Kigoma. Idadi ya wakimbizi kutoka Burundi
wanaokimbia nchi yao na kuingia nchini Tanzania imefikia 91,661 hadi
kufikia jana Jumanne. Wakimbizi hao kwa sasa wamehifadhiwa katika Kambi
ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Taarifa
ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa vyombo vya habari inasema kuwa tangu
wakimbizi hao waanze kuingia nchini mwezi Aprili mwaka huu, wizara hiyo
kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi
(UNHCR) na wadau wengine wameendelea kupokea wakimbizi na kwamba
wanawapa hifadhi na huduma nyingine muhimu.
“Hali ya
ulinzi na usalama katika Kambi ya Nyarugusu na maeneo yanayoizunguka
imeimarika ambapo upo usalama wa kutosha,” inasema taarifa hiyo na
kuongeza:
“Kazi hii inafanywa na polisi kwa
kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi vinavyojumuisha baadhi ya
wakimbizi wanaoishi katika kambi hii.”
Kwa mujibu wa
taarifa hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa Mambo ya Ndani, Isaac Nantanga,
serikali kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS)
imeimarisha huduma hizo kwa kuongeza idadi ya watendaji, vifaa na dawa.
Pia
inasema huduma za afya zimeimarishwa ambapo hali hiyo imesaidia
kudhibiti magonjwa ya mlipuko na kukabiliana na magonjwa mengine yasiyo
ya mlipuko.
“Kabla ya kufikia idadi hii ya sasa, wengi
wa wakimbizi walianza kuingia kwa maelfu kupitia kijiji cha Kagunga
kilichopo mpakani na nchi ya Burundi ambapo idadi ilianza kupungua
kidogo lakini kwa siku za hivi karibuni wakimbizi wameendelea kuingia
wakiwa katika vikundi vidogovidogo,” inasema taarifa hiyo.
Created by Gazeti la Mwananchi
Created by Gazeti la Mwananchi
0 comments:
Post a Comment