MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye
pia anaungwa mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, Edward Lowassa
amesema endapo atachaguliwa kuwa rais ataunda serikali isiyokuwa
‘nyoronyoro’.
Akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam katika
viwanja vya Shule ya Msingi Bunju ‘A’, Lowassa alisema muda umefika kwa
wananchi wa Tanzania kufanya mabadiliko.
“Naombeni mniteue niwe rais wenu ili mpate maendeleo ambayo hamkuwahi
kuyapata kwa kipindi cha miaka zaidi ya hamsini. “Mimi nitaunda
serikali isiyokuwa nyoronyoro na inayofanya kazi zake kwa ufanisi na
kila mtanzania ataweza kunufaika na rasilimali za nchi yake,” alisema
Lowassa aliyehutubia kwa takribani dakika kumi.
Alisema endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, serikali yake
itafanya kazi kwa spidi ya mwendo kasi wa 120 na hivyo lazima kutakuwa
na maendeleo makubwa kwa muda mfupi.
“Nitaondoa changamoto zote zinazowakabili wananchi wa Tanzania,
ikiwemo ukosefu wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo mengi
hapa nchini, nitatatua changamoto ya mazingira ya kufanyia biashara
ndogondogo pamoja na kutoa elimu bure,” alisema Lowassa.
Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa wasiwe na hofu kuwa kura zao
zitaibwa, akisema, “Hakuna atakayeiba kura ng’o. Nimesikia kuwa kuna
njama za kuiba kura, hakuna jambo kama hilo, bali kila mtu akipiga kura
ahakikishe analinda kura hadi mwisho ili kutoruhusu mwanya wa kuiba na
hakuna atakayeiba kura ng’o.”
Awali, akimkaribisha Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman
Mbowe alisema wamezunguka katika baadhi ya maeneo ya nchi na kuona
watanzania wamechoka na ugumu wa maisha na hivi sasa wanataka
mabadiliko.
“Watanzania wanahitaji mabadiliko, tumepata mapokezi makubwa sana
kila tulipopita kuomba ridhaa ya wananchi, hii inaonesha ni jinsi gani
wananchi hawa wapo tayari kukombolewa,” alisema Mbowe.
Mbowe aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na
kuchagua Chadema ili kiwakomboe na kutatua changamoto zinazolikabili
taifa. Baada ya kutoka Kawe katika Manispaa ya Kinondoni, jioni Lowassa
alikwenda katika jimbo lingine la manispaa hiyo, Kibamba, kuendelea na
mkutano wa kampeni.
Created by Gazeti la Habari Leo
Tuesday, 8 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment