngoma vilikuwa vikiimba “Mwaka huu tumeamua, CCM
hata wafanye nini sisi tumeamua kuwapa kura zetu Seif na Lowassa, tuna
imani mabadiliko yataletwa na ninyi, kura zetu tutawapa…CCM waone
kinguzungu.
Created by Gazeti la Mtanzania
Sunday, 13 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment