Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kutoshangazwa na matokeo ya
utafiti wa taasisi huru ya Twaweza yaliyotoa ushindi wa asilimia 65 kwa
Mgombea Urais wao, Dk John Magufuli, huku kikiahidi kuongeza kasi, nguvu
na mikakati zaidi katika nusu ya pili ya kampeni.
Hata hivyo, kimeshangazwa na taharuki hasa kutoka miongoni mwa wasomi
na wanaharakati, kuhusu matokeo ya utafiti huo na kusema kilitegemea
wasomi na wanaharakati hao wangefurahia utamaduni wa tafiti za kisiasa
ulioanza kujitokeza nchini kwa vile unajenga.
Pia kimesisitiza kuwa kimethibitisha kushiriki mdahalo wa wagombea
urais ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), lakini kikisitiza
uwashirikishe wagombea wenyewe na si wawakilishi wao, na pia wagombea
wote, hasa wa vyama vikuu wawepo na washiriki.
Juzi, Taasisi ya Twaweza ilitoa matokeo ya utafiti wake kuhusu ‘Sauti
za Wananchi’ kwenye siasa na kuonesha kuwa, kama uchaguzi huo
ungefanyika juzi, Dk Magufuli angeibuka mshindi wa asilimia 65 na
Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa
ambaye ana asilimia 25.
Pia Twaweza katika utafiti huo, ilisema wahojiwa hao walipoulizwa
wanajisikia kuwa karibu zaidi na chama gani, asilimia 62 walisema wako
karibu na CCM huku Chadema ikipata asilimia 25 na vyama vingine
vikiambulia asilimia zilizobaki.
Katika utafiti huo uliofanywa mapema Agosti hadi Septemba mwanzoni
mwaka huu, wahojiwa waliulizwa swali ni mgombea yupi watampigia kura na
kwa nini, na majibu yalikuwa asilimia 26 walisema watampigia Magufuli
kwa sababu ni mchapakazi huku asilimia 12, walisema watampigia Lowassa
kwa sababu ya kutaka mabadiliko.
CCM haikushangazwa
Akizungumzia matokeo hayo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
(NEC) ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba
alisema CCM haikushangazwa na matokeo ya utafiti huo ambao umeibua
mjadala mkubwa miongoni mwa jamii wakiwamo wasomi na wanaharakati.
“Hatukushangazwa na matokeo ya utafiti huu kwa sababu tano; moja;
siku Ukawa walipomteua Lowassa kuwa mgombea wao ndio siku CCM
ilipohakikishiwa ushindi katika uchaguzi wa mwaka huu.
CCM hatukumteua kwa sababu tuliamini hakuna namna ambapo Watanzania
wengi watamchagua,” January aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es
Salaam. Aliitaja sababu ya pili kuwa CCM inafanya utafiti wa ndani wa
kisayansi kila wiki kujua mwenendo na mwelekeo wa kampeni na maeneo
yanayohitaji nguvu mahsusi na kwamba tangu utafiti huo uanze mwishoni
mwa Agosti, karibu kila wiki asilimia za ushindi wa CCM hazijawahi
kushuka chini ya asilimia 60 na zimekuwa zikipanda.
Tatu; alisema kazi kubwa anayofanya mgombea wa CCM, Magufuli na
Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan, kuzunguka nchi nzima kwa barabara na
kuzungumza moja kwa moja na wapiga kura inazaa matunda kutokana na
kuwafikia wapiga kura wengi, hasa wa vijijini, na wapiga kura
wanawaelewa.
Aliitaja sababu ya nne kuwa ni kutokana na kampeni kubwa zinazofanywa
na wagombea ubunge na udiwani wa CCM na makada na viongozi wa chama
hicho katika ngazi zote za nchi nzima kila siku kumuombea kura Magufuli,
na kampeni hizo kuzaa matunda.
Kuhusu sababu ya tano, January alisema “Tunaamini pia migogoro ndani
ya Ukawa katika kipindi hiki cha uchaguzi iliyopelekea mitafaruku katika
kuachiana majimbo na baadaye, kutokana na uteuzi wa Mgombea Urais wa
Ukawa, kusababisha kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Lipumba na Dk Willbrod
Slaa, na migongano ndani ya NCCR- Mageuzi, ambayo yote yamepunguza imani
ya wananchi kwa vyama hivyo.”
Taharuki ya wasomi Akizungumzia wasomi, January ambaye pia ni Mgombea
Ubunge Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, alisema CCM imeshangazwa na
taharuki hasa kutoka miongoni mwa wasomi na wanaharakati kuhusu matokeo
ya utafiti huo.
“CCM ilitegemea kwamba jamii ya wasomi na wanaharakati ingefurahia
utamaduni wa tafiti za kisiasa unaoanza kujitokeza hapa nchini ili siku
zijazo tujikite katika kurekebishana kwenye kanuni za utafiti na
ithibati na uhakiki wa ubora,” alieleza January na kutoa mfano wa
utafiti wa Sinovate mwaka 2010 ambao ulionesha kuwa Rais Jakaya Kikwete
angeshinda kwa asilimia 61, na kweli akapata asilimia 61.17 kushinda
muhula wa pili na wa mwisho.
“Tunasikitika kwamba yanawekwa mazingira ya kutisha na kukatisha
tamaa kwa watu wanaotaka kufanya tafiti za kisiasa nchini. Utafiti ni
sayansi, na matokeo ya utafiti hupingwa kwa matokeo ya utafiti mwingine,
si kwa kuponda tu au kwa matusi na vitisho.
Ni vyema tukajifunza kupokea habari ambayo haikufurahishi bila
taharuki.” Kasi, mikakati kuongezeka Akizungumzia mwenendo wa kampeni,
January alisema CCM inaridhika na mwenendo wa kampeni, na katika nusu ya
pili ya kampeni itaongeza kasi na msukumo wa kuwafikia wananchi wengi
zaidi kwa mbinu na mikakati mipya.
“Kwa kifupi, mgombea Urais Magufuli na mgombea mwenza Samia,
wanaendelea vizuri na kampeni. Kila mmoja anafanya mikutano na wananchi
kati ya minane na 11 kwa siku na kukutana na maelfu kwa maelfu ya
wananchi.
“Tunawashukuru pia makada wa CCM wanaojitolea kwa hali na mali
kukipigania Chama Cha Mapinduzi na kumtafutia kura Ndugu Magufuli,”
alisema. Midahalo ya wagombea Kwa upande wa midahalo ya wagombea,
alisema CCM imeshangazwa na kauli ya Baraza la Habari Tanzania (MCT)
kupitia kwa Katibu Mtendaji wake, Kajubi Mukajanga kwamba CCM
haijathibitisha kushiriki mdahalo.
Akifafanua kilichotokea, January alisema; “CCM ilipokea mwaliko wa
MCT na kuijibu kwa barua ya tarehe 13 Septemba 2015 yenye kumbukumbu
CCM/ OND/M/190/132 iliyosainiwa na Stephen Msami ambaye ni Msaidizi wa
Katibu Mkuu, ikithibitisha kushiriki mdahalo.”
Alisema mbali ya hatua hiyo; CCM ilithibitisha kushiriki mdahalo huo
kupitia vikao mbalimbali na kwamba kauli ya Mukajanga inalenga
kuwasaidia kisiasa wale ambao hawajathibitisha au hawana nia ya
kuthibitisha kushiriki.
“Kwa msingi huu, tunaamini ni vyema mdahalo huu ukaandaliwa na
ushirika wa taasisi mbalimbali zilizokuwa na nia ya kuandaa midahalo
kama vile UDASA, Twaweza na nyinginezo ili kuiondolea uwezo taasisi moja
au kikundi cha watu wachache, kuhodhi na kuwa na ukiritimba kwenye
jambo hili kubwa na muhimu.
“CCM inapenda kusisitiza kwamba Magufuli amekubali kushiriki mdahalo
wa wagombea Urais, mdahalo uwashirikishe wagombea wenyewe na si
wawakilishi wao na wagombea wote, hasa wa vyama vikuu, wawepo na
washiriki,” alisema January.
ACT yafarijika Kwa upande wake, Chama cha ACTWazalendo kimesema mbali
ya kuchelewa kutangaza wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, lakini
kinafarijika kuwa chama pekee nje ya vyama vingine vya siasa kutajwa na
wapiga kura zaidi ya asilimia moja katika matokeo ya utafiti wa
Twaweza.
Kimesema kupitia utafiti huo, chama hicho kimeonekana kuwa cha nne
katika kukubalika kwa wapiga kura nyuma ya CCM, Chadema na CUF.
Kadhalika kimesema hadi sasa kimekusanya fedha Sh milioni 365 na kutumia
Sh milioni 363 huku kikiri kuwa na upinzani mkubwa katika majimbo 89
wakihitaji nguvu ya ziada.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi na
Kampeni Taifa, Nixon Tugara alisema katika utafiti wa Twaweza unaonesha
kuwa chama hicho hakikufanya vizuri na kwamba bado wana kazi kubwa ya
kuwafikia wapiga kura katika muda uliobakia wa kampeni.
“Licha ya kuonesha hali hiyo, sisi ACT Wazalendo tunafarijika kwamba
chama kimekuwa chama pekee nje ya CCM na vyama vinavyounda Ukawa
kilichotajwa na wapiga kura,” alisema Tugara.
Alisema kutokana na kufanya vizuri katika kampeni na bidii kubwa
ambayo mgombea urais wa chama hicho na wagombea wengine wamekuwa
wakifanya, wanaamini kuwa utafiti ungefanyika leo wangefanya vizuri
zaidi.
Tugara alitoa mwito kwa wagombea wa chama hicho popote walipo
kuchukulia matokeo ya utafiti huo kama changamoto ya kuongeza bidii
zaidi katika kampeni zao. Kadhalika aliwahimiza wagombea na makampeni
meneja na viongozi wa chama kuwekeza nguvu zaidi kwa makundi ya wananchi
ambayo katika utafiti huo yanaonekana bado kuunga mkono chama tawala.
Alitoa mwito kwa taasisi nyingine kufanya tafiti nyingine kabla ya
Uchaguzi Mkuu kwa kuwa wanatambua utafiti ni moja ya maoni ya wananchi
kuhusu siasa, ingawaje hawawezi kubashiri hali itakavyokuwa siku ya
uchaguzi.
Kuhusu kampeni alisema tayari uongozi wa chama hicho umefika mikoa
zaidi ya 10 na kuendelea kuwa na mtandao mpana hali ambayo ilisababisha
kusimamisha wagombea wengi zaidi ya vyama vingine ukiondoa CCM.
Imeandikwa na Oscar Mbuza na Lucy Lyatuu.
Created by Gazeti la Habari Leeo
Thursday, 24 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment