AZIZA MASOUD NA BASIL MSONGO (TUDARCO).
MAHUJAJI watano kutoka Tanzania wamekufa juzi wakati wakishiriki ibada ya hija inayofanyika Makka, nchini Saudi Arabia.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana ilisema kwa mujibu
wa taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini humo, mahujaji hao ni
miongoni mwa wengine 717 kutoka mataifa mbalimbali waliofariki dunia,
huku zaidi ya 800 wamejeruhiwa kutokana na msongamano mkubwa wa watu
katika eneo la Mina.
Taarifa hiyo iliyotumwa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa
Umma cha wizara hiyo iliwataja Watanzania waliokufa na kutambuliwa kuwa
ni Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla.
“Mtu mwingine aliyefariki ni raia wa Kenya anayeishi nchini ambaye
ametambulika kwa jina la Fatuma Mohammed Jama. Ubalozi unaendelea na
jitihada za kupata jina la Mtanzania mwingine aliyefariki katika tukio
hilo,” ilisema taarifa hiyo.
Pia ilisema Serikali inawaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi
hiki kigumu wakati inaendelea kufuatilia taarifa za tukio hilo.
“Pia ubalozi wetu kwa kushirikiana na taasisi zinazoshughulikia
masuala ya hija za Tanzania, ikiwemo Bakwata na mamlaka za Serikali ya
Saudi Arabia unaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua endapo kuna vifo
na majeruhi wengine kutoka Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.
Awali, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lilitoa taarifa iliyofanana na ile ya wizara.
Taarifa ya Bakwata iliyotolewa na Mufti wa Tanzania ambaye naye yuko
Makka, Sheikh Abubakari Zuberi, ilisema wamethibitisha kutokea kwa vifo
hivyo.
Mbali na vifo hivyo, pia alisema kuna taarifa ya mahujaji wanawake wawili ambao hadi juzi usiku hawakupatikana.
Kiongozi huyo alisema hawakuwa na uhakika kuhusu usalama wa mahujaji hao hadi watakapowaona au kupata taarifa zao.
Alisema majina hayo yamepatikana kupitia vitambulisho vilivyochukiliwa katika miili ya marehemu.
Alisema alipokea taarifa za kujeruhiwa mahujaji Watanzania na alionana na baadhi yao waliporuhusiwa kutoka hospitalini.
Sheikh Zuberi alisema ameagiza maofisa wa Bakwata waliopo mjini humo
kuendelea kufuatilia habari na taarifa za mahujaji wa Tanzania katika
hospitali na sehemu za kuhifadhia maiti.
“Nimefanya hivyo ili niweze kuwa na uhakika juu ya usalama wa
mahujaji wetu, katika kipindi hiki cha taharuki kubwa. Tunafanya
mawasiliano na wizara husika hapa Saudi Arabia kwa kushirikiana na
serikali yetu kupitia ubalozi wetu hapa Saudi Arabia,” alisema Sheikh
Zuberi.
Alisema anatambua uwepo wa mkanganyiko wa taarifa zinazozidisha
taharuki kwa ndugu na jamaa wa mahujaji nchini Tanzania, hivyo amewaomba
ndugu na jamaa wa mahujaji kuwa watulivu katika wakati huu mgumu.
Sheikh Zuberi alisema Bakwata inaendelea kufuatilia kwa karibu na wakipata taarifa za uhakika watawafahamisha wananchi.
Alisema kutokana na idadi ya maiti kuwa kubwa, Serikali ya Saudi
Arabia inaendelea na utaratibu wa kutambua uraia wa kila mwili ili
waweze kutoa taarifa.
Wakati huohuo, Serikali ya Saudi Arabia imesema kama mahujaji
wangefuata maelekezo ya mamlaka za nchini humo ajali iliyosababisha vifo
hivyo ingezuilika.
Eneo la Mina lipo takribani maili tatu kutoka Makka na ajali hiyo
ilitokea wakati wa tukio la mahujaji kumpiga mawe shetani, ikiwa ni
sehemu ya hija inayotarajiwa kumalizika kesho.
Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Khaled al-Falih, amesema uchunguzi
kuhusu tukio hilo utafanywa na matokeo yatatolewa haraka kama ilivyokuwa
katika matukio mengine.
Taarifa ya kiongozi huyo ilisema majeruhi walipelekwa katika
hospitali zilizopo Makka na ikionekana ni muhimu watatibiwa katika
maeneo mengine nchini humo.
Mahujaji na makundi ya Kiislamu wamezituhumu mamlaka za Saudi Arabia kuwa zinahusika na kuwepo kwa makosa ya kiusalama.
Hujaji aliyejitambulisha kwa jina la Ahmed Abu Bakr (45), alidai
polisi walifunga maeneo yote ya kuingilia na kutokea katika kambi za
hija na kuacha moja tu hivyo kusababisha msongamano.
Kwa mujibu wa raia huyo wa Misri, polisi wa eneo hilo wanaonekana hawana uzoefu na hawafahamu hata barabara za eneo hilo.
Pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imesema polisi 100,000 wamepelekwa kwa ajili ya ulinzi na usalama wakati wa hija.
Inadaiwa kuwa polisi hao hawakupata mafunzo ya kutosha na hawazijui
lugha ili kuwasiliana na mahujaji kutoka nje ya Saudi Arabia, ambao ndio
wengi.
Mwanzilishi mwenza wa Taasisi ya Utafiti ya Urithi wa Uislamu yenye
makao yake Makka, Irfan al-Alawi, alidai kuwa polisi hawafahamu namna ya
kuwasiliana na mahujaji na hakuna taratibu za kukabili misongamano.
Hujaji raia wa Misri, Mohammed Hasan (39), anasema anahofu kuwa ajali
kama hiyo iliyojeruhi zaidi ya watu 800 inaweza kutokea tena. “Unakuta
askari wamekusanyika eneo moja hawafanyi chochote,” alisema Hasan.
Katika hatua nyingine, Iran imesema watu 131 kati ya waliokufa ni
raia wake. India imetangaza kuwa raia wake 14 wamepoteza maisha katika
ajali hiyo kubwa kabisa wakati wa hija ndani ya kipindi cha zaidi ya
miaka 20.
Hija ni moja ya nguzo tano za Uislamu na kila muumini wa dini hiyo
mwenye uwezo anatakiwa kwenda kuhiji angalau mara moja wakati wa uhai
wake.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Alhamisi, mahujaji 1,952,817
wamefanya ibada ya hija mwaka huu, wakiwemo milioni 1.4 kutoka nje ya
Saudi Arabia.
Created by Gazeti la Mtanzania
Saturday, 26 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment