Zanzibar. Mgombea urais wa
Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif
Hamad amesema kama atapewa ridhaa ya kuwa rais atahakikisha Zanzibar
inapata mamlaka kamili.
Akihutubia wananchi leo kwenye
uzinduzi wa kampeni za Cuf katika viwanja vya Kibanda Maiti visiwani
Zanzibar, Maalim Seif amesema kuwa kama wananchi watamchagua atapigania
kupata serikali ya Muungano yenye serikali tatu.
“Kama
mtanichagua kitu cha kwanza, nawaahidi wananchi wa Zanzibar ni kupata
serikali ya muungano yenye serikali tatu… Zanzibar kuwa na mamlaka
kamili na kurejesha rasimu ya Jaji Warioba’’ amesema Maalim.
Hii ni mara ya tano kwa Maalim ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kugombea nafasi ya urais.
Mgombea
huyo ambaye ametumia dakika zisizozidi 15 kueleza vipaumbele vya
serikali yake, amesema kuwa atarejesha misingi ya utawala bora ili
wananchi waishi kwa amani.
Pia Maalim ameeleza kuwa,
atahakikisha anajenga uchumi imara na unaokua kwa kasi ikiwa ni sehemu
ya ndoto yake ya siku nyingi katika harakati za maendeleo.
“lingine
ni kujenga uchumi imara na unaokuwa kwa kasi, hiyo ndio ndoto yangu ya
kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki… kwa kuhakikisha
kujenga bandari ya kisasa, sio kwa maneno lakini kwa matendo’’ alisema.
Sambamba
na hayo, amewaahidi vijana kupata ajira na mitaji ili kujiendeleza
kimaisha ‘’ Nitafungua benki ya uwekezaji ya Zanzibar ili kutoa mitaji
kwa vijana wetu wanaojihusisha na uvuvi ili wamudu kujiendeleza na
kujiajiri’’ alisisitiza Maalim.
Aidha, katika kumalizia
vipaumbele vyake, Maalim ameahidi kuwa siku 100 za mwanzo ndani ya
utawala wake atahakikisha sheria ya mafuta na gesi inapatikana ili
kuanza kuchimba mafuta visiwani humo.
Katika uzinduzi
huo wa kampeni, pamoja na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi, viongozi
mbalimbali, pia tukio hilo limehudhuriwa na mgombea urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward
Lowassa na mgombea mwenza Juma Duni Haji.Created by Gazeti la Mwananchi
0 comments:
Post a Comment