Mgombea Urais wa CC, Dk John Magufuli.
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli,
amejitabiria ushindi wa ‘tsunami’ wa asilimia 95 na siyo 65 kama
ilivyotajwa katika utafiti wa Taasisi ya Twaweza.
Mbali na ushindi huo, Dk Magufuli aliyezungumza jana mjini Kahama,
mkoani Shinyanga katika mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya watu, pia
alitabiri baadhi ya vyama vya upinzani kufa baada ya uchaguzi.
Akihutubia mkutano huo ambao alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na
baadhi ya watu waliokuwa wakiimba ‘rais rais rais’, Dk Magufuli alisema
anatarajia umati unaohudhuria mikutano yake ndiyo utakaompa ushindi.
“Wala sijashinda…wa kunifanya nishinde ni nyie,” alisema na
kushuhudia umati mkubwa wa watu aliokutana nao katika mikoa mbalimbali
aliyofanya kampeni. “Wala si asilimia 65 inayosemwa, bali utakuwa ni
ushindi wa tsunami… na baadhi ya vyama vitakufa,” alisema na kutaja kuwa
atashinda kwa asilimia 95.
Katika utafiti wa Twaweza uliotangazwa wiki hii, matokeo yalionesha
kuwa Dk Magufuli ataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 kwa
kupata asilimia 65 ya kura na kufuatiwa kwa mbali na mgombea wa Ukawa,
Edward Lowassa ambaye ametajwa kupata asilimia 35. Akizungumzia ufisadi,
Magufuli alisema, Serikali na hata chama tawala haviwezi kuwa na
malaika pekee, bali wapo pia mafisadi wachache wakiwemo walioamua kuhama
chama baada ya yeye kutangazwa kuwa mgombea urais.
Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika Kijiji cha Mwabomba, Jimbo la
Ushetu na pia kwenye mkutano mjini Kahama, Magufuli alisema wapo ambao
baada ya kupewa dhamana ya uongozi, wamekuwa wasaliti wa Serikali.
“Hatuwezi kusema Serikali inaongozwa na malaika …wapo wabaya wachache.
Hata kwenye CCM wapo. Ndio maana wengine walipoona nimeingia wakaanza
kukimbia… na dalili ya mafisadi huwa ni kukimbia,” alisema.
Alisema walikimbia kwa sababu wanafahamu msimamo wake huwa anachukia
mafisadi, anamtanguliza Mungu na yupo kwa ajili ya wanyonge. “Nipeni
kura za kutosha niende nikashughulike na mafisadi,” alisema na kuendelea
kusisitiza nia yake ya kuanzisha Mahakama ya Mafisadi. Alisema Tanzania
imetoka kwenye mikono mizuri ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere
na imelelewa katika misingi ya umoja na amani.
Alisisitiza Serikali ya CCM siyo mbaya, bali wapo wachache hata ndani
ya chama. Alisema ndiyo maana ameomba urais ili nchi iwe na neema.
Alimfagilia Samuel Sitta (Waziri wa Uchukuzi) kuwa amesimama imara,
hababaiki, hadanganyiki na kwamba hata alipogombea naye urais kwenye
ngazi ya chama, alitambua kuwa wanaogombea ni wengi na wanaoitwa ni
wachache. “Lakini wapo wenzetu wanapokosa nafasi…,yuko mmoja aligombea
na Kikwete.
Wakati anagombea miaka ile ya nyuma, akasema yeye achaguliwe kwa
sababu amefanya kazi nzuri katika Serikali ya Mkapa…,” alisema Magufuli.
Aliendelea kusema akimlenga Frederick Sumaye, “Na sasa akagombea
akasema yeye ndiye mwanzo wa mafanikio yote. Alipokosa akahama na sasa
anasikika kwenye majukwaa akisema Serikali haijafanya kitu chochote.”
“Wewe mtu ulikuwa humo humo CCM miaka kumi, ukagombea wakakuweka
pembeni…leo unasimama na kusema hakuna mafanikio.
Kwa nini ulibaki sasa, ulikuwa unafanya nini,” alihoji na
kushangiliwa na umati wa watu mjini hapa. Magufuli ambaye alikuwa
akishangiliwa mara kwa mara na umati wa watu, aliwakumbusha wana Kahama
mafanikio yaliyoletwa na Serikali ikiwamo kukua kwa mji na uwepo wa
huduma za umeme, mtandao wa barabara na mawasiliano ya simu. “Kwa nini
watu wanasahau mapema hivi?
Ni vyema mtu ukatambua yale mazuri yaliyofanywa…,” alisema na kutaja
mafanikio ya ujenzi wa mtandao wa barabara nchi nzima. Alisema Wilaya ya
Kahama haikuwa na shule za sekondari tofauti na sasa ambapo zipo kila
mahali. Alisema watu wa Kanda ya Ziwa, hususani Kagera na Mwanza,
ilikuwa ni kawaida kwenda Dar es Salaam wakipita Uganda na Kenya tofauti
na sasa wanavyochagua mabasi ya kupanda.
“Haya yote hawayaoni…bado mtu anasimama kwenye majukwaa bila aibu
anasema hakuna chochote kilichofanyika…shukurani ya punda huwa ni
mateke,” alisema na kuongeza kuwa hata amani si chochote kwa hao
wanaokosoa. Aliwataka wana Kahama kutambua mahali walikotoka, walipo na
wanapokwenda wasije watu wakawapeleka pasipo. Alisema baadhi yao
wanaotaka kuipeleka nchi wanakojua, hawana rekodi nzuri.
Alisisitiza kuwa katika uongozi wake atamtanguliza Mungu na
atawatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Wachimbaji wadogo Akiwa eneo la Nyarugusu wilayani Geita, Magufuli
aliahidi kufanyia kazi mgogoro uliopo kati ya wachimbaji wadogo wa eneo
la Nyarugusu na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuhusu eneo la
uchimbaji. Alisema wakati takribani maeneo 24 yamesharudishwa kwa
wachimbaji wadogo, pia atahakikisha Serikali yake inatoa maeneo zaidi
kwa wachimbaji wadogo.
Katika maeneo mengi ya Mkoa wa Geita na Shinyanga aliyotembelea jana,
Magufuli aliendelea kusisitiza kwamba wachimbaji watakapovumbua madini
eneo lolote, hawatanyang’anywa bali watapewa leseni za umiliki. Eneo
linaloleta mgogoro katika eneo la Nyarugusu, ni ambalo Stamico kwa
kushirikiana na mwekezaji kutoka Marekani wanadaiwa kushindwa
kuliendeleza tangu mwaka 1983 na sasa wachimbaji wadogo wanataka wapewe.
Wamvaa Lembeli Wakati huo huo aliyekuwa Mbunge wa Kahama kwa tiketi
ya CCM, James Lembeli ambaye alihamia Chadema, amerushiwa makombora na
makada mbalimbali waliozungumza kwenye mikutano ya kampeni wilayani
hapa. Mwenyekiti wa Wazazi, Bulembo alimtaja Lembeli na aliyekuwa
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mngeja kuwa ni watu
wanaomnyonya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Edward Lowassa.
Bulembo alisema, kwa mujibu wa wananchi wa Jimbo la Ushetu, wanasema
Lembeli amekimbia kwa sababu hakutimiza matakwa yao. Lembeli na Kishimba
(Jumannemgombea ubunge wa CCM) wapi na wapi?,” alihoji Bulembo. Kwa
upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga,
Samuel Sitta, alisema Lembeli akiwa ndani ya CCM, alikuwa
akijitambulisha kuwa ni mtu anayepambana na uovu lakini sasa yuko kundi
moja na kundi alilokuwa akilipinga.
“Nasimama kwa masikitiko sana. Kulikuwa na ndugu yetu katika chama
hiki anaitwa Lembeli; Alijitahidi sana kujitambulisha kama mtu
anayepambana na maovu. Leo hii mtu aliyesema anapambana na maovu, yuko
katika kundi moja na Mngeja, wanamsujudia mtu anayeitwa Lowassa; hii ni
aibu sana,” alisema. Sitta aliendelea kusema, “Lowassa kwa sisi
tunaomfahamu akiwa kijana, ni mtafutaji tu. Huyu haridhiki na utajiri
wowote.
Alipogombea katika hatua za awali kwenye CCM alidhani ataitisha kwa
kutumia fedha nyingi ili ateuliwe, lakini vigezo vya CCM si hivyo bali
ni vya Chadema, ambavyo mtu akiwa na fedha anakuwa mwanachama namba
moja. “ Alisema hao alioahidi mali wakae naye huko huko, CCM inachagua
rais atakayejali Watanzania wa kawaida wakiwemo mama lishe, wenye
bodaboda na wamachinga.
Sitta alisema mwezi mmoja tangu kampeni zianze, ahadi zilizomo kwenye
ilani ya uchaguzi zinavyofafanuliwa na mgombea, ni tofauti na jinsi
ilivyo kwa mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na umoja wao wa Ukawa.
Sitta alisema, kwenye udiwani, ubunge anataka kata na majimbo yote ya
Shinyanga yachukuliwe na CCM. Alibeza wanaotumia helikopta nchi nzima na
kusema hawawezi kuona matatizo ya wananchi.
“Leo hii mgombea wetu kasimama katika vijiji visivyopungua saba
ambavyo vilikuwa njiani (wilayani Kahama), kwa sababu anatembea katika
barabara,” alisema. Mgombea urais wa CCM, Magufuli hadi sasa, amefika
kwenye vijiji zaidi ya 4,512 nchini. Mgombea huyo na mgombea mwenza,
wamesafiri jumla ya kilometa 32,800 kuomba kura nchini.
Created by Gazeti la HabariLeo
Saturday, 26 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment