Songea. Siku 10 tangu mgombea
wa urais kupitia chama tawala (CCM), Dk John Magufuli alipozindua
kampeni zake jijini Dar es Salaam zilizoambatana na ahadi mbalimbali kwa
lengo la kuleta mabadiliko ya kasi na kuijenga Tanzania mpya,
zilikamilika juzi.
Mgombea huyo anayetumia
kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, amekuwa akisisitiza zaidi mabadiliko na
kutangaza vita dhidi ya watendaji wazembe, wanaofanya kazi kwa mazoea
akiwataka wajiondoe endapo ataingia Ikulu.
Alitimiza
siku hizo 10 kwa mkutano mkubwa uliofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji
mjini Songea na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Katika
utekelezaji wa ilani ya CCM, Dk Magufuli amekuwa akiahidi baadhi ya
vitu kama; elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne,
kuboresha huduma za afya kwa kujenga zahanati na hospitali kila kijiji,
kata, wilaya na mkoa,
kukuza soko la mazao ya kilimo na ujenzi wa barabara za lami nchini.
Dk
Magufuli anasema pia kuwa atakachokiangalia ni pensheni kwa wazee,
mikopo ya Sh50 milioni kwa kina mama na vijana kwa kila kata, ujenzi wa
viwanda, usambazaji wa huduma za umeme, maji na kuboresha masilahi ya
wafanyakazi wote nchini na vyombo vya ulinzi na usalama.
Kwa
kipindi hicho cha siku 10 kutoka Wilaya ya Mpanda Vijijini hadi Songea
Mjini, mwandishi wetu ambaye ameambatana na mgombea huyo ameangalia kwa
ufupi baadhi ya mafanikio na changamoto za kisera katika kampeni za Dk
Magufuli.
Kuendana na ilani
Waziri
huyo wa Ujenzi amekuwa makini kwenye kuahidi miradi mikubwa ya
mabilioni ya fedha kama ujenzi wa daraja la Mto Ruhuhu, Barabara za
Njombe – Makete, Tabora – Ipole – Koga – Mpanda, reli ya kisasa kutoka
Mtwara – Songea – Mbamba Bay na matawi ya kwenda machimbo ya Mchuchuma
na Liganga mkoani Mbeya.
Utoaji wa ahadi hizo umemfanya
kuaminiwa na wananchi ambao wamekuwa wakitumia rekodi yake ya utendaji
katika wizara alizowahi kuongoza miaka 20 iliyopita ikiwamo ya Ujenzi.
“Ninaamini
anayosema atayatekeleza kwa sababu hata zile ahadi za barabara
amezitekeleza kikamilifu. Ni mkali anasimamia mambo,” anasema Esau
Bukila, mkazi wa Kijiji cha Lituhi, wilayani Nyasa.
Utoaji wa maagizo
Hata
hivyo, ahadi hizo na sifa za utendaji za Dk Magufuli, wakati mwingine
zimekuwa zikiambatana na maagizo ya moja kwa moja kwa watendaji husika
hasa kwa wale wa Wizara ya Ujenzi ambayo anaisimamia licha ya kuwa yupo
kwenye kampeni.
Akiwa Mbalizi, Mbeya Vijijini na
Makongorosi wilayani Chunya, mgombea huyo alimwagiza Meneja wa Wakala wa
Barabara Tanzania (Tanroads), atangaze haraka zabuni ya ujenzi wa
barabara ya kilomita moja ya Mbalizi na Makongorosi.
“Mkuu
wa Mkoa (Abbas Kandoro), nenda kamweleze meneja wa mkoa wa Tanroads
ndani ya wiki moja aanze kutekeleza ujenzi wa hii barabara.
Mwambie
aanze, nitazungumza na Ofisa Mkuu kule Dar es Salaam leo hii fedha zije
aanze kufanya kazi lakini mengine nitayafanya nikiteuliwa,” alisema Dk
Magufuli na kufafanua kuwa anaagiza kwa kuwa bado “ana kauwaziri wa
ujenzi hata kama ni mgombea.”
Kuwafikia wananchi wengi
Ndani
ya siku hizo, Dk Magufuli amekuwa akijitahidi kuhutubia karibu kila
eneo analokuta wananchi wamejikusanya au wamemzuia asipite mara nyingi
hadi awahutubie licha ya kutokuwapo kwenye ratiba ya mkutano.
Mwenyewe amekuwa akisema; “ameamua kufanya kampeni kwa kutumia barabara ili ayajue matatizo kwa kutaabika na wananchi.”
Hata
hivyo, mtindo huo umekuwa ukigharimu utunzaji wa muda na wakati
mwingine kumuathiri hadi ufanisi wa sauti kwa kuwa muda mwingi anautumia
kuhutubia.
Utii wa kusimama katika kila mkusanyiko
ulichangia kukausha sauti yake baada ya kuhutubia mikutano isiyopungua
12 ikilinganishwa na wastani wa mikutano mitano kwa siku wakati wa
safari ya Vwawa - Chunya na kupunguza ufanisi wa kampeni za Kyela,
Rungwe na Mbeya mjini siku iliyofuatia.
Kuunganisha makundi
Ni
dhahiri Dk Magufuli anatafuta njia madhubuti ya kuwanadi wagombea
ubunge wa chama hicho kwa wananchi lakini pia kuwaunganisha baadhi ya
makada waliogawanyika baada ya mtifuano wa kura za maoni za uteuzi wa
wabunge.
Katika mkutano amekuwa akiwanadi wabunge wa
majimbo husika na haraka kuwaomba wananchi “wawasamehe saba mara 70 kama
kuna makosa wamefanya” ili wapigie kura CCM kuanzia urais hadi udiwani.
Mfumo
huo, umeonekana kuwavutia makada wengi wa chama hicho tawala lakini ili
kuwapoza, Dk Magufuli amekuwa akiahidi kuletewa majina ya makada wote
walioshindwa kura za maoni ili awapatie kazi akiwa rais.
Ahadi za vyeo hivyo huenda zikaonekana lulu ya kuwaunganisha lakini hatari iwapo hatatimiza ahadi zake.
Kukisafisha chama
Mbali
na kuunganisha makundi ndani ya CCM, Dk Magufuli anafanya kazi kubwa ya
kuirudisha imani ya Watanzania kwa CCM baada ya chama hicho kukumbwa na
kashfa za utendaji mbovu na ufisadi.
Amekuwa akiwasihi wananchi kutoihukumu CCM kwa sababu ya waovu wachache ambao aliahidi kuwa akiingia madarakani, atawasafisha.
Amekuwa
akiwataka Watanzania kutokimbilia mabadiliko yasiyo na mipango kwa
shauku ya kuing’oa CCM ili kuyatimiza badala yake wampe urais ili akate
kiu yao ndani ya CCM.
“Wapo watu wanasema CCM imeoza tu
hata mngechagua nani, nataka niwaambie, hasa vijana, tusifanye
mabadiliko kwa jazba yakatuletea madhara kwa sababu mifano hai tunayo
duniani,” alisema Dk Magufuli mjini Mbinga na kutoa mifano ya mapinduzi
ya Libya yalivyoiacha nchi hiyo kwenye machafuko.
“Hivi
jamani kitanda kikiwa na kunguni unachoma kitanda? Hapana, unachofanya
ni kuwaua kunguni ili ulale kwa amani na raha mustarehe.”
Pamoja
na kukisafisha chama, kauli za Dk Magufuli wakati mwingine
zinatafsiriwa na upinzani kama njia ya kutengeneza hofu ya mabadiliko
miongoni mwa wananchi.
Vyanzo vya mapato
Mara
nyingi Dk Magufuli amekuwa akieleza kuwa Serikali yake itapunguza
sherehe zisizo na tija kama siku ya maziwa, maji au nyama ili kutunza
fedha za umma, lakini undani katika vyanzo vingine hasa vya kodi umekuwa
ukisikika kwa wastani.
“Wapo watu watasema hizo ni
siasa tu atatoa wapi wa fedha? Nchi hii, tajiri ina makaa ya mawe, ina
maziwa 21, bahari kubwa mpaka watu wanaiba tu pesa, madini ya kila aina,
wanyama, mifugo, hatuwezi tukashindwa, naomba mnipe urais niwafanyie
kazi,” anaeleza Dk Magufuli.
Anasema fedha ziko pia
katika maeneo ya utalii, kuwabana wasiolipa kodi na kwamba wakubwa na
wadogo wote walipe kodi na kuziba kwa kiasi kikubwa mianya ya rushwa kwa
kuongeza ufanisi wa kazi.
Vijembe
Licha
ya mgombea huyo kutangaza mara kadhaa kuwa atafanya kampeni safi
zisizomtukana mtu yeyote, baadhi ya makada wanaomnadi wamekuwa
wakimwangusha kwa kutumia jukwaa hilo kupiga vijembe na kutumia lugha za
maudhi kujibu mapigo ya upande wa pili wa upinzani hasa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akihutubia
wakazi wa Songea Mjini, mgombea huyo alisema: “Hatutamtukana mgombea
yeyote. Sisi tutafanya kampeni za kistaarabu kwa sababu tunahitaji kura
za Watanzania wote na hivi ndivyo ninavyotaka uongozi wangu uwe.”
Lakini
dakika sita tu baada ya kauli hiyo, Dk Magufuli alimwachia jukwaa
mjumbe wa kamati ya kampeni, Mwigulu Nchemba ambaye tangu sekunde ya
kwanza hadi ya mwisho alikuwa akirusha vijembe akiomba “kuweka
kumbukumbu na mambo sawa kwa Watanzania” ili watakapokuja upinzani
kuwadanganya wawe na majibu.
Vijembe hivyo vilivyoanzia
mkoani Mbeya kwa kuwaponda mgombea wa urais wa Chadema kupitia Ukawa,
Edward Lowassa na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye viliendelea
juzi ikiwa ni majibu ya vile vilivyotolewa siku ya uzinduzi wa kampeni
za Ukawa.
Pia, kada mwingine Amon Mpanju naye kwa siku
tatu zilizopita ameonekana kuwa mtambo wa vijembe kwa Ukawa akieleza
kuwa rais anayefaa ni Dk Magufuli wengine ni maigizo na mambo mengine
ambayo siyo rahisi kuandikika.
‘Mimi ni maji moto kuunguza mafisadi’
Jana,
akiwa Newala Mjini, Dk Magufuli aliwaomba Watanzania wamchague kwa kuwa
yeye ni maji ya moto ya kuwaunguza mafisadi wanaotafuna fedha za umma
na kuchelewesha maendeleo.
Akiwa katika Uwanja wa CCM –
Sabasaba, Dk Magufuli alisema hakuna haja ya kuichukia Serikali kwa
sababu ya mafisadi wachache aliowafananisha na kunguni kitandani ni
rahisi kuwaondoa.
Huku akishangiliwa na umati
ulijitokeza mahali hapo saa tatu asubuhi alisema: “Mimi ni maji ya moto
kwa mafisadi nipeni urais muone nitakavyowaunguza.”
Katika
mwendelezo wa ahadi zake mkoani Mtwara, msisitizo mkubwa aliuweka zaidi
katika namna atakavyokuza uchumi wa eneo hilo kwa kutumia gesi asilia
na kuongeza thamani ya zao la korosho kwa kujenga viwanda. Aliahidi pia
kujenga Barabara ya Masasi – Newala – Mtwara kwa kiwango cha lami.
“Nipeni
tu urais tuwaletee maji kwanza huyo waziri wa maji nitakayemteua,
hatashinda Dar es Salaam akisherehekea wiki ya maji. Katika uongozi
wangu sipendi ubabaishaji. Nikisema A basi ni A na nikisema mti unakuwa
mti ndiyo maana wale mafisadi walipoona nimeteuliwa walikimbia wenyewe,”
alisema na kushangiliwa.
Mgombea huyo ambaye yupo
katika siku ya 11 ya kampeni zake, alipofika katika Kijiji cha Lidumbe,
Newala saa 4.02 asubuhi, alijumuika na wanakijiji kuomboleza msiba wa
Zainabu Abdallah aliyefariki juzi na kutoa ubani wa Sh400,000.
Mmoja
wa ndugu wa marehemu huyo, Sofia Litonji alimwambia mwandishi wetu kuwa
amefurahishwa na kitendo cha Dk Magufuli kuwapatia pole kwa kuwa siyo
kawaida kiongozi wa ngazi yake kufanya hivyo.
Mtwara Mjini
Akiwa
Mtwara Mjini, alipokewa na maelfu ya wakazi wa ambao aliwaahidi kuwa
rasilimali ya gesi asilia iliyogundulika katika eneo hilo itatumika
kuwanufaisha wao kwanza na taifa kwa ujumla kwa kujenga viwanda vikubwa
na kuzalisha ajira.
Aliingia Mtwara Mjini saa 9.10 alasiri na kupokewa na msafara wa bodaboda hadi katika Uwanja wa Mashujaa.
Huku
akionekana mwenye furaha kubwa, Dk Magufuli alisema: “Awamu ya nne
imeshaanza kujenga viwanda hapa ikiwamo Kiwanda cha Saruji cha Dangote,
katika utawala wangu nitatandika viwanda kote hapahapa Mtwara.
Sehemu kubwa ya hotuba zake tangu alipoingia mkoani hapa amekuwa akizungumzia gesi.
Itakumbukwa
kuwa wakazi wa mkoa huo waliitikisa Serikali mwaka 2013 wakiigomea
isijenge bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa
madai kuwa ikisafirishwa hawatanufaika nayo na kubaki maskini.
Hata
hivyo, akiwa Ziwani, Mtwara Vijijini moja ya maeneo inakopatikana gesi
hiyo, wananchi walimpokea kwa shangwe naye kuwaambia: “nina deni la
kuwaletea maendeleo.”
Created by Gazeti leo
Created by Gazeti leo
0 comments:
Post a Comment