Tuesday, 8 September 2015

Tagged Under:

Kampeni za Magufuli zaua wawili

By: Unknown On: 08:15
  • Share The Gag


  • *Ni baada ya kukanyagwa wakiwa uwanjani
    *Rais Kikwete awalilia,atuma salamu za pole

    Ramadhan Libenanga Moro na Bakari Kimwanga, Handeni
    MKUTANO wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli juzi uliingia dosari, baada ya watu wawili kufariki dunia na wengine 17 kujeruhiwa.
    Tukio hilo la aina yake, lilitokea juzi jioni mkoani Morogoro wakati Dk. Magufuli alipohutubia maelfu ya wananchi wa mkoa huo katika Uwanja wa Jamhuri.
    Vifo hivyo ni kutokana na msongamano wa watu kuwa mkubwa wakati wakitoka uwanjani, hali iliyosababisha baadhi yao kupoteza maisha kwa kukosa hewa na wengine kujeruhiwa baada ya kuanguka na kukanyagwa.
    Idadi kubwa ya majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali  ya Mkoa wa Morogoro wakiendelea kupata matibabu.
    Akizungumza na waandishi wa habari mbele ya Rais  Jakaya Kikwete aliyetembelea majeruhi hao kuwapa pole jana, Mganga Mkuu  wa Hospitali  ya Mkoa, Ritha Lyamuya alithibitisha  kupokea majeruhi hao.
    Dk. Lyamuya alimwambia Rais Kikwete kuwa waliopoteza maisha katika tukio hilo, ni mwanafunzi wa darasa la tano, Ramadhan Abdalah (12), anayesoma Shule ya Msingi Mkundi na Grace George (39) mkazi wa  Kata  ya Kilakala.
    “Mheshimiwa Rais, katika tukio hili watu wawili wamepoteza maisha na wengine 17 wamejeruhiwa.
    “Hii imetokana na msongamano wa watu kuwa mkubwa wakati wanatoka uwanjani… mlango  wa kutokea ulikuwa mmoja tu.
    “Baadhi ya watu waliishiwa nguvu na kuanguka chini na kujikuta wakikanyagwa na wenzao katika harakati za kutoka uwanjani,”alisema.
    Dk. Lyamuya, aliwataja majeruhi waliolazwa kuwa  ni Mariana Mkunda, Nasra Abdalha, Christopher Luice, Frola Maduka, Jalia Mohamed na Prodencia  Chuma.
    Wengine ni Zahela Shanite, Fatuma Omar, Sania said, Sifa Mohemed, Ally Juma, Kokoliko Ramadhan  na  Awadhi Kenedy.
    Hata  hivyo,  Dk. Lyamuya alisema kati  ya hao,  majeruhi  saba   wameruhusiwa  na  wengine bado wanaendelea na matibabu.
    Alisema majeruhi mmoja ambaye hakumtaja jina, hali yake ni mbaya.
    Katika  hatua  nyingine, Rais Kikwete  alituma  salamu  za rambirambi  kwa ndugu, jamaa na marafiki wa walipoteza ndugu zao.
    Alisema amesikitishwa na   vifo hivyo na kusisitiza kuwa watu waliopoteza maisha walikwenda katika mkutano kwa mapenzi  ya  chama  chao.
    “Nimesikitishwa na vifo hivi, marehemu walikwenda kwenye mkutano ule kwa amani  na upendo mkubwa wa chama chao…Mungu aziweke roho zao mahali pema,”alisema Rais Kikwete.
    “Hali  hiyo  imetokana na  wingi wa  watu  katika  uwanja  kwa kufungua  mlango  mmoja kutokana na tukio hilo tunapaswa  kujifunza  wakati mwingine kutumia milango  yote minne ya  uwanja wetu  ili kunusuru madhara  kama  haya,” alisema  Rais Kikwete.
    Watu mbalimbali waliozungumza na MTANZANIA, walisema walisema wahusika wa uwanja huo pamoja na Jeshi la Polisi wanapaswa kubeba lawama kutokana na uzembe.
    “Hakukuwapo na utaratibu wowote wa polisi kulinda usalama wa raia ndani ya uwanja kwa kusimamia utaratibu wa kutoka, badala yake askari wote walikuwa wakitizama na kusimamia zaidi ulinzi wa viongozi wa kitaifa pale uwanjani,”alisema mwananchi mmoja na kuongeza. “baada ya polisi kugundua watu wameanza kuzimia na kupoteza fahamu,walianza kuzunguka huko na kule na kuanza kuokoa waliokuwa wamezidiwa kwa kukanyagwa na wengine ambao walikuwa wamezirai.
    “Baada ya mkutano kumalizika, watu walianza kukimbilia kutoka nje kupitia geti namba moja ambalo ndiyo geti kuu la upande wa mashariki mwa uwanja huo,” alisema mwananchi mmoja.

    MVOMERO
    Katika hatua nyingine, Dk. John Magufuli jana alikumbana na mtihani wa kwanza wa wananchi baada ya kupokewa na mabango yenye ujumbe mbalimbali.

    Miongoni mwa mabango hayo ni lile lililokuwa limeandikwa. Waziri Mkuu mstaafu Federick Sumaye arudishe shamba analomiliki kwani limegeuka pori,”.
    Hali hiyo, ilitokea wakati msafara wa Dk. Magufili ukielekea  wilayani Mvomero.
    Alipofika Kona ya Wami, alijikuta akipokewa na mabango mengine ambapo alilazimika kusimama kwa muda.
    Baada ya kusimama, Dk. Magufuli alishuka kwenye gari lake na kumwita mgombea ubunge wa Jimbo la Mvomero, Sadik Murad asome kwa sauti mabango hayo mbele ya wananchi hao.
    Murad, alisoma bango hilo lililokuwa limeandikwa ‘Magufuli chukua shamba la Sumaye’.
    Kutokana na maneno hayo, Dk. Magufuli aliwajibu wananchi hao kwa kifupi na kusema amesikia kilio chao na kuahidi kukifanyia kazi.
    “Nimesikia ombi lenu wananchi nitalishughulikia,” alisema kwa kifupi Dk. Magufuli.
    Akihutubia wananchi wa Wilaya za Mvomero, Kilindi na Handeni kwa nyakati tofauti jana, Dk. Magufuli alisema ameziona changamoto zinazokabili wilaya hizo, ikiwamo adha ya barabara na migogoro ya ardhi inayosababisha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
    “Nipo hapa Kilindi, napenda kuwaahidi lazima tujenge barabara ya kutoka Handeni, Kilindi kupitia Mvomero , Ifakara, Malinyi hadi Wilaya ya Namtumbo.
    “Najua kuna watu wamekuwa wakichochea migogoro ya ardhi, ikiwamo mpaka kati ya Kilindi na Kiteto. Kuna viongozi wanahongwa ng’ombe sasa jueni sasa ni mwisho wenu.
    “Ukiacha hao kuna baadhi ya watu hapa Tanga, wamechukua mahekta ya ardhi na kwenda kukopa mikopo benki na leo hii wamekua mabilionea, huku wananchi wakibaki maskini,” alisema.

    Created by Gazeti la Mwananchi


    0 comments:

    Post a Comment