Thursday, 24 September 2015

Tagged Under:

Sumaye: Nimeanza kutishwa

By: Unknown On: 02:48
  • Share The Gag
  • *Lowassa atumia mahakama ya wananchi kuchagua mbunge
    Na Fredy Azzah, Masasi
    WAZIRI Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amesema ameanza kupata vitisho baada ya kuzungumza mambo mbalimbali ya Serikali katika kampeni za mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa.
    Akizungumza jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja vya Madeko, Jimbo la Ndanda wilayani Masasi mkoani Mtwara, Sumaye alisema vitisho hivyo ni pamoja na kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliyemtaka kunyamaza vinginevyo atamshughulikia.
    “Anasema Sumaye anyamaze vinginevyo tutamshughulikia, sijui atanishughulikia kwa lipi, lakini ole wake nikipata tatizo lolote.
    “Nataka wapande jukwaani watuambie dawa za kulevya zinazokamatwa kila siku magunia na magunia ni za nani na mpaka sasa amefanywa nini? Meno ya tembo yanayokamatwa huko ni ya nani na mpaka sasa hivi kafanywa nini?
    “Meli mbovu iliyopo Dar es Salaam ambayo sasa imeletwa Lindi ili kuwadanganya wananchi, nani kainunua na kafanywa nini, mabehewa mabovu nani kanunua na kachukuliwa hatua gani.
    “Siyo nikisema haya unasema utanishughulikia, utanishughulikia we nani? Kama hawana majibu ya haya, lazima waondoke, ndiyo utaratibu duniani kote, wanashangaa nini?
    “Kama hawataki kuondoka waseme kuwa wao ni madikteta tujue… Kama ni chama cha siasa kama vingine, Oktoba 25 wanaondoka asubuhi,” alisema Sumaye.
    Sumaye alisema hali ya kutishwa haipo kwake pekee, bali hata kwa wananchi ambao wanadanganywa wakichagua upinzani nchi itakuwa na vita.
    Alisema Libya, Misri ilipata machafuko, baada ya Serikali kukataa kusikiliza wananchi.

    LOWASSA
    Naye Lowassa akizungumza katika mkutano huo, alisema amechoka na umasikini ambao umekuwa ukiimbwa tangu mwaka 1962.
    Alisema kama atachaguliwa Oktoba 25, atataka wananchi wawe huru ndani ya nchi yao ili kama wakitaka kuuza mazao yao ya biashara wafanye hivyo sehemu yoyote.
    “Na nitaanza na eneo la elimu, kubadili mfumo wa elimu na masilahi ya elimu yawe bora na kilimo cha kisasa. Nilivyokuwa Bukoba nilisema kama kahawa Uganda ni bei nzuri, watu waruhusiwe kuuza huko.
    “Lazima raia wawe huru, kama ulikuwa uwasaidii wananchi wakati wanalima, kwanini uwaingilie wakati wa kuuza?” alisema Lowassa.
    Kuhusu suala la gesi asili, alisema Serikali ya Ukawa ikiingia madarakani, ahatahakikisha wanapitia upya mikataba ya gesi na mafuta ili kuona kama inanufaisha wananchi, hasa wale wa mikoa ya kusini na Watanzania kwa ujumla.

    NGUVU YA UMMA
    Katika hatua nyingine, Lowassa jana alilazimika kutumia mahakama ya wananchi kuchagua mgombea ubunge wa Jimbo la Masasi ambapo kulikuwa na msuguano kati ya mgombea wa Chadema na NLD.
    Katika jimbo hilo, Chadema imemsimamisha Cecil David Mwambe, huku NLD ikimsimamisha Angelous Gadriel Thomas.
    Kutokana na hali hiyo, wagombea wote hao walipewa nafasi ya kupanda jukwaani na kila mmoja kwa wakati wake kutakiwa aeleze changamoto za Jimbo la Ndanda na atakavyokabiliana nazo.
    Baada ya kunadi sera zao, Lowassa kabla ya kumaliza kuhutubia aliwaita wagombea hao na kisha kuhoji wananchi ni nani wanayemtaka, ambapo karibu uwanja mzima ukamchagua Mwambe.
    Lowassa alihoji wananchi hao mara mbili kisha kumuuliza mgombea na NLD kama anakubaliana na matokeo.
    “Sikubaliani nayo kwa sababu yalishapangwa,” alijibu.
    Baada ya kauli hiyo, Lowassa alisema kwa mamlaka aliyopewa, anamtangaza Mwambe wa Chadema kuwa mgombea wa jimbo hilo kwa kuwa amekubaliwa na wananchi walio wengi.
     Created by Gazeti la Mwananchi

    0 comments:

    Post a Comment