MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John
Magufuli, ameahidi serikali yake itaimarisha uhusiano na nchi jirani,
lakini kwa kuonya wageni wanaoingia nchini kufanya uhalifu kwa
kushirikiana na Watanzania, akisema wajirekebishe mara moja.
Aidha, ameahidi atakapochaguliwa kuwa rais, serikali yake itapanga
namna ya kuboresha biashara za mpakani kwa kuhakikisha kunakuwa na uhuru
miongoni mwa wananchi.
Dk Magufuli ambaye amesisitiza dhamira yake ya kutaka Tanzania
iendelee kuwa kimbilio la wageni kutokana na amani, alitoa ahadi hizo
jana katika mikutano mbalimbali aliyoifanya kwenye maeneo tofauti katika
wilaya za Buhigwe na Kasulu, mkoani Kigoma.
Kiama kwa wahalifu
Akizungumza katika kijiji cha Mnanila Jimbo la Manyovu, Dk Magufuli
alisema atahakikisha Tanzania inaendelea kuwa kimbilio la watu wote kwa
amani na usalama.
“Tutaendelea kuimarisha uhusiano na nchi jirani, na wananchi
watapangiwa namna ya kuboresha biashara za mipakani, kuwe na uhuru…dunia
hii ni moja,” alisema.
Hata hivyo, alisema wapo watu wachache kutoka nchi jirani, wenye nia
mbaya ambao wamekuwa wakishirikiana na Watanzania kufanya uhalifu
hususani katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Katavi.
“Niombe hao wachache wanaokimbia kutoka Rwanda, Burundi , DRC Congo,
wanaotoka na mabomu, wengine na bunduki wengine wanakimbia kwa nia
mbaya; ambao wanashirikiana na watu wa huku wenye nia mbaya, wanateka
mabasi, wanaua watu, waache,” alisema.
Alisisitiza, “Kwa sababu tukiichafua amani ya Tanzania watakimbilia wapi? Kuwa mkimbizi ni kitu kibaya,”
Aliahidi kuwa wakimbizi kutoka Burundi wenye nia njema, watapewa uraia.
Akitoa mwito kwa watu hao kuacha mara moja, Magufuli alisema ilani ya
CCM inasisitiza kulinda amani jambo atahakikisha analisimamia.
“Nataka haya yaishe… wale wenye nia mbaya wajirekebishe,”alisema na
kuhimiza wananchi kutoa taarifa kwa vyombo na mamlaka zinazohusika na
usalama wakiona watu wanaowashuku kufanya uhalifu.
Alisema imekuwa ni kawaida kwa mikoa ya Kagera, Kigoma, Katavi,
mabasi kusindikizwa na polisi kwa hofu ya usalama. Alisema anataka chini
ya serikali yake, utaratibu huo wa kusindikiza magari uishe.
“Kazi ya polisi si kusindikiza mabasi. Kazi ya polisi ni kulinda
amani…wamo polisi ambao wamepoteza maisha yao kwa kupigwa na majambazi.
Lakini wahalifu hawa wengine tunawakaribisha sisi wenyewe (wananchi),
wengine tunawajua…ukimpata mtu ambaye unafikiri anatishia amani kwenye
eneo lako, ripoti kwa vyombo vya dola,” alisema.
Akihutubia maelfu ya watu mjini Kasulu, alihimiza wananchi kuogopa
wanasiasa wanaohubiri uvunjifu wa amani. Magufuli alisema, “watu
wanaotaka kuchezea amani ya Tanzania, nitalala nao mbele.” Kukomesha
matabaka Magufuli alisisitiza kwamba hataki serikali ya Watanzania wenye
madaraja.
Alisema lengo lake ni kuhakikisha watu wa maisha ya chini, kati na juu wanakuwa sawa.
“Sitaki serikali ya Watanzania wenye madaraja. Kwangu madaraja yote
ni sawa, watu wote wameumbwa na Mungu,” alisema na kusisitiza nia yake
ya kutaka uchumi na maendeleo yapae.
Bima ya afya Aliahidi pia kuhamasisha bima ya afya kwa Watanzania wote.
Aidha katika mikutano kwenye maeneo mbalimbali, aliahidi serikali
yake kuendelea kuwajengea barabara, kutatua tatizo la maji, elimu na pia
kurekebisha bei ya kahawa
Created by Gazeti la Habari leo
Friday, 18 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment