Ndugu wa karibu na watoto wa aliyekuwa waziri wa nchi, ofisiya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani wakitoa
heshima zao za mwisho kwa mwili wa marehemu wakati wa ibada ya kumuaga
iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee, Dae es salaam.
MAKAMU wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal jana aliongoza mamia ya
Watanzania waliojitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
Mwili wa Kombani uliagwa katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam
huku idadi kubwa ya watu wakiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph
Warioba, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, Mawaziri, Manaibu Mawaziri,
viongozi wa vyama vya siasa na wabunge wakihudhuria.
Jeneza lenye mwili wa marehemu liliwasili katika viwanja hivyo majira
ya saa 5:00 asubuhi, likiwa limebebwa na askari wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania waliokuwa wamevalia suti nadhifu huku
wakisindikizwa na Mawaziri na Manaibu Mawaziri hadi kwenye jukwaa.
Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama alisema, serikali imepata pigo
kubwa kutokana na kifo cha Kombani kwani alikuwa ni kiongozi aliyekuwa
mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya taifa kupitia wajibu wake na
majukumu aliyopewa na serikali.
Alisema pengo aliloacha Kombani haliwezi kuzibika kirahisi kwani
mchango wake ulikuwa ukihitajika kwa ajili ya kuendeleza harakati za
kuleta maendeleo ya taifa. “Alijitahidi kuwapigania wananchi wa jimbo
lake, hakuna ubishi alifanya kazi kubwa kwa wananchi wa jimbo lake.
Amefanya mageuzi makubwa katika sekta ya utumishi na atakumbukwa
daima,” alisema Mhagama. Awali akizungumza, Spika wa Bunge, Anne Makinda
alisema, Kombani aliwasaidia kuunda muundo mpya wa utumishi wa Bunge
ambapo alisema, Agosti 16, mwaka huu walipitia muundo huo kwa mara ya
mwisho ambapo Kombani alishiriki.
Alisema wakiwa katika kikao hicho Kombani alitoka nje na baada ya
muda alipewa taarifa kuwa anajisikia vibaya. “...Kwa kuwa nilikuwa
Mwenyekiti wa kile kikao nikapewa taarifa kuwa Waziri anajisikia vibaya
nikawa nimeshangaa kwa sababu tulikuwa naye yuko vizuri, nikawa nimetoka
kwenda kumuona,” alisema.
Alisema wakati wakiwa hapo Katibu wa Bunge alimwambia kuwa Waziri
anataka apelekwe kwa daktari wake ambapo alipelekwa kwa daktari huyo
katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni. Aliwataka waliohudhuria tukio
hilo kuchukulia kifo cha Kombani kama somo la kutenda mema kama
ilivyokuwa kwa Waziri huyo.
Akitoa salamu za uliokuwa Umoja wa Wabunge Wanawake, Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angellah Kairuki alisema, bado
mchango wa waziri huyo ulikuwa ukihitaji kwani alikuwa ni mshauri mzuri
katika mambo mbalimbali ya umoja huo pamoja na Bunge kwa ujumla.
Alisema umoja huo ulipokea kifo chake kwa mshtuko mkubwa kwani
hawakutegemea kama wangempoteza mapema kiasi hicho na hasa katika
kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi ambapo pia alikuwa anatetea jimbo
lake la Ulanga Mashariki.
Mwili huo jana ulisafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya
maziko ambapo kwa mujibu wa ratiba ya maziko, leo mwili huo unatarajiwa
kuwasili katika uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya sala kabla ya kwenda
kuhifadhiwa katika nyumba yake ya milele.
Katika sala hiyo itakayofanyika uwanjani hapo, inatarajiwa
kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Rais Dk Bilal,
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Bunge
Makinda na viongozi mbalimbali.
Kombani alifariki Septemba 24, mwaka huu katika Hospitali ya Apollo
nchini India na anatarajiwa kuzikwa shambani kwake, Lukobe, nje kidogo
ya mji wa Morogoro.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 29 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment