NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
OFISA wa Umoja wa Mataifa Kitengo cha Uchumi Afrika (UNECA),
Hopestone Chavula, ameishauri Tanzania kuzalisha bidhaa zenye viwango
ili kukwepa kuagiza vitu kutoka nje ya nchi.
Ushauri huo ameutoa jijini hapa jana wakati wa uzinduzi wa ripoti ya
utafiti wa maendeleo ya viwanda na biashara Afrika kwa mwaka huu
iliyofanyika katika Ukumbi wa Dar es Salaam Convention Center.
Chavula alisema watu wengi wamekuwa wakiamini bidhaa zenye ubora ni
zile zinazozalishwa nje ya nchi, hivyo kuzidi kudidimiza uuzwaji wa
malighafi za ndani jambo linalochangia viwanda kuzidi kufa.
“Licha ya kubaini kuwa yapo mambo mbalimbali yanayochangia kushuka
kwa hali ya biashara na viwanda nchini, kubwa ikiwa ni ukosefu wa
miundombinu bora kama barabara, umeme na maji, lakini bidhaa nyingi
kuingia kutoka nje ndio kumechangia zaidi,” alisema Chavula.
Alisema ripoti hiyo imebaini kuwa endapo wakulima watazalisha mazao
mengi kwa kiwango kizuri na wafanyabiashara wakaongezea thamani ya
malighafi zao huku Serikali ikifufua viwanda, kutasaidia kukuza biashara
na kuliingizia taifa pato kwa kuuza bidhaa nje ya nchi.
Alisema taifa litafikia wakati ambao litaacha kutumia vitu kutoka
nje. Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye viwanda nchini
(CTI), Samuel Nyantahe, alisema maendeleo yanategemea viwanda lakini kwa
sasa nchi
imevamiwa na bidhaa za nje hivyo inapaswa kufufua viwanda vilivyopo.
Alisema viwanda hivyo ni pamoja na vinavyoshughulikia kilimo, uchimbaji wa madini na zana nyingine na kuongeza ubora wa bidhaa.
“Lakini mpango huu ili ufanikiwe inabidi wafanyabiashara na wenye
viwanda kuungana kutatua tatizo na ndilo lengo la ripoti hii,” alisema
Nyantahe.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu waWizara ya Afrika Mashariki, Joyce
Mapunjo, alisema Serikali ipo kwenye mkakati wa kuandaa mpango wa miaka
mitano ambao utaweka mkazo kwenye sekta ya viwanda na kuvifufua.
Created by Gazeti la Mtanzania
Saturday, 26 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment