*Asema kitanda chenye kunguni hakichomwi moto
*Ataka wananchi waichague CCM, aahidi kushughulikia ‘mchwa’
Bakari Kimwanga na Raphael Okello, Bunda
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli
amewaangukia wananchi na kuwaomba wasikiadhibu chama chake katika
uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao.
Mgombea huyo amewaomba wananchi kuichagua CCM na kuahidi
kuwashughulikia watu ambao amewaita kuwa ni mchwa, endapo watampa
ridhaa.
Akihutubia mamia ya wananchi wa mji wa Bunda mkoani Mara jana, Dk.
Magufuli alisema amejipanga vizuri kuwateketeza mchwa hao mara tu baada
ya kuingia madarakani.
“Nawaoamba wananchi msiiadhibu CCM, kwa kuwa nimejipanga kuwashughulikia mchwa serikalini.
“Nawaomba wana Bunda msiipe CCM adhabu…kama ambavyo huwezi kuchoma
kitanda kinachoingiliwa na kunguni, badala yake utachoma kunguni, acheni
tuwachome kunguni walioko serikalini,” alisema Magufuli.
Kuhusu suala la kuwapatia wananchi wa Bunda maji, Dk. Magufuli alisema.
“Niwaahidi wanabunda, mtapata maji ndani ya miezi mitatu tangu
kuunda baraza langu la mawaziri… kama waziri wa maji atashindwa
kutekeleza ahadi hii, waziri huyo atageuka kuwa maji,” alisema huku
akishangiliwa na mamia ya wananchi.
Alisema kila sehemu ambayo amekuwa akipita, amekuwa na kazi ya
kuwaombea msamaha wagombea ubunge na udiwani na kuwasihi wananchi
wawachague ili kama akiingia madarakani wasaidie kuleta maendeleo.
AMANI
Katika hatua nyingine Dk. Magufuli amepuuza hoja za baadhi ya watu
wanaodai ametoa kauli za vitisho kwa wananchi kwa kuhusisha uchaguzi na
vurugu za nchi ya Libya.
Akiwa katika Wilaya za Butiama, Bunda na Serengeti, kwa nyakati
tofauti, Dk. Magufuli, alisema kamwe hataacha kuzungumzia amani japo
kuna watu wanachukizwa na kauli yake.
Alisema ataendelea kuhubiri amani ya nchi, kwani asipofanya hivyo ni bora asichaguliwe kuwa rais wa awamu ya tano.
“Nimeanzia Butiama kutokana na historia ya amani ya nchi hii. Najua
wapo watu eti wanasema nisihubiri amani ya nchi…nasema nitaendelea
kuisemea wakati wote.
“Iwe usiku, mchana na hata wakati wote nitazungumzia amani, nisipohubiri amani basi sisitahili kuwa rais.
“…leo Mama Maria Nyerere yupo nchini Namibia anapokea tuzo ya amani
kwa sababu ya amani ya nchi yetu kutokana na misingi imara iliyowekwa na
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Kituo cha Haki za Binadamu na
Msaada wa Kisheria (LHRC) pamoja na wasomi mbalimbali, kumtaka mgombea
huyo kuacha kutumia mifano ya nchi za Libya na Misri katika kampeni
zake.
Itakumbukwa katika nchi hizo, machafuko yalisababisha Kiongozi wa
Libya, Kanali Muamar Gaddafi kung’olewa madarakani, huku nguvu ya umma
nayo ikimuondoa madarakani Rais wa Misri, Hosni Mubarak.
Dk. Magufuli alisema amedhamiria kuwatumikia Watanzania kwa vitendo
na atahakikisha anaunda baraza la mawaziri dogo, lakini lenye uadilifu.
JAJI WARIOBA
Naye Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, jana aliibuka kwenye
kampeni za Dk. Magufuli na kuwashangaza watu wanaobeza maendeleo
yaliyopatikana katika miaka 54 ya uhuru.
Jaji Warioba, alitoa kauli hiyo kwenye uwanja wa Mwenge kijijini Butiama alipopewa nafasi ya kusalimia.
Alisema umefika wakati watu wanaomtumia kama dira Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika kampeni zao wajitafakari zaidi.
Bila kutaja jina la mtu, Jaji Warioba alisema wakati wa mchakato wa
urais ndani ya CCM kila mgombea alikwenda katika kaburi la Mwalimu
Nyerere aliyezikwa eneo la Mwitongo na kuanza mikakati yake.
“Wengine katika kampeni zao wanatumia maneno ya Mwalimu kama
wamechanganyikiwa. Huwezi kumtumia Mwalimu Nyerere kama dira halafu
unasema CCM haijafanya kitu, aliijenga Tanzania kwenye misingi na wote
waliomfuata wanapita kwenye misingi yake,” alisema Jaji Warioba.
Alisema hatua ya nchi kupoteza maadili ilitokana na uamuzi wa baadhi ya viongozi kuwa na uhusiano na matajiri.
Created by Gazeti la Mwananchi
Friday, 11 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment