MWENYEKITI wa CCM mkoa wa Geita, Joseph Msukuma akihutubia mkutano wa hadhara mjini Chato.
MWENYEKITI wa CCM mkoa wa Geita, Joseph Msukuma amemvaa mgombea wa
urais kupitia Chadema, Edward Lowassa na wengine waliohamia Ukawa
akisema wanashukuru chama kimetua mzigo.
Msukuma, ambaye anaaminika kuwa swahiba wa Lowassa wakati wa mchakato
wa kura ya maoni kwenye CCM, aliuambia mkutano jana kwamba hakuna
anayefahamu siri za Lowassa.
“Nataka nimwambie ndugu yangu, rafiki yangu Lowassa, huu ni muziki
mkubwa,” alisema Msukuma kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea wa urais
wa CCM, Dk John Magufuli uliofanyika jana mjini Chato, mkoani Geita.
Msukuma ambaye aliponda waliohama CCM baada ya kura za maoni kwa
kutaja majina ya baadhi, akiwalinganisha na bendera inayofuata upepo na
kusisitiza kuwa wenye akili hawahami.
“Tumeshukuru sana CCM tumetua mizigo…”, alisema Msukuma ambaye ni
mgombea ubunge, Jimbo la Geita Vijijini akiwataja Lawrence Masha,
Msindai, Mngeja akisema wamehamia Ukawa si kwa mapenzi mema isipokuwa,
ni kutokana na kukosa ushindi kwenye kura za maoni.
“Tuna hasara gani Masha akihama CCM?” alihoji umati ambao uliitikia
kwa kusema hakuna hasara. Msukuma ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi
wa CCM waliohudhuria mkutano wa Lowassa uliofanyika Arusha wakati wa
mchakato wa kura za maoni, akisifia mkutano wa jana wa Magufuli,
alisema, “Toka niwe mwenyekiti sijawahi kuona watu wengi kama hawa.
Hata nilipoteremka Arusha na chopa, haikuwa hivi.” Alieleza
kushangazwa na baadhi ya picha zilizooneshwa kuwa ni za mkutano wa
Lowassa mjini Chato na kusema mandhari iliyooneshwa, haikuwa ya uwanja
huo wa stendi.
“Stendi ya Chato haina miembe wala lami,” alisema. Akiendelea kuponda
waliohama, alisema, kama Dk Magufuli angekuwa anatoa rushwa,
wasingehama. “Hakuna hasara na wote waligombea wakashindwa,” alisema na
kueleza kumfahamu Mngeja kwa kuwa walikuwa wakikaa kwenye helikopta
moja.
“Tunaomba wachukue na wengine wenye tabia kama hizo. Wenye akili
timamu tutabaki CCM...Mgombea wetu (Magufuli) anatosha. Na hapa ndiyo
kwao…nimetembea na Lowassa gari moja, ndege moja, tunachagua rais na sio
bora rais…,” alisema.
Alisisitiza, “Katika Kanda ya Ziwa, hakuna aliye na siri za Lowassa
kama mimi…naomba waniweke kwenye mdahalo nitagharimia, niwapige kavu
kavu. Watu wanaokwenda kule (Ukawa) zinatangulizwa hela. Nani anachukia
hela?.”
Aliendelea kusema, “najua mengi ya kambi ile nilikwenda kufanya kazi.
Hata wale wachungaji waliokwenda Dodoma, ni wachungaji feki
walionunuliwa.” Mke wa Magufuli Mke wa Magufuli, Janeth, alishukuru wana
Chato kwa kumpa heshima kubwa mbunge wao kwa kipindi chote cha miaka 20
hadi chama kikamteua kuwa mgombea urais.
Wakati akizungumza, zilisikika sauti kutoka kwenye mkutano
zikishangilia ‘rais rais’. Mke huyo wa mgombea aliomba Oktoba 25 wana
Chato wamchague kwa wingi. Aliomba pia wamchague Dk Medard Kalemani kuwa
mbunge wa Chato. Ameomba pia wachague madiwani wa CCM wapeperushe
bendera vyema.
Created by Gazeti la HabariLeo
Monday, 21 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment