Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli.
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli
ameendelea kueleza msimamo wake wa kutaka Tanzania yenye viwanda kwa
kusisitiza kuwa hatakubali kuwepo kwa urasimu kwa watu wanaotaka
kuwekeza nchini.
Amekemea pia utaratibu wa baadhi ya watumishi serikalini kuwazungusha
watu wanaotaka kuwekeza kwa kauli za ‘njoo kesho’ akisema, katika
uongozi wake, hataruhusu vitendo hivyo.
Akihutubia umati wa wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika
katika uwanja wa Samora, mjini Iringa, Magufuli alisema atakapoingia
madarakani, atataka kuona kiwanda cha usagishaji cha NMC cha mjini
Iringa kinafanya kazi mara moja.
“Nataka serikali ya wachapakazi,” alisema na kumuita mwekezaji
mzalendo wa kiwanda cha ASAS, Salim Abri, huku akisisitiza kwamba, nchi
inahitaji wawekezaji wanaotengeneza ajira kama huyo.
Akizungumzia mafanikio ya serikali yake, Magufuli alimsuta Mchungaji
Peter Msigwa (Mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema aliyemaliza muda
wake) kutokubali kusema ukweli juu ya mafanikio yaliyopo Iringa.
“Lakini leo mchungaji, tena mchungaji wa bwana, mchungaji wa kondoo
anasema hakuna chochote,” alisema Magufuli na kutaja maeneo kadhaa
yanayodhihirisha maendeleo ya nchi ikiwamo, huduma za mawasiliano,
barabara na ujenzi wa nyumba bora.
Alihoji wanaodai hakuna chochote kilichofanyika, wanashindwa kuona
hata suala la amani kuwa pia ni sehemu mafanikio? “Shukurani ya punda ni
mateke,” alisema. Magufuli aliendelea kusisitiza msimamo wake juu ya
uwajibikaji na kusema, kwenye kazi hatokuwa na blabla.
Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi, mgombea huyo wa urais alisema,
lengo ni kuhakikisha kila anayefanya kazi vizuri, anafaidi badala ya
kuwapo tofauti kubwa ya mishahara. Alisema ndiyo maana imeundwa tume ya
kupitia mishahara ili wafanyakazi wanaofanya vizuri wanufaike na siyo
kuhangaika na mwisho wa siku, kuichukia serikali yao.
Alisema utaratibu wa watu wachache wanaopata fedha za rushwa na
kudhulumu watu wa chini, kuharibu eneo moja na kuhamishiwa lingine,
hataukubali katika serikali yake kama ataingia madarakani.
Mgombea urais huyo alisisitiza kwamba anataka kuleta mabadiliko ikiwa
ni pamoja na kutekeleza ilani ya chama inayotaka zitengenezwe ajira
asilimia 40. Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye, akihutubia mkutano huo, alisema Watanzania hawataki Rais wa
majaribio Nape ambaye alisema CCM siyo chama kinachoongozwa na malaika,
alikiri kuwa kina upungufu wake lakini pia kina mambo mengi mazuri
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 29 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment