NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van Pluijm, amesema haofii lolote
kuelekea mechi dhidi ya hasimu wake, Simba Jumamosi hii kwenye Uwanja wa
Taifa Dar es Salaam huku akitamba yupo tayari kwa vita ya kuwachakaza
wekundu hao.
Msimu huu pambano hilo limetabiriwa kuwa litakuwa ni la kukata na
shoka kutokana na timu hizo kupata matokeo ya ushindi kwenye mechi za
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) walizocheza mpaka sasa.
Yanga iliyo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi tisa sawa na Simba, Azam
na Mtibwa Sugar zinazofuatia imeshinda mechi zake zote dhidi ya Coastal
Union (2-0), Tanzania Prisons (3-0) na juzi ikailaza JKT Ruvu 4-1 zote
ikicheza Uwanja wa Taifa.
Pluijm aliliambia MTANZANIA kuwa anauchukulia kawaida mchezo huo na
hata maandalizi yake atakayofanya ni sawasawa na yale atakayofanya
wakati akicheza na timu nyingine.
“Kwangu mimi ni mechi ya kawaida kama nyingine, lakini huwa na
mashabiki wengi zaidi, vile vile ni kama vita kama usipoua, basi
utauliwa wewe. Tutafanya maandalizi yetu kawaida kama kwenye mechi
nyingine.
“Binafsi naamini ya kuwa tutacheza mpira wetu mzuri kwani timu
inapofanikiwa kumiliki mpira, kufanya mambo yote uwanjani kwa kasi na
umakini, tutaiweka Simba pabaya na kuipa wakati mgumu kwenye mchezo
huo,” alisema.
Mholanzi huyo tokea aanze kuifundisha Yanga, hajawahi kupata ushindi
kwenye mechi zote mbili alizocheza dhidi ya Simba, alitoa sare ya bao
1-1 msimu wa 2013-14 kabla ya kufungwa 1-0 msimu uliopita, mara zote
hizo alikabidhiwa timu hiyo kwenye mechi za mzunguko wa pili.
Pluijm aligoma kuzungumzia rekodi yake hiyo mbaya dhidi ya Simba
akidai kuwa: “Hiyo ni historia na sitaki kuangalia huko, ninachoangalia
ni hiki kilichoko mbele yangu. Niweke wazi kuwa siiogopi Simba na hata
timu nyingine yoyote, lakini zote naziheshimu.”
Hata hivyo, Pluijm akizungumzia ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya JKT
Ruvu alisema bado vijana wake hawajacheza katika kasi anayoihitaji,
wamekuwa wakicheza kasi ya chini lakini akadai huo ni mwanzo tu na timu
yake imekuwa ikiimarika kadiri siku zinavyosogea.
Created by Gazeti la Mtanzania
Monday, 21 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment