*Asema hawezi kuwa rais bila kupigiwa kura
*Aanza kurusha makombora Ukawa
Na Bakari Kimwanga, Kahama
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John
Magufuli, amewataka Watanzania kutodekezwa na matokeo ya utafiti
unaoendelea kutolewa na taasisi mbalimbali.
Kauli hiyo aliitoa jana kwa nyakati tofauti, alipohutubia mikutano ya
kampeni iliyofanyika katika majimbo ya Busanda, Mbogwe ya mkoani Geita
na majimbo ya Ushetu na Kahama Mjini ya mkoani Shinyanga.
Alisema katu utafiti huo hauwezi kumfanya awe rais na hivyo ni lazima
wana CCM na Watanzania kwa ujumla wampigie kura nyingi za ndiyo ili
ashinde kwa asilimia 95.
Pia aliwataka wanachama wa CCM kutobweteka kwa kuwahamasisha watu kwenda kupiga kura.
“CCM na Watanzania tusidekezwe na utafiti, nataka kushinda kwa
asilimia 95, nendeni mkapige kura, maana sasa watakuja watu na kuwaambia
tumeshinda kwa utafiti.
“Hapana, siwezi kushinda kwa maneno, Oktoba 25 nendeni asubuhi na
mkapige kura kwa wingi kwa kuweka alama ya vema katika picha ya Magufuli
na pigeni kura kwa amani na utulivu, kwangu ni kazi tu,” alisema Dk.
Magufuli.
Msimamo huo alioutoa umekuja siku chache baada ya Taasisi ya Twaweza
kutoa matokeo ya utafiti na kueleza kuwa mgombea huyo wa urais anaweza
kushinda kwa asilimia 65, akifuatiwa na mgombea urais wa Chadema chini
ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa,
angepata asilimia 25.
Taasisi nyingine ya Utafiti ya Ipsos ilitoa matokeo yake juzi na
kusema Dk. Magufuli angeshinda urais kwa asilimia 62 (kama uchaguzi
ungefanyika juzi), huku Lowassa angepata asilimia 31.
ILANI NA KERO YA MAJI
Akizungumza na wananchi wa Nyarugusu, Dk. Magufuli, alisema anajua
changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.
Kutokana na hali hiyo, amejipanga kutatua kero hiyo kwa kuwa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM imeeleza kwa maeneo ya vijijini maji yatapelekwa kwa
asilimia 75 na mijini asilimia 95.
Alisema haiwezekani maeneo yanayozalisha madini ambayo pia huchangia pato la Taifa kukosa maji ya uhakika.
“Ilani ya uchaguzi ya CCM imeeleza vizuri sana na mipango yetu
kuanzia mwaka kesho tutasambaza maji kwa asilimia 75 vijijini na mijini
asilimia 95. Lakini pia ninajua hapa kuna wachimbaji wadogo ambao
wanahitaji maeneo ya kuchimba dhahabu yao.
“Sawa tutalinda maslahi ya wachimbaji, lakini si wakubwa peke yao,
hata wadogo pia tutawapa maeneo yao ili nao wafaidi rasilimali za nchi
yao kama CCM inavyotaka,” alisema Magufuli.
Alitaka Watanzania waendelee kumwamini kwa kuwa amejipanga kutatua kero zao kwa vitendo.
Alisema hawezi kutoa ahadi za uongo kwa Watanzania ambazo
hazitekelezeki, ikiwemo ya kuondoa nyumba za tembe ila atakachokifanya
ni kuhakikisha Serikali yake inapunguza bei ya vifaa vya ujenzi ili
wananchi wajenge nyumba nzuri na za kisasa.
Alisema anatambua Watanzania wanahitaji mabadiliko ya kweli katika nchi yao na yatapatikana chini ya Serikali yake.
KOMBORA UKAWA
Mgombea huyo wa urais alisema anashangazwa na baadhi ya wanasiasa
aliowataja majina kwa mara ya kwanza, hasa Lowassa na Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye, wanaodai CCM haijafanya kitu.
Alisema viongozi hao pamoja na kuwahi kuwa katika nafasi za juu
serikalini, lakini wameshindwa kutambua hata baadhi ya huduma
walizosimamia wenyewe.
“CCM si malaika, ila kuna watu ambao si wazuri na wengine wameondoka,
je, Lowassa, Sumaye, Mgeja (Khamis) wote walikuwa CCM, sasa leo
wanasema hakuna kilichofanyika, kama wameshindwa wakiwa katika nafasi ya
uwaziri mkuu, je wakipewa nchi?
“Ninaomba mniamini mimi ndiye Magufuli, nimejipanga kutatua kero za
Watanzania wote bila kujali itikadi zao za vyama, wanasema Serikali ya
CCM imechoka, ila ni wao ndiyo wameifanya ichoke kwa kuifikisha hapa
ilipo.
“Wao walikuwa na madaraka makubwa kwa kuwa unapokuwa waziri mkuu
ndiyo mshauri mkuu wa rais, mimi sijawahi kuwa na madaraka makubwa, sasa
nataka kuwatumikia Watanzania,” alisema Dk. Magufuli.
SITTA AMSIKITIKIA LEMBELI
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni za CCM Taifa, Samuel
Sitta, amesikitikia kitendo cha rafiki yake, James Lembeli kukimbia CCM
na kujiunga na Chadema.
Alisema Lembeli alikuwa ni mmoja wa wabunge waliojipambanua kupinga
maovu, ikiwemo ufisadi, lakini naye ameshindwa kuhimili vishindo na
kuamua kuondoka.
“Hapa Kahama kuna ndugu yetu James Lembeli ambaye alikuwa ni mmoja wa
watu waliokuwa wanapinga maovu, leo naye ameungana na wale wenzie kule.
“Si ajabu kama amekwenda huko naye lakini nauliza yale aliyokuwa
anayasimamia ataweza? Pia ninawaomba sana majimbo yote ya Mkoa wa
Shinyanga tunataka yawe chini ya mikono ya CCM na ninawaomba mniunge
mkono,” alisema.
Sitta, aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la tisa na kwa sasa ni Waziri wa
Uchukuzi, aliwataka wananchi wa Kahama kujitokeza kwa wingi siku ya
uchaguzi na kumpigia kura Dk. Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la
Kahama Mjini, Jumanne Kishimba.
Awali, kabla ya Dk. Magufuli hajaanza kuhutubia, mkuu wa msafara za
mgombea urais, Abdallah Bulembo, aliwataka wananchi waliofurika katika
uwanja wa mkutano kumkumbuka aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Utumishi wa Umma), Celina Kombani, aliyefariki dunia juzi nchini India
Baada ya dua hiyo, Bulembo alisema anashangazwa na kitendo cha
Lembeli badala ya kugombea ubunge kwao Ushetu ametafuta kivuli cha
kujifichia Kahama Mjini.
“Leo (jana) tumetoka Ushetu ambapo ni kwao, kule wamesema pamoja na
kuwa kwake, lakini asingepata kura, sasa nanyi hapa Kahama Mjini
mnyimeni kura.
“Alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili amewafukuzisha
kazi watu na hata kuonekana ni mtu mwenye heshima na ninapata tabu na
watu wenye nywele nyeupe kama Lembeli,” alisema Bulembo.
Created by Gazeti la Mtanzania
Saturday, 26 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment