Raisi Jakaya Kikwete akiwasilisha hotuba kuhusu Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa
Mwanamke katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,
jijini New York, Marekani jana.
TANZANIA imeahidi kuchukua hatua tano muhimu za kutetea na kuendeleza
haki za wanawake kati ya sasa na mwaka 2030, ikiwa ni pamoja na kufanya
mabadiliko makubwa ya kufuta sheria zinazokandamiza wanawake.
Badala yake itatunga sheria za kuleta usawa wa kijinsia, yote katika
utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) mapya kwa manufaa ya
wanawake wa Tanzania. Miongoni mwa hatua hizo itakuwa ni pamoja na
kufuta ama kufanya mabadiliko ambayo yanaendeleza vitendo vya
kiutamaduni ambavyo vinaendeleza ubaguzi wa wanawake kama vile Sheria ya
Ndoa ya Mwaka 1971, Sheria ya Urithi na kutunga Sheria ya kukomesha
ukatili dhidi ya wanawake.
Msimamo huo wa Tanzania umeelezwa mwishoni mwa wiki na Rais Jakaya
Kikwete alipozungumza katika Mkutano wa Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa
Akinamama: Dhamira ya Kuchukua Hatua uliohudhuriwa na wakuu wa nchi
mbalimbali duniani kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New
York, Marekani.
Rais Kikwete ameuambia mkutano huo ulioitishwa kwa pamoja na China,
Denmark, Mexico na Kenya kuwa hatua ya pili ambayo Tanzania inakusudia
kuchukua ni kuridhia makubaliano yote ya kimataifa kuhusu haki za
akinamama hasa Makubaliano ya Kimataifa Juu ya Kukomesha Aina Zote za
Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW).
Hatua nyingine ambazo Rais Kikwete amesema Tanzania itachukua katika
miaka 15 ijayo ili kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na kuendeleza na
kuunga mkono upatikanaji wa rasilimali fedha.
Rasilimali hizo zinazolenga kuongeza usawa wa kijinsia kwa mujibu wa
Ajenda ya Kugharimia Maendeleo ya Addis Ababa, ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha zinatolewa pesa za kutekeleza mipango ya kitaifa na ya
Serikali za Mitaa za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake.
Itahakikisha pia utekelezaji wa uwakilishi wa uongozi wa asilimia 50
kwa 50 kati ya wanawake na wanaume katika nafasi zote za maamuzi kwenye
ngazi zote.
Created by Gazeti la HabariLeo
Tuesday, 29 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment