MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama hicho kimechukua
majimbo mengi katika kuachiana majimbo na kata, kutokana na makubaliano
ya kuwa mgombea atasimamishwa kulingana na chama kinachokubalika katika
jimbo husika.
Amesema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam kuhusu mambo mbalimbali, ikiwemo taarifa kuwa Chadema inalenga
kuvunja upinzani kutokana na mgawanyo wa majimbo kwa vyama vinavyounda
umoja huo.
Kwa mujibu wa Mbowe, katika suala hilo la kuachiana majimbo, pia
walikuwa wanaangalia katika uchaguzi wa mwaka 2010 jimbo hilo nani
alishinda na aina ya mtu kama anaweza kuongoza au la.
Mbowe aliwajia juu Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Leticia Mossore
na Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe, kwa kumshutumu
Mwenyekiti wao, James Mbatia kwa madai ya kutaka kuua chama chao cha
NCCR-Mageuzi.
Alisema shutuma zilizotolewa na viongozi hao zinatokana na kutaka
kuachiwa majimbo bila kuzingatia vigezo vilivyowekwa na umoja huo,
ambapo alisema Mossore alitaka aachiwe jimbo la Segerea huku akijua wazi
jimbo hilo walistahili kupewa Chadema.
“Kama mnakumbuka uchaguzi wa mwaka 2010 jimbo lile alishinda
Mpendazoe wa Chadema, kwa hiyo hata mwaka huu ilitakiwa sisi ndiyo
tusimamishe lakini viongozi wa CUF walikuja tukakaa mezani wakasema
tumweke Mtatiro na tukakubali,” alisema.
Alisema Nyambabe alitaka aachiwe jimbo la Serengeti, ambapo alisema,
kwanza hakubaliki lakini hata Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, NCCR
hawakupata kura katika jimbo, pia katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliofanyika mwaka jana pia hawakuchukua mtaa wowote.
Created by Gazeti la Habari Leo
Sunday, 20 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment