Mbunge wa Iringa Mjini anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa.
WATU 62, akiwemo Mbunge wa Iringa Mjini aliyemaliza muda wake,
Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za
kuhusika kufanya fujo na kufunga barabara mjini hapa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi alitoa taarifa
hiyo jana mkoani hapa kwa waandishi wa habari na kusema waliokamatwa,
wanasadikiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Akieleza sababu za kumkamata Msigwa ambaye ni mgombea wa Jimbo la
Iringa Mjini, Kamanda alisema yeye hakuwepo eneo la tukio, isipokuwa
anatuhumiwa kutoa hamasa kosa lifanyike. “Katika kutenda makosa,
hakuwapo pale katika eneo, lakini wakosaji wakuu wako katika makundi
manne.
Kuna anayetenda makosa kwa mkono wake, kuna yule anayewezesha, kuna
anayesaidia, hata mshauri au kutoa hamasa kwa watu kutenda makosa. Yeye
ndiye huyo wa la nne,” alisema.
Akielezea tukio, Kamanda alisema juzi saa 12 jioni wafuasi hao
walikuwa kwenye barabara inayotoka Iringa mjini kwenda eneo la Kihesa,
wakiwa wamezuia barabara na kucheza katikati ya barabara.
Alisema akiwa katika mkutano wa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Dk John Magufuli, zilipatikana taarifa kwamba waendesha bodaboda
zaidi ya 150, walikuwa wamekusanyika katika hoteli ya Sambala.
“Tukafuatilia kuona kwa nini wamejikusanya; tukafuatilia tukaona wako
kwenye kikao chao cha ndani. Hatuna usumbufu na watu wanaofanya vikao
vyao vya ndani kwani ni haki yao,” alisema Kamanda Mungi. Hata hivyo,
alisema mkutano wao ulipoisha, wale watu walitoka na kuingia barabarani
na kuanza kucheza wakizuia watu na magari kupita.
Alisema alimwagiza mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU)
akawaondoe watu hao barabarani. Kwa mujibu wa kamanda, Mkuu wa FFU
alipotaka kuwaondoa kwa amani, walikaidi na alipojaribu kutumia nguvu,
walianza kumrushia mawe na kukimbilia kwenye hoteli waliyokuwa
wakifanyia mkutano.
Alisema FFU waliingia kwenye hoteli hiyo na kukamata baadhi; tukio
ambalo lilisababisha wengine kuumia kutokana na kuruka ukuta na wengine
kuanguka. Akitoa taarifa hizo jana mchana, Kamanda alisema walitarajia
kufikisha watuhumiwa hao mahakamani wakati wowote.
Kamanda alionya vyama vya siasa na viongozi wake kuepuka vitendo
vinavyoashiria kuhatarisha usalama. Alisema katika kipindi hiki cha nusu
ya kampeni kuelekea siku ya uchaguzi, upo mhemko mkubwa wa kisiasa
ikilinganishwa na siku za mwanzoni.
“Sasa hivi tuko karibu nusu ya muda wa kampeni. Kipindi cha awali,
kimekwenda vizuri. Kwa mfano katika Mkoa wa Iringa, Kuanzia tarehe
ishirini na mbili hadi tarehe thelathini mwezi wa nane hakuna kosa hata
moja lililotendeka pale kuhusiana na kampeni,” alisema kamanda.
Alisema Septemba mosi hadi Septemba 5, yaliripotiwa makosa sita.
Septemba 5 hadi 19, kulikuwa na makosa 17 ambayo kati ya hayo, ambayo
kati yake, 15 yalitokea Iringa mjini na yaliyobaki ni ya Kilolo. Alisema
kadri inavyoelekea katika uchaguzi, watu wanapata mihemko na kusahau
kanuni ya maadili ya uchaguzi.
Aliwaomba viongozi wa siasa kuzingatia maadili, wawaelekeze na
kuwaelimisha wafuasi wao wayafuate. “Tusipofanya hivyo, amani
itavurugika. Sisi polisi Iringa hatutakuwa na huruma na chama chochote,
mtu yeyote ambaye anaonesha dalili zozote za kuvuruga amani katika mkoa
wetu wa Iringa,” alisema.
Alisisitiza, “sisi amani ni kipaumbele cha kwanza, mengine yote
yatafuata. Yeyote anayetishia amani Iringa, anatishia kazi ya polisi,
hatutamvumilia.” CCM yasikitishwa Naye Emmanuel Ghula, anaripoti kuwa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeelezea kusikitishwa na kitendo cha wafuasi
wa vyama vinavyounda Ukawa kupiga mawe, kurusha chupa na kuharibu ofisi
za chama hicho mkoani Tanga juzi wakati wa kampeni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni
ya CCM, January Makamba, wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni
Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, walisababisha uharibifu mkubwa katika
ofisi za chama hicho mkoani Tanga wakati wa kampeni.
“Tunasikitika sana kwa wenzetu kukosa ustaarabu katika kampeni zao
kwani mikutano yote ya CCM imekuwa ikifanyika katika hali ya amani,
utulivu na ustaraabu,” alisema. Makamba alisema kampeni zimekuwa
zikienda vizuri, lakini vijana wa vyama vinavyounda Ukawa wamekuwa
wakisababisha uvunjifu wa amani katika mikutano ya CCM, lakini CCM wao
wamekuwa wakiendesha kampeni zao kistaraabu.
Alisema ni lazima watanzania waelewe kuwa uchaguzi utapita na taifa
litabaki, hivyo ni vyema wananchi wote hasa viongozi wa vyama vya siasa
kuendesha kampeni zao kistaarabu pasipo kusababisha vurugu.
Creted by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 29 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment