NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
RAIS Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, kufuatia kifo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti na Utumishi wa Umma, Celina Kombani, kilichotokea
juzi katika Hospitali ya Apollo nchini India alipokuwa akipatiwa
matibabu baada ya kugundulika kuwa na saratani.
Rais Kikwete pia amemtumia salamu za pole mume wa marehemu, Swaleh
Ahmad Pongolani, watoto, ndugu na jamaa kutokana na msiba huo.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu
ilisema marehemu Kombani atakumbukwa kwa kuwa hodari na aliyependa
kushirikiana na wenzake na kwamba wamepoteza mama mchapakazi.
“Nimepokea taarifa za kifo cha mama Kombani kwa huzuni kubwa, najua
machungu na maumivu mliyonayo kwa kuondokewa na kiungo muhimu katika
familia yenu, poleni sana, mama ni nguzo ya familia niko nanyi katika
msiba huu mzito kwenu,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema pamoja na kwamba kifo hakiepukiki, bado ni kitu ambacho kinashtua, kuhuzunisha na
kuleta unyonge mkubwa kwa wafiwa katika jamii.
“Naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu kumuombea Mama Kombani ili
Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema ya milele, nawaombea wana familia na
ndugu wa marehemu, Mwenyezi Mungu awatie nguvu, uvumilivu na
subira katika kipindi hiki, niko nanyi katika kipindi hiki kigumu kwa
hali na mali, nawaomba msijisikie wapweke,”
alisema Rais Kikwete.
Mwili wa marehemu Kombani unatarajia kuwasili nchini leo mchana na
kuzikwa shambani kwake mkoani Morogoro. Marehemu Kombani alikuwa mgombea
ubunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na tayari alikwishalitumikia jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 10.
Kombani alizaliwa Juni 19, 1959 na ameacha mume, watoto watano na wajukuu wanne
Created by Gazeti la Mtanzania
Saturday, 26 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment