JOSEPH HIZA NA MITANDAO
JUMANNE wiki hii Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, alitangaza
mageuzi makubwa juu ya namna kanisa hilo linavyoweza kushughulikia
ubatilishaji wa ndoa.
Vifuatavyo ni baadhi ya vitu unavyotakiwa kuvifahamu.
Kwanza tuangalie; Ndoa batili ni nini? Je ni sawa na talaka? Ndoa batili ni uamuzi wa kutangaza kuwa muungano
huo wa watu wawili baina ya mwanamume na mwanamke haukutimiza vigezo vinavyoweza kuihalalisha ndoa tangu mwanzo.
Kwamba kuna kitu hakikuwa sawa wakati wa ufungaji ndoa hiyo na
hivyo kumeizuia kuwa halali tangu kufungwa kwake. Sababu zinaweza kuwa
nyingi ikiwa ni pamoja na kutokuwa muwazi kuhusu kuwa na watoto au ndoa
ilifungwa kwa msingi wa kilaghai.
Michakato ya awali ya kubatilisha ndoa ilitawaliwa na urasimu, ikichukua hata miaka mingi, wakati mabadiliko ya
sasa yanapunguza muda wa kubatilisha ndoa na kuondoa sehemu kubwa ya ada na inampa mamlaka askofu wa
dayosisi.
Kwa sababu hiyo ubatili ni tofauti na talaka, ambayo inahusu uvunjaji
wa ndoa iliyokuwa halali na hivyo haikuhusishwa katika mageuzi ya Papa
kama wengi wanavyoweza kufikiri, isipokuwa kuruhusu kubakia kama waumini
wa kanisa. Kwanini ubatili ni suala muhimu kwa Kanisa la Katoliki?
Yesu Kristo anafundisha kuwa iwapo watu wanatalikiana na kuoa tena,
wanafanya dhambi kubwa ya uzinifu. Pamoja na mambo mengine alifundisha;
“Akawaambia, kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu
yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini. (Mark
10:11-12).
Kwa sababu ya fundisho hilo, kanisa haliwezi kutoa kiholela ruhusa kwa
watu kuoa. Kwa kufanya hivyo litakuwa linaruhusu utendaji wa dhambi ya
uzinifu.
Kwa sababu hiyo, iwapo mtu aliyetaliki au kutalikiwa anataka kuoa, Kanisa linahitaji kufanya tathmini ya ndoa ya
kwanza kuangalia iwapo ni halali au laa.
Iwapo linaona ni halali bado kwa msingi wa mafundisho ya Biblia, mtu
huyo bado anapaswa kueendelea na mwenzi wake wa awali na hawezi kuoa
mtu mwingine.
Lakini iwapo haikuwa halali, waliokuwa wenzi wa ndoa ya kwanza
walikuwa hawajashikamana na hivyo, isipokuwa tu kama kutakuwa na
kipingamizi kingine, watakuwa huru kuoa wengine. Namna mchakato
wa ubatilishaji ndoa unavyofanya kazi Hili ni suala tata, lakini mfano
unaweza kuchukuliwa kupitia nyaraka mbili: Kanuni za Sheria za Kanisa,
ambazo zinaendesha Kanisa la Katoliki la Magharibi na zile za makanisa
ya Mashariki.
Wakati mwanamume na mwanamke wanapotalikiana, wanaelekea kwenye
dayosisi husika kuwasilisha suala lao ili kuanza mchakato wa uchunguzi
kuangalia iwapo ndoa ilikuwa halali.
Mchakato huu, unaweza kuwa rahisi au mrefu, kwa kutegemea mazingira ya suala lenyewe na aina ya ushahidi
unaopatikana.
Iwapo ndoa yao haikuwa halali, watapewa amri ya kuivunja au kuibatilisha. Papa Francis alichukua hatua gani?
Ametoa nyaraka mbili, ambayo kila moja inajulikana kwa kilatini kama ‘motu proprio’.
Motu proprio ni waraka unaotolewa kutokana na mpango wa Papa mwenyewe.
Mara nyingi hutumika kuanzisha au kuhalalisha masuala yakisheria,
yasiyohusiana na mafundisho ya kanisa, ambayo hushughulikiwa na
nyaraka nyingine kama vile encyclicals. Nyaraka hizo mbili zilizotolewa
na Papa Francis
ni: Mitis Iudex Dominus Iesus, yaani Bwana Yesu Jaji Mwema, ambayo
inaleta mageuzi ya mchakato wa ubatilishaji ndoa katika kanisa la
kimagharibi na; Mitis et Misericors Iesus, yaani Yesu Mwema na Mwenye
huruma, ambayo ni mageuzi ya mchakato wa ubatilishaji wa makanisa
ya mashariki.
Hadi sasa nyaraka hizo zinapatikana kwa kilatini na Kiitaliano, ambapo toleo la Kiingereza bado kupatikana.
Nyaraka hizo ziliandaliwa na maagizo ya Papa Francis, baada ya kuwapa
kazi hiyo wataalamu wa sheria wa Vatican, kupitia jopo aliloliteua na
kulikabidhi kazi hiyo ya kurekebisha na kuboresha sheria Oktoba 2014.
Nyaraka zote hizo mbili zina usuli unaoeleza sababu za maamuzi ya
papa, zikifuatiwa na sheria ambazo zinachukua nafasi ya vipengele vya
ubatilishaji ndoa katika Kanuni za Sheria za Kanisa na Kanuni za Sheria
za Makanisa ya Mashariki.
Kila waraka una mchakato wa kisheria ukieelekeza maaskofu na wengine namna michakato mipya inavyofanya
kazi.
Kwanini Papa Francis amechukua hatua hizo? Alisema anachukua
hatua hiyo si kuchochea ubatilishaji ndoa bali kurahisisha mchakato,
uliokuwa mrefu na mzigo mkubwa kwa wengi waliotumia hadi mamia
kwa maelfu ya dola.
Hatua yake hiyo ni ishara ya nyingine ya dhamira yake ya kulifanya
kanisa liwe rafiki zaidi na kuendana na walio wengi, ambao
baadhi wamekuwa wakilikimbia kutokana na sababu kama hizo za misimamo
mikali.
Ikumbukwe ni msimamo wa Papa kumgomea Mfalme Henry the VIII wa Uingereza kumtaliki mkewe Catherine
wa Aragon katika karne ya 16, uliosababisha England ijitenge na Rome na kushuhudia kuundwa kwa Kanisa la
England huku mfalme akiwa mlinzi wa Imani wa kanisa hilo.
Katika sehemu nyingi za dunia mchakato umekuwa wa taratibu mno na
mgumu. Katika baadhi ya nchi, inaweza isiwezekana kufikisha kesi
kanisani na hata kusikiliza kesi ya fulani na iwapo hilo litafanyika,
inaweza kuchukua miaka mingi kabla ya uamuzi wa kutolewa.
Hivyo, Papa Francis aliitikia ombi la Sinodi ya Maaskofu mwaka 2014 iliyoomba mabadiliko ya mchakato wa kubatilisha ndoa.
Mabadiliko gani Papa Francis aliyafanya katika mchakato? Mabadiliko makuu matatu aliyotangaza Papa ni kuondoa
mchakato wa mapitio ya mara ya pili wa uamuzi kutoa talaka kupitia mahakama ya kanisa kabla ya ndoa kubatilishwa;
Kuwapatia maaskofu uwezo wa kuharakisha na kubatilisha ndoa pale
wenzi wanapoamua wenyewe katika mazingira fulani kama vile ukatili
katika ndoa au uasherati na;
Mchakato kuwa bure, isipokuwa kwa ulipaji wa ada ndogo kwa ajili ya gharama za kiutawala.Kabla ya sheria
hiyo Wakatoliki waliotaka talaka walihitaji kibali kutoka kwa mahakama mbili za kanisa, wakati sheria mpya
inabakiza moja, ijapokuwa rufaa bado zinaruhusiwa.
Aidha kabla ya sheria hiyo wanandoa wa kikatoliki wanaotalikiana bila idhini ya kanisa na kuolewa upya
walihesabiwa kama wazinifu na hawakuruhusiwa kupokea komunio.
Lakini chini ya utaratibu mpya wanaotalikiana, wakioa au kuolewa tena watabakia kuwa wafuasi wa kanisa hilo.
Zitakuwa rasmi kama sehemu ya sheria za kanisa (canon law) ifikapo
Desemba 8 mwaka huu, wakati Papa atakapoanza kutangaza Mwaka wa Jubilee,
ambao kwa kawaida huhusishwa na msamaha.
Created by Gazeti la Mwananchi
Sunday, 13 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment