Mwenyekiti wa Chadema ,Freeman Mbowe akihutubia katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais kupitia chama hicho ,Edward Lowassa uliofanyika katika uwanja wa kizwitwe ,mjini Sumbawanga jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Rukwa. Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe amesema Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa
aliyetangaza kujiondoa ni sawa na abiria wa treni ya kati aliyeshukia
njiani kabla ya mwisho wa safari, huku mgombea urais wa chama hicho
chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa akisema: “Tanzania ya CCM
sasa basi, ni wakati wa mabadiliko.”
Akizungumza
katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi
Nduwa, Sumbawanga, Mbowe akiwa sambamba na Lowassa alisema hakuna
kiongozi wa Chadema ambaye ni mkubwa kuliko chama hicho.
“Mtu
yeyote anaweza kuondoka katika chama lakini kikabaki salama na
kuendelea na safari yake ya mabadiliko,” alisema na kushangiliwa na
maelfu ya wananchi wa mji huo waliojitokeza kwa wingi katika Uwanja wa
Ndege wa Sumbawanga kuwapokea viongozi hao wakitokea Ruvuma.
Juzi,
Dk Slaa alitangaza kuachana na siasa za vyama kutokana na kutofautiana
na viongozi wa Chadema juu ya masharti ya kumpokea Lowassa.
Mbowe
ambaye alipokewa na mabango ya kumtaka atoe kauli kuhusu Dk Slaa
alisema: “Watu wengi waliniambia nikifika hapa nizungumze habari ya Dk
Slaa sasa ngoja niwaambie kwa kifupi sana.”
Alisema
mwaka 1992, Chadema kilipoundwa kilianza safari yake, akiifananisha na
ile ya treni ya Reli ya Kati inayoanzia Dar es Salaam hadi Kigoma,
kwamba katika safari hiyo wapo wanachama walioshukia njiani, akimaanisha
walioamua kuachana na chama hicho... “Tukafika Pugu wapo walioshuka na
wengine wakapanda, tulipofika Morogoro wapo walioshuka na wapo
waliopanda. Oktoba mwaka huu treni itafika Kigoma mwisho wa reli na
tutaingia Ikulu,” alisema.
Alisema vikao vya Baraza
Kuu, Kamati Kuu na Mkutano Mkuu wa chama hicho vilikubali Lowassa kuwa
mgombea urais wa Chadema na Ukawa... “Hiyo ndiyo habari ya mjini, sasa
kama kuna mtu na mke wake wana mawazo tofauti watatukuta mbele ya
safari. Hatuna muda wa kupoteza tunahitaji mabadiliko.”
Mbowe
aliwataka askari kuwalinda wananchi kwa maelezo kuwa Oktoba 25 wataamua
hatima ya nchi yao kwa kukichagua Chadema kuingia Ikulu na kusisitiza
kuwa uamuzi ya Watanzania hausababishwi na mapenzi kwa Chadema, bali
maumivu, tabu, umaskini, ujinga, kukosa maji, matumizi mabaya ya
rasilimali za nchi na ukosefu wa pembejeo.
“Tusijenge
uadui na askari polisi kwa sababu ni ndugu zetu, wadogo zetu, baba zetu
na tunawahitaji kama wao wanavyotuhitaji, nao wanahitaji mabadiliko
kwani wapo hoi,” alisema.
Mbowe aliwataka wanaCCM kuiga
mfano wa Lowassa kwa kujiunga na mabadiliko na kuwataka wanachama wa
Chadema kuwashawishi wanachama wa chama hicho tawala kujiunga na safari
ya mabadiliko.
Lowassa apunguziwa safari
Alisema
Chadema kimeunda timu nne zitakazoundwa na wabunge wake kwa ajili ya
kuzunguka mikoa mbalimbali kufanya kampeni kwa maelezo kuwa Lowassa
hawezi kumaliza majimbo yote ya uchaguzi ndani ya siku 60 za kampeni
zilizopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Alisema wabunge hao watatumia helikopta (chopa) nne kuzunguka katika majimbo mbalimbali.
Wabunge
hao waliomaliza muda wao na majimbo wanayogombea katika mabano ni Tundu
Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini), David Silinde
(Momba), Ezekia Wenje (Nyamagana), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Halima
Mdee (Kawe), John Mnyika (Kibamba) na yeye mwenyewe.
Alisema
kuna majimbo ya uchaguzi 265 na Lowassa akifanya kampeni katika majimbo
manne kwa siku, atamaliza majimbo 240 ndani ya siku 60, kwamba yapo
ambayo atashindwa kuyafikia.
Lowassa
Akizungumza
katika mkutano huo, Lowassa alisema licha ya kutawala kwa miaka zaidi
ya 50, CCM imeshindwa kumaliza matatizo yanayowakabili wananchi. “Nipeni
dhamana ya kuibadilisha nchi yetu kwani chama hiki (CCM), kipo miaka 50
lakini hakuna kilichofanya. Nipigieni kura na kulinda kura yako.”
Lowassa
alisema akiwa rais wa awamu ya tano, elimu itakuwa bure na atafuta kodi
na ushuru kwa wakulima, kusisitiza kuwa anataka kuwaonyesha Watanzania
kuwa anaweza kuwaletea mabadiliko na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye
maendeleo makubwa.
Aanza kutumia chopa
Jana,
Lowassa alianza kutumia chopa katika mikutano yake ya kampeni ili
kurahisisha kuwafikia wapiga kura wengi zaidi. Mbali na chopa, mgombea
huyo ambaye ameshafanya mikutano ya kampeni katika mikoa ya Iringa,
Njombe na Ruvuma pia atatumia ndege.
Jana aliruka na chopa kutoka Songea Mjini na kufanya mikutano Mbinga na Namtumbo na baadaye Sumbawanga.
Mkuu
wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema:
“Tutakuwa na chopa nyingi si moja lakini hawezi kuitumia kila siku na
kuna maeneo atatumia ndege. Suala la matumizi ya chopa pia linahitaji
vibali.”
Kwa mujibu wa ratiba ya NEC leo Lowassa
atafanya mkutano wa kampeni Mlele na Mpanda mkoani Katavi na kesho
atakuwa mkoani Kigoma ambako atafanya mikutano Uvinza, Kigoma Vijijini
na Kigoma Mjini.
Keshokutwa atakuwa Tabora ambako atatumia siku mbili kufanya mikutano wilaya za Sikonge, Urambo, Tabora Mjini, Nzega na Igunga.
Septemba
7, atafanya mkutano jijini Dar es Salaam katika jimbo la Kibamba na
Bunju na kuendelea katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyanga,
Simiyu, Geita, Kagera na Mtwara.
0 comments:
Post a Comment