NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete na mwenzake Yoweri Museveni wa nchini
Uganda, wamekutana jijini New York, Marekani na kujadili mambo
mbalimbali ikiwemo maendeleo ya uchimbaji wa mafuta yanayopatikana
nchini Uganda.
Marais hao walikutana juzi katika Hoteli ya Trump International and
Tower iliyopo jijini humo ambako viongozi hao wapo huko ili kuhudhuria
shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
ilisema mbali na hilo pia viongozi hao walizungumzia uhusiano kati ya
nchi hizo mbili pamoja na masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
ambako nchi hizo ni wanachama.
“Miongoni mwa mambo ambayo viongozi hao walizungumzia ni maendeleo ya
uchimbaji mafuta nchini Uganda na faida za mafuta hayo kwa Tanzania na
kwa nchi zote wanachama wa EAC, wakati mafuta hayo yatakapoanza
kutumika,” ilisema taarifa hiyo.
“Rais Kikwete na Rais Museveni pia walipata nafasi ya kujadiliana
kuhusu hali ya kisiasa Afrika na jinsi gani inavyoweza
kuimarishwa katika baadhi ya nchi,” ilisema taarifa hiyo.
Katika mazungumzo hayo, Kikwete na Museveni walijadili pia hali ya
kisiasa nchini Burundi ambako rais huyo wa Uganda ndiye aliyepewa jukumu
na viongozi wenzake wa EAC kusimamia mazungumzo ya kuleta maelewano na
maridhiano.
Burundi pia ni mwanachama wa EAC ambayo Mwenyekiti wake ni Rais Kikwete.
“Mbali na hilo, viongozi hao walijadili hali ya kisiasa na kiusalama
ilivyo katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na
juhudi zinavyoweza kufanyika kusaidia kuboresha hali hiyo hasa kwa
kutilia
maanani kuwa Tanzania inayo majeshi ya kulinda amani nchini humo,” ilisema taarifa hiyo.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Sam Kutesa ambaye ni Waziri
wa Mambo ya Nje wa Uganda anayemaliza muda wake na Rais wa Baraza Kuu
la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Tuvako Manongi ambaye ni
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa Mataifa.
Created by Gazeti la Mtanzania
Saturday, 26 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment