Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jji Mstaafu, Damian Lubuva akizungumza na wanahabari juu ya mambo yahusuyo tume hiyo
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitoa wasiwasi vyama vya siasa
kuwa hakutakuwepo na wizi na udanganyifu wa kura katika matokeo ya
uchagauzi wa rais, wabunge na madiwani, utakaofanyika nchini kote Oktoba
25, mwaka huu.
Aidha, NEC imesema ipo tayari kushirikiana na wataalamu wa vyama
hivyo kubaini vyanzo vya wizi wa kura, iwapo tatizo hilo litajitokeza na
hivyo kuhakikisha haki inatendeka kwa vyama vyote vinavyoshiriki
uchaguzi huo.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji
mstaafu Damian Lubuva wakati wa mkutano wake na wawakilishi wa vyama vya
watu wenye ulemavu, aliokutana nao kupata ushauri na maoni ya taasisi
hizo kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Alisema hadi kufikia sasa, vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo
vimefanyika kampeni za kistaarabu. Lakini, alisema katika siku za hivi
karibuni, baadhi ya vyama vimekuwa vikitoa kauli na matamshi yaliyovuka
mipaka. Alisema NEC inavionya vyama hivyo kuacha mara moja tabia hiyo.
“Vipo baadhi ya vyama vya siasa na wagombea wao wamekuwa wakitumia
muda mwingi kutoa lugha zisizofaa baada ya kunadi sera ya vyama vyao,
vyama hivyo tumekutana navyo na kuwataka kuacha mara moja kampeni za
aina hiyo,” alisema Jaji Lubuva.
Jaji Lubuva alisema Julai 27 mwaka huu, vyama vyote vya siasa
vinavyoshiriki uchaguzi mkuu, vilisaini mkataba wa maadili ya uchaguzi
huo, hivyo ni wajibu wa vyama hivyo kuzingatia viapo walivyotoa katika
maktaba huo.
Akifafanua, Jaji Lubuva alisema iwapo chama chochote hakina hoja ya
kuzungumza na wananchi ni vyema kikawa kimya hadi siku ya uchaguzi
Oktoba 25 mwaka huu. Aidha, Jaji Lubuva alivitaka vyama vya siasa kuacha
tabia ya kuingilia masuala ya utawala ya tume hiyo, kwani kufanya hivyo
vyama hivyo vitakuwa vikifanya kazi za tume hiyo na hivyo kuingilia
masuala ya ndani ya kiutendaji ya taasisi hiyo.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi huo, Jaji Lubuva alisema mahitaji
yote ya msingi ya uchaguzi huo tayari yamepokewa na NEC, ikiwemo
karatasi, wino, na masanduku ya kura, ambapo baadhi yake yameanza
kusafirishwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akisisitiza juu ya kuamini utendaji wa tume, alisema haioni sababu ya
vyama hivyo kuwa na wasiwasi na tume na kutaka kubaki vituoni kwa madai
ya kulinda kura. Alisema matokeo ya uchaguzi mkuu, yatatangazwa kwa
mujibu wa sheria na taratibu na mapema iwezekanavyo, tofauti na siku
saba sheria inavyotaka, huku kukiwa na waangalizi 140 kutoka Umoja wa
Ulaya (EU) na wengine wa nje.
Waangalizi wa ndani watakuwa 75. Wapigakura wanatakiwa kurejea
nyumbani mara tu baada ya kupiga kura na hawatakiwi kuendelea kukaa
vituoni kwa madai kulinda kura. Aidha, alisema Tume imepokea taarifa ya
vifo vya wagombea watano wa nafasi za udiwani na vifo vya wagombea
wawili wa nafasi ya ubunge, ambapo uchaguzi katika maeneo hayo
umeahirisha hadi Novemba 22 mwaka huu.
Alisema katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu, NEC imefanya uteuzi
wa wagombea nane wa urais, wagombea 1,218 wa ubunge, kati yao wanaume
wakiwa 985 na wanawake 233. Kwa upande wa udiwani ni 10,879, kati yao
wanaume ni 10,191 na wanawake 679.
Akizungumzia walemavu wasioona, alisema watatumia kifaa maalumu cha
‘Tactile Ballot Folder’kupigakura, ambacho kitamwezesha mlemavu huyo
kupiga kura yake mwenyewe bila kusaidiwa na mtu mwingine, hivyo kutimiza
lengo la usiri wa kura kwa mpigakura.
Kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura, Jaji Lubuva alisema katika
kipindi cha siku 10 zijazo kuanzia sasa, Tume hiyo inatarajia kusambaza
daftari la kudumu katika mikoa yote nchini na wananchi watatakiwa
kuhakiki majina yao katika kipindi cha siku 8.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 29 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment