NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
BAADA ya timu ya TP Mazembe (DRC) wanayochezea Watanzania, Mbwana
Samatta na Thomas Ulimwengu, kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa
Afrika, sasa itakuwa na shughuli pevu kufika fainali baada ya kupangiwa
Waarabu.
Samatta ndiye aliyekuwa chachu ya Mazembe kufika hatua hiyo baada ya
kufunga mabao matatu ‘hat trick’, wakati miamba hiyo ilipoifunga Moghreb
Tetouan ya Morocco mabao 5-0 wikiendi iliyopita.
Mabao hayo yalimfanya Samatta kuondoa ukame wa kufunga mabao kwenye
mechi saba zilizopita, mara ya mwisho kufunga kwenye michuano hiyo
ilikuwa ni miezi mitano iliyopita walipoifunga Mamelodi Sundowns (Afrika
Kusini) 3-1 Aprili 5.
Mazembe sasa ina mtihani mwingine mgumu zaidi ili kutwaa kombe hilo,
kwani imepangwa kucheza na timu za Kiarabu, El Merreikh ya Sudan kwenye
nusu fainali na ikiitoa italazimika kupambana na mshindi wa nusu fainali
nyingine kati ya Wasudan wengine, Al Hilal na U.S.M Alger ya Algeria.
Akizungumza na MTANZANIA kutoka nchini humo jana, Samatta alikiri
ugumu kwenye mchezo huo kutokana na kocha wa El Merreikh, Diego
Garzitto, kuwahi kuinoa Mazembe kwa mafanikio mwaka 2003-2004 na
2009-2010.
“Kuna sababu mbili au tatu za ugumu, kwanza kocha wao anatufahamu.
Pia tumeshawahi kukutana nao mara kadhaa. Pia kuna upinzani wa kimpira
kati ya klabu za Kongo na Sudan kwa miaka ya hivi karibuni,” alisema.
Samatta pia aliizungumzia ‘hat trick’ yake ya hivi karibuni na kusema
kuwa: “Najisikia furaha kwanza mimi binafsi kwa kuwa mmoja wa wachezaji
walioweka rekodi ya kufunga hat trick, pia kwa kuiwezesha timu yangu
kuingia kwa kishindo nusu fainali.”
TP Mazembe kwa sasa imepania nasaka kurudia rekodi ya mwaka 2010,
walipotwaa ubingwa wa Afrika na kufika fainali ya Kombe la Dunia la
klabu na kufungwa na Inter Milan ya Italia mabao 3-0.
Created by Gazeti la Mwananchi
Wednesday, 16 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment