Friday, 11 September 2015

Tagged Under:

Mwinjilisti auawa kwa mishale

By: Unknown On: 00:49
  • Share The Gag
  • NA UPENDO MOSHA, KILIMANJARO MWINJILISTI wa Kanisa la Wasabato wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, Yese Milenyi (50), ameuawa kwa kuchomwa mishale na watu wasiojulikana.
    Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Flugence Ngonyani, alisema Mwinjilisti Milenyi aliuawa Septemba 8, mwaka huu saa 1:14 jioni katika Kijiji cha Mahongo Mterini.
    Kamanda Ngonyani alisema mwinjilisti huyo, aliuawa kwa kupigwa kwa mishale miwili sehemu ya shavu la kushoto na mwingine mgongoni na watu ambao hadi sasa hawajafahamika wakati akirudi nyumbani kutoka shambani.
    “Mwinjilisti huyu, alikuwa anatoka shambani kwake kurudi nyumbani, alikutana na watu ambao hawajafahamika, walichoma mishale miwili kwenye shavu lake la kushoto na mgongoni na kumsababishia kifo chake  papo hapo,” alisema Kamanda Ngonyani.
    Alisema chanzo cha mauaji hayo, hakijafahamika na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma kwa uchunguzi zaidi wa daktari.
    Alisema Jeshi la Polisi linandesha msako mkali ili kuwabaini waliohusika na mauaji hayo.
    Wakati huo huo, Kamanda Ngonyani alisema Sweetberth Magila (48), mwalimu wa Shule ya Sekondari Minja, ameuawa kwa kuchomwa kisu na mkewe kutokana na wivu wa kimapenzi.
    Alisema tukio hilo lilitokea Septemba 9, mwaka huu saa 2:20 usiku katika Kijiji cha Masumeni wilayani Mwanga.
    Kamanda Ngonyani alisema mwanamke huyo, Tumaini Magila (27), mwalimu wa Shule ya Sekondari Minja, alimchoma mumewe kisu kwenye paji la kushoto.
    Alisema baada ya kumchoma kisu, alivuja damu nyingi na kufariki dunia.
    Alisema kabla ya mauaji hayo, inadaiwa wanandoa hao walikuwa wakiishi pamoja, lakini wakiwa na ugomvi wa mara kwa mara kutokana na wivu wa kimapenzi huku mkewe akimtuhumu mumewe kuwa na mahusiano na mwanamke mwingine.
    “Kabla ya mauaji haya, walitoka pamoja kwenda kunywa pombe na baadae walirudi nyumbani, ambako baada ya muda walianza kugombana na kuanza kupigana… Wakati wakiendelea na ugomvi, mke alichukua kisu na kumchoma mume wake,” alisema Kamanda Ngonyani.
    Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa  Hosptali ya KCMC kwa uchunguzi zaidi na wanamshikilia Tumaini kwa upelelezi zaidi.

    Created  by Gazeti la Mwananchi

    1 comments: