*Mkurugenzi Tehama aondolewa
* Maofisa watoa kauli tofauti
NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Sisti Cariah ameondolewa kwenye nafasi
hiyo, imefahamika.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya NEC ambazo MTANZANIA ilizipata
juzi na jana zimeeleza kuwa mkurugenzi huyo ambaye ni mtu muhimu katika
Tume ameondolewa katika siku za karibuni huku kukiwa hakuna taarifa ya
wapi alikohamishiwa serikalini.
Chanzo hicho cha ndani ya tume kimesema mkurugenzi huyo ameondolewa
siku tano zilizopita huku zikiwa zimesalia siku 25 tu kufikia Uchaguzi
Mkuu Oktoba 25 wakati idara hiyo ya Tehama ikiwa ndiyo ina orodha nzima
ya Watanzania wanaotarajiwa kupiga kura.
“Ni kweli mkurugenzi huyo wa Tehama ameondolewa na nafasi yake
imechukuliwa na aliyekuwa msaidizi wake (bila kumtaja) na nafasi
nyingine zinaendelea kusukwa upya.
Hadi jana tovuti ya Tume hiyo hadi ilikuwa ikionyesha kuwapo
mkurugenzi mmoja tu ambaye ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan
Kailima, huku ukiwapo unaosomeka kwamba kurugenzi nyingine zinaendelea
kusukwa upya.
Tume hiyo ina kurugenzi saba ambazo ni Elimu ya mpiga kura na habari, Uchaguzi, Ununuzi, Uhasibu, Ukaguzi, Utawala na Tehama.
MTANZANIA lilipomtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari wa NEC, Clarence Nanyaro kupata ufafanuzi wa suala hilo alisema:
“Ndugu yangu hakuna mkuu yeyote wa idara aliyehamishwa hadi sasa
lakini ngoja nifuatilie zaidi nitakupa jibu zuri kwa kutumia simu ya
mezani.”
Baada ya dakika chache alipiga simu lakini aliendelea kusisitiza kwamba anaamini idara hizo hazijafanyiwa marekebisho.
Hata hivyo alisema hazisimamiwi na wakurugenzi bali zinasimamiwa na wakuu wa idara.
“Watu wengi wamekuwa wakiwaita wakuu wa idara hizo kama wakurugenzi
jambo ambalo si sahihi na hata hivyo wote bado wapo,” alisema Nanyaro na
kuongeza:
“Sina taarifa za kuhamishwa Dk. Cariah kwa kuwa hadi jana (juzi) alikuwa kazini akiwajibika hadi saa nne usiku tulipoachana.
Alipoulizwa kuhusu tovuti ya NEC kuwa na ujumbe unaoonyesha
kufanyika marekebisho ya wakuu wa kurugenzi zote saba, alisema suala
hilo aulizwe Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima kwa kuwa ndiye
mwenye mamlaka ya kuzungumzia wafanyakazi wa Tume.
MTANZANIA lilipomtaka asaidie kupata jibu hilo kutoka kwa bosi wake
huyo alisema kwamba wakati huo mkurugenzi huo alikuwa kwenye mkutano
na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU). Aliahidi kutoa jibu baadaye kama
angeonana na Kailima na kukata simu.
Baadaye Nanyaro alipiga tena simu na kusema kwamba taarifa
zilizokuwa zikielezea mabadiliko ya viongozi wa kurugenzi za Tume
zilitokana na viongozi hao saba kutowasilisha picha zao kwa ajili ya
kuziingiza taarifa hizo kwenye tovuti.
“Napenda kusema wakurugenzi wote saba wapo kazini; katika Idara ya
elimu ya mpiga kura na habari, Uchaguzi, Ununuzi, Uhasibu, Ukaguzi na
Utawala akiwamo Dk. Cariah wa Tehama ambaye alikuwa kazini hadi juzi na
alitoka muda wa saa nne usiku,” alisema Nanyaro.
Kauli ya Jaji Lubuva
Wakati Nanyaro akisema hivyo, juzi Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu
Damian Lubuva, alipoulizwa na Mtanzania alikiri kuwa Mkurugenzi huyo wa
Tehama, Dk. Cariah, amehamishwa.
Hata hivyo dakika chache baadaye Jaji Lubuva alipiga simu kwa
mhariri wa gazeti hili akikanusha taarifa yake hiyo ya awali akisema
hakuna mkurugenzi yeyote aliyehamishwa katika Tume yake tofauti na
mabadiliko yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika nafasi ya
mkurugenzi wa uchaguzi iliyokuwa inashikiliwa na Julius Malaba ambaye
aliteuliwa kuwa jaji hivi karibuni.
“Nakwambia ndugu yangu, Mbowe na Chadema waache kutapatapa,
wanaingilia utendaji wa Tume na serikali nawaomba wasiendelee kupotosha
umma, ” alisema Jaji Lubuva.
Alichosema Mbowe
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Himo
Polisi mkoani Kilimanjaro juzi, Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe aliituhumu Serikali kwa kile alichokiita
uchakachuaji wa NEC kwa kubadilisha wakurugenzi wote na kuweka wapya
kutoka idara nyeti za usalama.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) alidai viongozi hao wa Tume wameondolewa na serikali lengo
likiwa ni kuiba kura.
“Mtu mwenye wajibu wa sheria wa kusimamia uchaguzi ni Tume ya Taifa
ya Uchaguzi, baada ya CCM kuona Lowassa (Mgombea Urais wa Chadema,
Edward Lowassa), anashinda wameamua kuandaa mazingira ya kuchakachua
Tume yenyewe.
“Walianza kumuondoa Mkurugenzi wa Tume Malaba (Julius) mwezi mmoja
uliopita katika mazingira ya kutatanisha wakaleta mwingine, wiki mbili
zilizopita…. wakurugenzi wote wamewang’oa na kuwaingiza wengine.
“Tume kwa sasa siyo huru huku Serikali ya CCM pia ikiingiza wanajeshi
kwenye tume hiyo. Namuuliza Mkuu wa Majeshi atueleze hao wanajeshi
huko wameenda kufanya nini?” aliuliza Mbowe
Mbowe alisema pia kuwa CCM imeanza mkakati mwingine wa kutengeneza
kura bandia na tayari zimepelekwa mkoani Kilimanjaro, Mamlaka ya
Barabara (Tanroads) ambayo iko chini ya Magufuli ndiyo inasambaza kura
hizo,” alidai Mbowe.
Mwenyekiti mwenza huyo wa Ukawa alisema hakuna mkakati wowote ovu
utakaopangwa na CCM bila Umoja huo kuujua kwa sababu kila inachokipanga
asubuhi wao wanakipata mchana.
“Mnaopanga nao mchana, usiku tunakuwa nao. Kikwete wewe ni rais wa
nchi usifikiri una usalama sana kama utaharibu uchaguzi wa nchi hii.
Watanzania ndiyo wataamua, Kikwete na familia yako hamtatuchagulia mtu,
tumia majeshi, tumia vyote unavyotaka, tutapiga kura na kuzilinda kwa
gharama yoyote… nimesema haya nitoe onyo kwa CCM,” alisema Mbowe.
Akiwa kwenye mkutano wa kampeni katika Kata ya Kahe kwenye Viwanja
vya Shule ya Oria, Mbowe alisema kila mtu atakayejaribu kuzuia
mabadiliko na kuwa wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ya
masilahi binafsi, mafuriko yatamkumba.
“Mabadiliko tunayozungumzia hapa yako kwa vyama vyote, mtu yeyote
atakayekuwa wakala wa kuitetea CCM kwa sababu ya ubinafsi mafuriko
lazima yamkumbe, tuna kila sababu ya kupigania mabadiliko,” alisema
Mbowe.
Alisema mabadiliko ambayo Ukawa unayapigania yanamgusa kila
Mtanzania bila kujali dini yake wala kabila lake hivyo ni vigumu mtu
kuyahujumu.
Created by Gazeti la Mwananchi.
Tuesday, 29 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment