Mgombea Urais wa CC, Dk John Magufuli akihutubia wananchi wa Chato.
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli amewaaga
rasmi wananchi jimboni kwake Chato, mkoani Geita kwa kuwashukuru na
kueleza namna alivyofikia uamuzi wa kugombea nafasi hiyo ya juu, huku
akisema hata akiwa Rais wa Tanzania, kamwe hatabadilika.
Aidha, ameendelea kusisitiza kuwa, atakuwa Rais wa Watanzania, bila
kujali dini, kabila au vyama, hivyo maendeleo ya serikali yake
hayatabagua. Akizungumza jana mjini hapa kwenye mkutano wa kampeni
uliohudhuriwa na maelfu ya watu ambao alikiri kuwa ni mkubwa ambao
hajawahi kuuona, amewahakikishia kuwa ataiendesha nchi kwa ustaarabu na
si kwa udikteta kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidai.
“Hata baada ya kuchaguliwa, mimi sitabadilika, nitabaki kuwa mtoto
wenu yule yule John Magufuli,” alisema na kuongeza; “Nitaiendesha nchi
kwa ustaarabu, sitaiendesha nchi kwa udikteta…pamekuwa na watu
wanazungumza, kwa sababu nazungumza ukweli na ukweli utabaki ukweli
kweli. Watu wanabaki kutishiana. Nyie wana Chato waelezeni ukweli kwamba
nilipokuwa waziri nilikuwa nachunga ng’ombe, nilikuwa nakamua maziwa.
Mimi kazi ni kazi.” Magufuli aliwaambia wananchi hao waliompa ubunge
kwa miaka 20 mfululizo, kwa kuwaambia kwamba, wanaompiga vita ni
mafisadi wanaoogopa jeuri yake ya kusimamia kazi na utendaji.
Akizungumzia uamuzi wake wa kugombea urais, alisema alijipima kwenye
moyo wake kwa kumtanguliza Mungu. Alisema ameomba nafasi hiyo si kwa
majaribio bali anaamini na kujiamini kwamba atakapokuwa rais atasimamia
mambo mengi na kuifanya Tanzania mpya.
“Nafahamu tumetoka mbali, tumefika mbali na tunaelekea mbali.
Niliomba nafasi ya urais si kwa majaribio bali nataka niwatumikie
watanzania,” alisema na kusisitiza kwamba anafahamu kwa dhati bila
kubagua vyama, makabila, wanataka mabadiliko kwa maana wanataka
maendeleo na Tanzania mpya. Ashukuru mapokezi Dk Magufuli aliwashukuru
wananchi na kusema, mapokezi ya namna hii hayajawahi kutokea.
Huku akishangiliwa mara kwa mara, aliwashukuru wananchi hao kwa
kushirikiana naye kwa raha na shida akiwa mbunge wao kwa miaka 20.
Alisema katika kipindi cha miaka 10 mfululizo, wananchi walimpitisha
bila kupingwa. “Nafahamu tumetoka mbali, tumefika mbali na tunaelekea
mbali.
Niliomba nafasi ya urasi si kwa majaribio bali nataka niwatumikie
watanzania,” alisema. Aliongeza kuwa, anafahamu kwa dhati bila kubagua
vyama, makabila, wanataka mabadiliko kwa maana wanataka maendeleo na
Tanzania mpya.
Alisema alijipima kwenye moyo wake kwa kumtanguliza Mungu na anaamini
yuko tayari kuwapatia Tanzania mpya. Magufuli ambaye amekuwa
akisisitiza suala la amani, alipongeza marais waliotangulia kwa
kusimamia amani ya nchi na kuamini kuwa Tanzania ni moja.
Alisema yako mengi yamefanyika katika awamu zote. Lakini
yanawezekana, yaliyofanyika yanaweza yasionekane licha ya mengine kuwa
kwenye maeneo yao. Alieleza kushangazwa na baadhi ya watu kusema hakuna
chochote kilichofanyika.
Alielezea Chato ilivyokuwa na kusema kilikuwa kijiji na nyumba za
bati hazikuwa nyingi kama hizi. Alitaja pia barabara za lami hazikuwepo,
shule za msingi zilikuwa nne wakati sasa zipo zaidi ya shule 130.
“Lakini bado kuna mtu anaweza kusimama akasema haya yote ni ziro
tu…,” alisema na kuongeza kwamba wakati anasoma, sekondari haikuwapo
hata moja lakini sasa zipo shule zaidi ya 30. Alikumbusha namna ambavyo
wana Chato walivyokuwa wakishonana kwenye mabasi.
“Chato kilikuwa kijiji na leo ni wilaya…umeme Chato haukuwepo, na
sasa hivi tumeunganishwa na gridi ya taifa,” alisema na kuongeza kuwa
umeme unapelekwa kwenye kila kata. Akisisitiza kuwa wanaelekea mbali
kimaendeleo, Magufuli alisema si vyema kwa Mtanzania aliyeishi nchini
akaanza kuzungumza kuwa hakuna chochote bila kukumbuka hata uwapo wa
amani. “Wengine wanasema usihubiri amani.
Amani nitaihubiri siku zote,” alisema. Aliomba Watanzania wanaoipenda
nchi kuhubiri amani na kusema inafahamika nchi zinapokosa amani, hali
inakuwaje. Alitoa mfano wa Uganda, Kenya baada ya uchaguzi na Sudan ya
Kusini.
“Ndiyo maana mimi nina hofu ya Mungu, namuogopa Mungu na Watanzania,”
alisema. Hata hivyo alisema pamoja na mafanikio hayo, zipo changamoto.
Alisema anataka ashushe zaidi umasikini, ikiwa ni pamoja na kudhibiti
ushuru kwa wazalishaji wadogo wakiwemo bodaboda na mama lishe.
“Nataka watanzania walipe kodi, wakubwa walipe kodi, wa kati kati
walipe kodi, na wa chini walipe kodi kidogo,” alisema. Viwanda
Aliendelea kusisitiza kuwa anataka Tanzania iwe ya viwanda itakayotoa
ajira kwa vijana.
Alisema wataletwa wawekezaji kutoka nje na wa ndani watapewa fursa
bila kuwekewa vipingamizi. Alisema waliobinafsishwa viwanda waviendeleze
bila kufanya hivyo, moto wao uko karibu kwa kuwa watanyang’anwa. Alitoa
mfano wa kiwanda cha nguo cha Mwatex cha mkoani Mwanza.
Wakulima, wafanyakazi Alisema atahakikisha bei ya pamba anaipandisha.
Kuhusu mishahara ya wafanyakazi, alisema itaboreshwa kwa kuhakikisha
wanapunguza makato yasiyo ya msingi. Alisema pia wafanyakazi wanaofanya
kazi katika mazingira magumu, wataangaliwa. Pia ataangalia utofauti wa
mishahara baina ya wafanyakazi.
Alisema yeye ni rafiki wa wafanyakazi wanaofanya kazi na sio wale
wanaokosea mahali na kuhamishiwa maeneo mengine. “Kwangu hakuna hama
hama… utahamishwa tu kwamba unahama kwenda kufanya kazi kama kawaida na
si kuhamishwa kwa sababu umekosea... najua wafanyakazi wengi ni wazuri.
Wabaya ni wachache.
Najua wengine wamekuwa wakipita na kusema Magufuli ni mkali mno kwa
wafanyakazi,” alisema. Alisema hana tatizo na wafanyakazi kwa kuwa
amewahi kuwa katika nafasi hiyo ikiwamo kufundisha katika Shule ya
Sekondari ya Sengerema.
“Nimeuza maziwa, nimechunga ng’ombe, nimeuza furu..,” alisema na
kuongeza kuwa pia atakuwa rafiki wa wakulima. Wavuvi Alisema ushuru wa
mitumbwi utashushwa. Alisema itaanzishwa pia mipango mizuri ya kufuga
samaki kwa kuleta utaalamu.
Alitoa mfano wa nchi ya Vietnam kwamba inaongoza kwa kuwa na utaalamu
wa kufuga samaki. “Wanaonipiga vita ni wale mafisadi wanaoogopa jeuri
yangu…ndiyo maana mliona nilipoteuliwa tu kupeperusha bendera ya CCM
wamekimbia.
Wanafahamu nitawafunga magufuli,” alisema na kusisitiza kuwa atakuwa
Rais wa Watanzania asiyebagua vyama, dini wala makabila. Hakuna bure
Aliwaasa vijana kutambua kwamba hakuna vitu vitakavyokuja bure.
Alisisitiza umuhimu wa kuwaambia ukweli wananchi huku akitolea mfano
wa mgombea ambaye aliahidi kuwa akiwa rais, ndani ya siku chache
atahakikisha nyumba zote za nyasi zinatoweka.
Katika mkutano huo, msemo wa ‘Mcheza Kwao Hutuzwa’, ulidhihirika,
kwani kwenye Uwanja wa Michezo ujulikanao kama Uwanja wa Mama Zaina
ulifurika mno, ukikusanya idadi kubwa ya watu kwenye mji huo wa nyumbani
kwa Dk Magufuli.
Magufuli, ambaye ni Waziri wa Ujenzi, alifika nyumbani kwake juzi
akitokea mkoani Kigoma . Tangu kampeni zianze, mgombea huyo ameshafika
mikoa 13 na kuomba kura katika majimbo yote.
Ikiachwa mkoa wa Kigoma ambako Dk Magufuli alihitimisha kampeni zake
katika Wilaya ya Kakonko kabla ya kuja Chato, mikoa mingine
aliyokwishakamilisha kampeni ni Katavi, Rukwa, Mbeya, Njombe, Ruvuma,
Mtwara, Morogoro, Tanga, Mara, Simiyu na Tabora
Created by Gazeti Habari Leo
Monday, 21 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment