Thursday, 24 September 2015

Tagged Under:

Zanzibar itamuenzi Karume kwa kutoa elimu bure

By: Unknown On: 03:10
  • Share The Gag
  • Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, Dk Ali Mohamed Shein.

    MIONGONI mwa mambo yaliyokuwa kero na kikwazo kwa wazazi kusomesha watoto wao elimu ya sekondari ni ada iliyokuwa ikitozwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali. Ada ilikuwa kikwazo kwa kuwa baadhi ya wazazi hawakuwa na uwezo wa kutoa fedha za michango hiyo na wengine wana zaidi ya mtoto mmoja.
    Ni kutokana na ugumu huo baadhi ya wanafunzi wanarudishwa makwao kwa sababu ya kukosa ada au michango ya mitihani ya majaribio. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa jibu la tatizo hilo. Mgombea wake kwa nafasi ya urais Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein ametangaza kwamba, michango na ada zote kwa wanafunzi wa sekondari zinafutwa.
    Shein anatangaza uamuzi huo katika uwanja wa mchezo Chokocho Pemba wakati akinadi sera zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 na kusema hakutakuwa michango wala ada kwa wanafunzi wa sekondari za Unguja na Pemba. Dk Shein anasema huu ni ulimwengu wa sayansi na teknolojia hivyo wanafunzi wa shule za sekondari wanatakiwa kujengwa na kukuzwa katika elimu.
    Anasema, uamuzi huo utapunguza mzigo uliokuwa ukibebwa na wazazi kwa ajili ya kugharamia elimu ya watoto sekondari hadi kuelekea chuo kikuu. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, uamuzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais wa kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Amani Karume ambaye ametangaza elimu bure kwa wanafunzi wote wa Unguja na Pemba ilipofika Septemba 23 mwaka 1964.
    Anasema uamuzi ule wa mwaka 1964 unakwenda sambamba na kutangaza elimu bure na kuzifuta shule zote zilizokuwa zikitoa elimu kwa njia ya ubaguzi wa makabila. “Wananchi mkinichagua kuwa Rais wa Zanzibar naahidi kufuta michango na ada zote zilizokuwa zikitolewa na wazazi kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari Unguja na Pemba,” anasema. Ada zilizokuwa zikitozwa kwa wanafunzi wa sekondari ni pamoja na zile za kufanya mitihani ya taifa ,ya majaribio na zile za kila mwaka mpya unapoingia.
    Dk Shein anasema, ahadi hiyo ataifuatilia kwa karibu kuona kwamba taasisi husika na wizara wanatekeleza agizo hilo bila ya matatizo. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, atahakikisha kwamba mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu inaongezeka maradufu hasa kwa wanafunzi wa kike ambao wameonesha ari kubwa na mapenzi ya kutafuta elimu.
    Anasema kwa muda mrefu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekuwa ikitoa wito kwa wanafunzi wa kike kuongeza juhudi ya kutafuta elimu ili kuondokana na tatizo la kuwa tegemezi kwa wanaume. Dk Shein anasema, katika miaka mitano ataongeza idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaopata mikopo kutoka 2,658 hadi kufikia 22,404 ikiwa ni sawa na asilimia 11. Si hivyo tu, kitajengwa chuo kikuu kipya Dole mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
    Katika utoaji wa mikopo vipaumbele zaidi vitawekwa kwa wanafunzi wa kike katika masomo ya sayansi ikiwemo uhandisi na udaktari. Anasema wanafunzi wa kike wameonesha uwezo mkubwa katika masomo ya sayansi huku wakiongoza katika shule za sekondari na vyuo vikuu ikiwemo idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu mitihani ya mwisho.
    Kiongozi huyo anasema, Wizara ya Elimu tayari imekamilisha utaratibu wa kutenga baadhi ya shule kutumika kwa wanafunzi wa kike tu na kwamba shule ya sekondari ya Utaani iliopo Pemba na Ben Bella ya Unguja zinatoa elimu kwa kundi hilo. Anasema kati ya mwaka 2012 hadi 2014 wanafunzi wa sekondari kuanzia darasa la tisa hadi la 14 imeongezeka kutoka 78,165 hadi 79, 662.
    Kati ya wanafunzi hao wavulana ni 36,361 , wasichana 41,804. Dk Shein anasema, shule za sekondari zimeongezeka Unguja na Pemba kutoka 194 katika mwaka 2010 hadi kufikia 213 katika mwaka 2014. Anayataja mafanikio ya ujenzi wa shule 19 za kisasa za sekondari zilizoleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu kwenye masomo ya sayansi.
    Kwa mujibu wa Dk Shein, shule hizo zote zina vifaa vya maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi ya Fizikia, Baiolojia na Kemia hivyo wanafunzi wanafanya kazi zao za vitendo zaidi. “Shule 19 tulizojenga ni kwa ajili ya wanafunzi wa masomo ya sayansi kwani vifaa vya maabara vya kisasa vinapatikana bila ya matatizo,” anasema. Kiongozi huyo anasema, madarasa mapya 263 yamejengwa, shule 6 maarufu za zamani zilizokuwepo katika kipindi cha ukoloni zimefanyiwa matengenezo ili kuwawezesha wanafunzi zaidi kupata elimu.
    Shule hizo ni Fidel Castro ya Pemba na Utaani ambayo sasa inatumiwa na wanafunzi wa kike tu. Shule nyingine ni Tumekuja, Hamamni, na Donge. “Majengo ya shule za sekondari yaliyojengwa tangu utawala wa kikoloni yote tumeyafanyia ukarabati mkubwa wa kisasa,” anasema. Dk Shein anasema, ili kuboresha elimu katika shule za msingi na sekondari Serikali imejizatiti kuwaendeleza walimu kuanzia cheti hadi stashahada.
    Anasema, vituo vya mafunzo ya elimu vitaimarishwa kwa ajili ya kuwaandaa walimu waweze kupata taaluma nzuri ili watekeleze vizuri wajibu wao. Kiongozi huyo anasema, elimu ya ujasiriamali itapewa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wanaohitimu waweze kujiajiri. Anasema wakati umefika kwa vyuo vya amali kuimarishwa ili kuwawezesha wanafunzi wanaohitimu waweze kuingia katika soko la ajira na kuajiriwa.
    “Vyuo vya Amali katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 tumeweka kipaumbele kuviendeleza kwa ajili ya kupata vijana ambao wataweza kujiajiri na kupunguza tatizo la ajira,” anasema.
    Hizo ndiyo ahadi za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015 kwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho Dk Ali Mohamed Shein katika sekta ya elimu.
    Created by Gazeti la HabariLeo


    0 comments:

    Post a Comment