Kikosi cha Yanga. |
ILIKUWA miezi, mwezi, wiki, siku na sasa ni saa kabla ya vigogo vya soka Tanzania Bara vya Simba na Yanga kuchuana katika moja ya mechi za Ligi Kuu kwenye mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Tofauti na mara nyingi zinapokutana, leo timu hizo zinashuka dimbani zikiwa zinalingana kwa pointi wakati Yanga iko kileleni ikiwa inaongoza kwa tofauti ya mabao tu, huku kila moja ikiwa na pointi tisa.
Si Simba na Yanga tu zenye pointi tisa, Azam FC na Mtibwa Sugar, nazo zina idadi kama hiyo ya pointi na hivyo kufanya raundi ya nne kuwa na mvutano wa aina yake. Makocha wa pande zote mbili wametamba kuibuka na ushindi katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka hapa nchini na hata nje ya Tanzania.
Kocha wa Yanga, Hans van de Pluijm alisema kuwa mazoezi ya timu yake katika kisiwa cha Pemba yameisaidia timu hiyo kutokana na utulivu wa kisiwani humo. Pluijm anataka kuvunja mwiko wa timu hiyo kusumbuliwa na Simba katika kipindi cha hivi karibuni licha ya Yanga kuonekana bora zaidi, ukilinganisha na vijana hao wa Msimbazi.
Kocha wa Simba ambaye hii ni mechi yake ya kwanza dhidi ya Yanga, Muingereza Dylan Kerr ametamba kuwa lolote litakalokuwa, Yanga lazima wakae. Kerr, ambaye kikosi chake kilipiga kambi Unguja amesema kuwa amewapanga vizuri vijana wake ili kuhakikisha leo wanaoondoka na pointi zote tatu na kuwafurahisha wapenzi na mashabiki wao.
Mbali na makocha, wapenzi, mashabiki na wachezaji nao wamekuwa wakitambiana huku kila upande ukitamba kuwa wataibuka washindi na kuwalaza mapema wapinzani wao baada ya dakika 90.
Mshauri wa ufundi wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Abdallah Kibadeni alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, Yanga wataibuka washindi katika mchezo huo kutokana na ubora wa timu yao kwa sasa.
Kibadeni mbali na kuwahi kuwa mchezaji anayeshikilia rekodi ya kuwafunga Yanga hat-trick, pia aliwahi kuwa kocha wa timu hiyo mara kadhaa na ile ya Taifa. Simba ambao ni wenyeji katika mchezo huu wa leo, walishinda mechi zao tatu kwa kuzifunga African Sports 1-0 na Mgambo JKT 2-0 zote katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kabla ya kuifunga 3-1 Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa.
Licha ya kucheza kwenye uwanja inaotumia kama wa nyumbani, Yanga leo ni wageni na walishinda mechi zao tatu katika uwanja huo wakiwa wenyeji. Yanga waliwachapa 2-0 Coastal na baadae walishinda 3-0 dhidi ya Prisons kabla ya kukutana na JKT Ruvu kwa kuipiga 4-1.
Kwa upande wa mabao ya kufungwa, timu zote mbili zimefungwa bao moja na hivyo kuonesha ugumu wa safu zao za ushindi lakini kwa ushambuliaji, Yanga haina mpinzani baada ya kufunga mabao tisa wakati wenzao wamefunga mabao sita tu.
Simba wanaonekana kumtegemea sana Hamisi Kiiza aliyefunga mabao matano hadi sasa wakati Yanga ina wafungaji kama Amissi Tambwe na Donald Ngoma ambao kila mmoja amefunga mabao matatu.
Katika safu ya kiungo, Yanga inatarajiwa kuwa na akina Haruna Niyonzima, Thabani Kamosoko huku Simba huenda ikawategemea Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto na wengineo. Simba imepata pigo baada ya kocha wake wa mazoezi ya viungo, Dusan Marmcilovic kutimka siku chache kabla ya pambano hilo kwa madai ya kutoelewana na bosi wake.
Hata hivyo, uongozi wa Simba umedai kuwa kocha huyo aliondoka baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa miezi mitatu wa kuinoa timu hiyo. Viingilio vya mchezo huo ni Sh 7,000, wakati kiingilio cha juu ni Sh 30,000 kwa viti vya VIP A, Sh 20,000 kwa viti vya VIP B & C.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi wa kimataifa mwenye beji ya FIFA, Israel Nkongo (Dar es Salaam) akisaidiwa na Josephat Bulali (Tanga), Ferdinand Chacha (Mwanza), mwamuzi wa akiba Soud Lila (Dar es Salaam) wakati kamishna wa mchezo huo atakuwa Charles Mchau kutoka Kilimanjaro.
Michezo mingine ya Ligi Kuu leo ni Coastal Union dhidi ya Mwadui FC katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Maafande wa jeshi la Magereza (Tanzania Prisons) watawakaribisha maafande wa Mgambo Shooting katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mechi zingine ni JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Stand United katika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, huku wakata miwa wa Turiani Mtibwa Sugar watawakaribisha Majimaji ya Songea katika Uwanja wa Manungu wakati Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Toto Africans katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Kesho Jumapili Azam FC watawakaribisha Mbeya City katika Uwanja wa Chamazi Complex, huku African Sports wakiwa wenyeji wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga
Created by Gazeti la HabariLeo
0 comments:
Post a Comment