CHAMA cha ACT- Wazalendo kimejipanga kutatua kero ya maji kwa
wananchi vijijini ili kuwakomboa kinamama wanaopata shida ya kutafuta
maji kwa kuanzisha Mamlaka ya Maji Vijijini.
Akizungumza na wakazi wa Tabora katika maeneo tofauti, Kiongozi wa
chama hicho, Zitto Kabwe alisema ACT-Wazalendo imeandaa mpango maalumu
ambao umeainishwa katika ilani yao ya uchaguzi, ambayo inalenga
kuwakomboa wananchi.
Zitto alisema wagombea mbalimbali wamekuwa wakitoa ahadi lukuki
wakijinadi kutatua tatizo la maji kwa wananchi wa vijijini, lakini
hazijatekelezwa kutokana na kwamba hawakuwa na mpango madhubuti wa
kumaliza tatizo hilo.
“Kila watu 100 watu 62 vijijini hawana maji safi na salama huku ndiko
wanakoishi watanzania wengi, sisi tutamaliza tatizo hilo,” alisema.
Ilani ya ACT -Wazalendo inasema chama kitaanzisha Mfuko wa Maji
Vijijini utakaotumika kuendeleza na kulinda vyanzo vya maji vijijini na
kukarabati miundombinu ya maji mijini na katika majiji.
Alisema wananchi watahamasishwa kuhusu umuhimu wa kuendelea kutunza vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.
Zitto alisema wabunge waliopita mkoa wa Tabora hawakuwa na
ushirikiano na walikuwa wakigombana bungeni kila mara, jambo ambalo
lilifanya washindwe kutatua kero za wananchi waliowatuma na kuzitetea
kwa pamoja.
“Wabunge wa Tabora sifa yao kubwa ni kugombana, sio kuzungumzia
changamoto zao na wananchi wao, hawana umoja katika hoja zao,” alisema
Zitto na kuwahakikishia wananchi hao kwamba sasa wanataka wabunge wa
Kigoma na Tabora kushirikiana kuondoa matatizo ya mikoa hiyo.
Mgombea udiwani wa kata ya Kamsekwa kijiji cha Igagala, aliahidi
atakapoingia madarakani atawasaidia wananchi kuchimba visima virefu,
ambavyo vitawasaidia wananchi kuondokana na tatizo la kutembea muda
mrefu kutafuta maji ambayo yanapatikana mbali na sio salama.
Aidha, aliahidi pia kuwasaidia wanawake kwa kununua gari aina ya
Toyota Noah kwa ajili ya kubeba wagonjwa na kinamama wanaoenda
kujifungua hospitali. Wananchi walilalamikia tatizo la maji safi na
salama katika vijiji vyao kuwa ni kikwazo kikubwa na cha muda mrefu.
Walisema hupoteza muda mwingi kutafuta maji.
Created by Gazeti la Habari leo
Sunday, 20 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment