SHIRIKISHO la Soka Tanzania, (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo
wa watani wa jadi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania utakaochezwa
Jumamosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo kiingilio
cha chini kitakuwa ni Sh 7,000.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Habari wa TFF, Baraka
Kizuguto alisema kuwa, katika mchezo huo kiingilio cha juu kitakuwa ni
Sh 30,000 kwa viti vya VIP A, 20,000 kwa viti vya VIP B & C, huku
kiingilio cha 7,000 kikiwa ni kwa viti vyenye rangi ya Bluu, Kijani na
Orange.
“Mchezo wa Jumamosi (keshokutwa) viingilio vyake ni Sh 7000, 20,000
na 30,000 pia mchezo utaanza saa 10:00 jioni,” alisema Kizuguto. Pia
aliwataka mashabiki kutoonesha hisia za vyama wala kuvaa fulana zenye
kuonesha wapo chama gani ili mchezo uwe wa amani na utulivu.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi wa kimataifa mwenye beji ya FIFA,
Israel Nkongo Dar es Salaam akisaidiwa na Josephat Bulali Tanga,
Ferdinand Chacha toka Mwanza, mwamuzi wa akiba Soud Lila wa Dar es
Salaam wakati kamisaa wa mchezo huo atakuwa Charles Mchau kutoka
Kilimanjaro.
Pia Kizuguto alisema tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa kesho
Ijumaa saa 2:00 asubuhi katika vituo vifuatavyo: Karume – Ofisi za TFF,
Buguruni – Oilcom, Dar Live – Mbagala, Uwanja wa Taifa, Luther House –
Posta, Ferry – Kivukoni, Mnazi Mmoja, Ubungo – Oilcom na Makumbusho –
Standi ya mabasi ya daladala.
TFF inawaomba wapenzi, wadau na mashabiki wa mpira wa miguu nchini
kununua tiketi katika magari yaliyopo kwenye vituo vya kuuzia tiketi ili
kuondokana na kuuziwa tiketi zisizo sahihi.
Simba na Yanga zinakutana katika mchezo wa raundi ya nne wa Ligi Kuu
bara huku Yanga ikiwa haijapata ushindi dhidi ya Simba tangu Mei, 2013
waliposhinda kwa mabao 2-0. Hii inamaanisha mabingwa Yanga wataingia
uwanjani kusaka ushindi wao wa kwanza ndani ya miaka miwili.
Aidha, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limejipanga
kikamilifu kuhakikisha kuwa pambano la mpira wa miguu kati timu za Simba
na Yanga lenye kuvuta hisia kwa mashabiki wengi wa hapa Tanzania, na
nchi jirani linafanyika katika hali ya amani na usalama.
Wananchi wanashauriwa wasiwe na shaka yoyote ya kiusalama na pia
watupe ushirikiano kwa kutoa taarifa za jambo lolote watakaloliona kuwa
linaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani kwa kipindi chote
watakapokuwa nje au ndani ya uwanja.
Wananchi wanatakiwa kuwa watulivu wakati wa kushangilia mechi hiyo
huku kila mmoja akiwa amekaa kwenye kiti kulingana na tiketi aliyokata
ili kuondoa usumbufu usiokuwa wa lazima.
Craeted by Gazeti La HabariLeo
Thursday, 24 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment